Ajiua kwa kunywa sumu kisa kufukuzwa kwa mpenzi wake

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, SACP Nicodemus Katembo.

Muktasari:

  • Kijana Hamis Lidonge amejiua kwa kunywa sumu baada ya kukataliwa na kufukuzwa nyumbani na mpenzi wake kisa wivu wa mapenzi.

Mtwara. Kijana mmoja mkazi wa kijiji cha Ukombozi kilichopo katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Hamis Lidonge (31) amejiua kwa kunywa sumu baada ya kukataliwa na mpenzi wake.

Akizungumzia tukio hilo leo Februari 17, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, SACP Nicodemus Katembo amesema uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini chanzo cha kijana huyo kujiua kuwa ni wivu na migogoro baina yao.

SACP Katembo amesema kuwa zimefanyika jitihada za kuokoa maisha ya kijana huyo lakini hazikufanikiwa ambapo alifariki dunia akiwa nyumbani.

Mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu zake baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kubainika kuwa kifo hicho kilisababishwa na kunywa sumu.

“Niwasihi wananchi kutumia njia sahihi za kutatua migogoro na matatizo katika familia zenu na uhusiano wenu kwa kushirikisha ndugu, jamaa na marafiki ili waweze kuwasaidia kuyamaliza ili yasilete madhara,” amesema Katembo.

Kwa upande wake, Athumani Mchanga (baba mdogo wa marehemu) amesema kijana huyo amekuwa akiishi nyumbani kwa mpenzi wake, ambapo siku tatu kabla ya kifo chake alishangaa kumuona amerudi nyumbani kwao.

Amesema kitendo cha kurudi kwao kilisababisha amuulize ambapo alimweleza kuwa amefukuzwa na huyo mpenzi wake.

“Mimi niligundua kuwa amekunywa sumu baada ya kuanza kutapika matapishi ambayo yalikuwa na harufu ya sumu, kitu ambacho kilinishangaza. Tulianza jitihada za kumuwahisha hospitali ili kuokoa maisha yake, hata hivyo hatukufanikiwa, akawa tayari amefariki,” amesema Mchanga.

Kwa upande wake, Rashidi Manzi Nngoni ambaye ni mzee wa kijiji hicho, amesema kitendo alichokifanya kijana huyo siyo kizuri kwa kuwa ameacha mtoto mdogo ambaye alikuwa akimtegemea.

“Sio vizuri kujiua, ni dhambi kubwa kufanya hivyo hata vitabu vya dini vinakataza, yeye angekaa na watu wazima wamsaidie kutatua tatizo hilo badala ya kuchukua uamuzi huo,” amesema Nngoni.