Mwalimu Mkuu adaiwa kujiua kwa sumu

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga

Muktasari:

  • Mwalimu huyo anadaiwa kujiua kwa kinachodaiwa kuwa ni msongo wa mawazo, baada ya kupokea fedha za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya kuchonga kibao cha klabu ya rafiki katika shule ya sekondari Mtanila iliyopo wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya.

Mbeya. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtanila, iliyopo Kijiji cha Igagwe, Wilaya ya Chunya mkoani hapa, Magwira Nkuta (41), amefariki dunia baada ya kunywa kimiminika kinachodhaniwa kuwa ni sumu, kutokana na msongo wa mawazo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema leo Septemba 16, 2023 kuwa marehemu alifikwa na umauti, Septemba 13 majira ya saa 1:30 asubuhi akiwa ndani ya nyumba anayoishi shuleni hapo.

Imeelezwa kuwa awali marehemu alitumiwa fedha kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa ajili ya kuchonga kibao cha klabu ya wanafunzi ya Takukuru rafiki, ambayo ilikuwa inakwenda kuzinduliwa na mbio za Mwenge wa Uhuru, jambo ambalo hakuweza kutekeleza.

Kuzaga amesema huenda hiyo ilikuwa sababu kubwa ya kufikia hatua ya kujikatisha uhai wake kwa kunywa sumu.

Kufuatia tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema mkoa huo utaweka utaratibu wa kuanza kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na dalili za matatizo ya afya ya akili, ili kupungunza kukithiri kwa matukio ya watu kujiua .

“Lazima hilo lifanyike watu wapatiwe elimu ya matatizo ya afya ya akili na dalili zake ili kuchukua tahadhari, wanapoona dalili kwani kumeibuka matukio ya watu kufanya mauaji au kujinyonga,” amesema.

“Hivi karibuni kuna mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loleza, alijiua huku sababu zikitajwa kuwa ni msongo wa mawazo, sasa katika hili lazima elimu ya kuhusu afya ya akili itolewe kwa jamii ili kupunguza matukio hayo katika jamii,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Saimon Mayeka Salmon, amesema kuwa tayari utaratibu nyingine za mazishi zinaendelea huku akieleza kusikitishwa kwa tukio la Mwalimu huyo kuchukua jukumu la kujikatisha uhai.