Ajiunguza na pasi ili afute tatuu

Muktasari:

  • Mkazi wa kwa msomali mji mdogo wa Boma ng’ombe wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro, Issa Athuman (18) amejiunguza na pasi  ili afute tatuu aliyoichora mkononi, hatua aliyoichukua ili ajiunge na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).



Hai. Mkazi wa kwa msomali mji mdogo wa Boma ng’ombe wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro, Issa Athuman (18) amejiunguza na pasi  ili afute tatuu aliyoichora mkononi, hatua aliyoichukua ili ajiunge na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Athuman aliomba  kujiunga na JKT ila kikwazo akabaini ni tatuu aliyojichora kwenye mkono wake wa kushoto hivyo asingepata nafasi hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi  Oktoba 6,2022  amesema alijichora tatuu hiyo miaka miwili iliyopita mara baada ya kuona watoto wenzake wawili nao wamejichora.


“Baada ya kutokea fursa ya kujiunga na JKT nikaona siwezi kupokelewa nikiwa na tatuu hivyo nikalazimika kujichoma na pasi mkononi ili kufuta alama ila nikaungua,” amesema Athuman.

Amesema mara baada ya kujiunguza na kupata majeraha ambayo yalipona alifika kwenye usaili ila hakufanikiwa kupata.

“Kwa bahati mbaya nimekosa nafasi ya kujiunga JKT na kubaki na maumivu makali kwani kidonda cha kujichoma na pasi bado kipo mkononi mwangu,” amesema Athuman.

Jirani wa Athuman, John Mushi amesema vijana wanapaswa kuwa makini pindi wanapofanya maamuzi kama hayo ya kujichora  mwilini.

"Yaya anafahamu kuwa hajaanza kujitegemea pia ana umri mdogo ila anajichora tatuu na kuomba kazi serikalini anaishia kujiumiza mwilini ili afute alama," amesema Mushi.