Kivuko chazama Moro, 31 wanusurika kifo

Wakazi wa Kilombero mkoani Morogoro wakiangalia kivuko cha MV Kilombero ll baada ya kukumbwa na dhoruba na baadaye kupinduka. Kivuko hicho kinasadikiwa kilikuwa na watu kati ya 35-50 na 31 wameshaokolewa. Picha na Juma Mtanda

Muktasari:

Mhagama alisema kila juhudi zinafanyika ili kuokoa mali na watu kwenye kivuko hicho.

Kilombero. Kivuko cha Mto Kilombero ‘MV Kilombero ll’, kinachosadikiwa kuwa kilibeba kati ya watu 35 na 50, juzi usiku kilipinduka baada ya kusukumwa na upepo mkali uliosababisha kigonge kingo ya daraja la muda.

Jeshi la Polisi lilieleza kuwa watu wawili waliokuwamo kwenye kivuko ambao hadi sasa hawajapatikana ni Dustin Wasira na mtu mwingine ambaye jina lake halikupatikana na kwamba wanaendelea na jitihada za kutafuta abiria wengine.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Vijana, Ajira na Walemavu), Jenista Mhagama, alitoa taarifa bungeni kuwa hadi jana asubuhi watu 30 kati ya 31 waliokuwemo kwenye kivuko hicho walishaokolewa.

Mhagama alisema kila juhudi zinafanyika ili kuokoa mali na watu kwenye kivuko hicho.

Alisema Serikali ilipokea taarifa za kuzama kwa kivuko hicho, usiku wa kuamkia jana na kwamba mbali ya watu, kulikuwa na magari matatu, bajaji mbili pamoja na mizigo mingine.

Kabla ya kuzama kivuko hicho, kilipoteza mwelekeo kutokana na dhoruba iliyosababishwa na upepo mkali na kusombwa umbali wa mita 40, kutoka eneo la njia ya kuu.

Akizungumza na Mwananchi katika mji mdogo wa Ifakara, mmoja wa waokoaji, Stanley Mlongola (33) alisema kazi ya kuokoa abiria ilikuwa ngumu kutokana na wengi kung’ang’ania kupanda boti moja ya iliyokuwa ikitumika kwa uokoaji.

Mlongola ambaye anafanya kazi ya kuvusha abiria kwa kutumia boti ndogo, alisema alishuhudia MV Kilombero 11 ikipoteza mwelekeo baada ya kusukumwa na dhoruba, kisha kugonga nguzo za daraja la muda la Wachina lililoko pembeni ya njia kuu ya kivuko hicho.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa aliyefika eneo la tukio jana  mchana, alisema Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa za ajali hiyo na kuahidi kuangalia namna ya kurejesha mawasiliano kati ya Ulanga na Kilombero.

Naye Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Mhandisi Magreth Mapela alisema MV Kilombero 11 kina uwezo wa kubeba tani 50 za mizigo  na abiria  kati ya 100 hadi 150, kwa wakati mmoja.

“Tulipata  taarifa kutoka kwa nahodha amenieleza kuwa watu waliopanda katika kivuko hicho ni kati ya 30 na 35, lakini mpaka sasa hivi bado hatujapata maafa.” alisema Mapela.

Mmoja wa abiria hao, Habiba Ngakongwa alisema nahodha wa kivuko hicho alipambana na tufani kwa zaidi ya dakika 50, kabla ya kuzidiwa nguvu na kuvutwa na maji na kugonga nguzo za daraja la muda la Wachina.

“Tulitangaziwa  kivuko  kupoteza mwelekeo na nahodha akatusihi tuvae maboya ya kujiokoa  na asiwepo mtu wa kuruka kutoka ndani ya kivuko,” alisema Habiba.

Magari yaliyozama ni pamoja na Mitsubishi Fuso, Toyota Land Cruiser mbili ikiwamo mali ya Benki ya CRDB tawi la Ifakara na nyingine ya kampuni ya Mitiki (KVTC). Baadhi ya watumiaji  wa kivuko hicho walilalamikia hitilafu za mara kwa mara za kivuko hicho, hivyo kuiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la kipekee wananchi wa wilaya za Ulanga na Kilombero.

Richard Lucas alisema ni vyema Serikali ikaharakisha ujenzi wa daraja katika eneo hilo ambalo umesimama.

Hafidh Mohamed na Ally Mohamed, wakazi wa Kilombero walisema kivuko hicho ndiyo tegemeo la la wakazi wa wilaya hizo, ambao wengine wamekuwa wakifanya shughuli za kibiashara  katika pande hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul  alisema taarifa zaidi zitaendelea kutolewa wakati juhudi za kutafuta watu wengine na kukiopoa zinazofanywa na wananchi, vikosi vya uokozi vya ulinzi na usalama zikiendelea.

Mkuu wa kivuko hicho, Mhandisi Fadhir Haroub alisema wakati kivuko kikipata ajali kilikuwa katika safari ya mwisho kutoka Ulanga kwenda Ifakara.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge,Vijana, Ajira na Walemavu),  Jenista Mhagama alisema bungeni juhudi zinafanyika  kuokoa abiria na mali  zilizokuwamo kwenye kivuko hicho.

Mhagama alisema Serikali ilipokea taarifa za awali za kuzama kwa kivuko hicho usiku wa kuamkia jana zikieleza  kulikuwa na abiria 31, magari matatu, bajaji mbili na mizigo.

Awali Naibu Spika wa Bunge,  Dk Tulia Akson: “Serikali ilipokea taarifa hizo usiku wa kuamkia leo (jana) na Waziri Mkuu alimuagiza Waziri wa Ujenzi kwenda eneo hilo mara moja kuongeza nguvu katika uokoaji na kutafuta mawasiliano ya Kilombero na Ulanga ambayo yamekatika,” alisema Mhagama.

Alihiadi Serikali kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na tukio hilo na kuwaomba wananchi kuwa watulivu wakati juhudi mbalimbali zikiendelea.