Prime
Akili unde yazua hofu kutumika shule za msingi, sekondari
Muktasari:
- Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kupitia mahojiano na wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu unaonyesha kuwa baadhi ya wanafunzi hutumia programu za akili unde kupata majibu ya moja kwa moja ya kazi wanazopewa darasani, huku baadhi wakinakili majibu hayo bila kuyasoma au kuyaelewa.
Dar es Salaam. Kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia ya akili unde miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kumeibua hofu iwapo teknolojia hiyo inawajengea uwezo wa kujifunza au inazalisha kizazi kinachotegemea majibu ya mashine badala ya kufikiri na kutatua matatizo chenyewe.
Ingawa akili unde imekuwa nyenzo muhimu ya kujifunzia duniani kwa kutoa maelezo, mifano ya maswali na mbinu za kujifunza, walimu, wazazi na wataalamu wa elimu wanaonya kuwa matumizi yasiyo na mwongozo, hasa katika kazi za nyumbani (homework), yanaweza kudhoofisha uwezo wa wanafunzi kufikiri kwa kina, kufanya utafiti na kuandika kwa lugha yao wenyewe.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kupitia mahojiano na wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu unaonyesha kuwa wanafunzi wengi, hasa wa sekondari, hutumia programu za akili unde kupata majibu ya moja kwa moja ya kazi wanazopewa darasani, huku baadhi wakinakili majibu hayo bila kuyasoma au kuyaelewa.
Kwa mujibu wa wataalamu wa elimu, kuongezeka kwa matumizi ya akili unde kwa walimu na wanafunzi kunadhihirisha kuwa mfumo wa elimu unaingia katika zama mpya, ikiwamo kubainisha matumizi yanayokubalika katika kazi za nyumbani, tathmini za wanafunzi, utungaji wa mitihani na usahihishaji.
Akizungumza na Mwananchi, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule moja binafsi jijini Dar es Salaam, ambaye aliomba kutotajwa jina lake, amesema karibu kila mwanafunzi katika darasa lao hutumia akili unde wanapopewa kazi za nyumbani.
"Ukipewa maswali mengi unayaweka kwenye akili unde, halafu inakuletea majibu yote. Wengine hata hawaongezi neno lolote, wananakili tu na kuwasilisha kwa mwalimu," amesema.
Mwanafunzi mwingine wa Darasa la Saba amesema baadhi ya wanafunzi hutumia simu za wazazi wao kupata majibu ya maswali ya hesabu, sayansi na Kiingereza.
"Wakati mwingine naelewa ilivyoeleza, lakini mara nyingi nikinakili tu ndiyo napata muda wa kufanya mambo mengine," amesema.
Mzazi wa watoto wawili wanaosoma shule za msingi na sekondari, Rehema Mushi wa Mtoni Kijichi, amesema mwanzoni alifurahia kuona watoto wake wakimaliza kazi za nyumbani kwa haraka, lakini baadaye aligundua walikuwa hawajifunzi bali wanategemea akili unde.
"Nilimuuliza mwanangu afafanue jibu aliloandika, akashindwa. Nikagundua alikuwa amenakili tu kutoka kwenye AI. Hapo ndipo nilipoona kuna tatizo," amesema Rehema.
Mzazi mwingine, George Mrema, amesema anaona hatari kubwa kama mtoto hatatumia akili unde kujifunza hatua za kutatua tatizo badala ya kutafuta jibu la mwisho.
"Tatizo si teknolojia yenyewe, tatizo ni namna watoto wanavyoitumia. Wengi wanataka njia ya mkato na hili linaweza kuwa tatizo kubwa tusipokuwa makini," amesema Mrema.
Walimu waanza kuona mabadiliko
Baadhi ya walimu waliozungumza na Mwananchiwamesema sasa wanapokea kazi zilizoandikwa kwa lugha ya kitaalamu kuliko kiwango cha mwanafunzi, lakini mwanafunzi huyo huyo hushindwa kujibu maswali ya kawaida darasani.
Mwalimu mmoja wa shule ya sekondari jijini Mwanza amesema imekuwa kawaida kuona wanafunzi wakileta majibu yenye istilahi ngumu ambazo hawajawahi kuzitumia darasani.
"Ukimwita mbele afafanue alichoandika, anakaa kimya. Hapo unajua kazi hiyo haikutokana na uelewa wake," amesema mwalimu huyo.
Amesema hali hiyo imewalazimu walimu kuongeza maswali ya papo kwa papo na majaribio ya darasani ili kupima uelewa halisi wa wanafunzi.
Walimu nao wamo
Wakati mjadala mkubwa ukielekezwa kwa wanafunzi wanaotegemea akili unde kufanya kazi za nyumbani, imebainika kuwa walimu nao wameanza kutumia teknolojia hiyo katika kuandaa mitihani, kazi za majaribio na hata kusaidia kusahihisha baadhi ya majibu ya wanafunzi.
Baadhi ya walimu waliozungumza na Mwananchikwa sharti la kutotajwa majina yao wamesema akili unde imekuwa nyenzo inayowarahisishia kazi, hususan wanapohitaji kuandaa maswali mengi kwa muda mfupi au kupata mifano ya maswali kulingana na mada wanazofundisha.
Mwalimu mmoja wa sekondari amesema zamani alitumia saa kadhaa kuandaa mtihani mmoja, lakini sasa hutumia akili unde kupata rasimu ya maswali, kisha huiboresha ili iendane na kiwango cha wanafunzi wake.
"Teknolojia hii inanisaidia kuokoa muda. Sipakui maswali na kuyatumia moja kwa moja, bali nayahariri na kuhakikisha yanaendana na nilichofundisha darasani," amesema.
Mwalimu mwingine amesema akili unde humsaidia pia kuandaa mpango wa usahihishaji na kutoa maoni ya awali kwenye insha za wanafunzi, ingawa uamuzi wa mwisho hubaki kwake.
"Akili unde inaweza kupendekeza maeneo ambayo mwanafunzi amekosea au kuboresha lugha, lakini siwezi kuiachia iamue alama za mwisho. Lazima mwalimu ahakiki kila kitu," amesema.
Mtaalamu wa teknolojia katika elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Deus Ngaruko, amesema matumizi ya akili unde kwa walimu yanaweza kuongeza ubora wa ufundishaji ikiwa yatatumika kama msaidizi, si mbadala wa taaluma yao.
Amesema akili unde inaweza kusaidia kuandaa maswali yenye viwango tofauti vya ugumu, kuandaa mipango ya masomo na kutoa mrejesho wa awali kwa wanafunzi, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya uamuzi wa kitaaluma wa mwalimu.
"Hatari inaanza pale ambapo mwalimu anatumia majibu hayo bila kuyapitia. Akili unde inaweza kutoa taarifa zisizo sahihi au maswali yasiyoendana na mtaala wa Tanzania. Ndiyo maana uamuzi wa mwisho lazima ubaki kwa mwalimu," amesema Ngaruko.
Amesema mwanafunzi anapotumia akili unde kupata maelezo ya ziada, mifano ya maswali au ufafanuzi wa mada, teknolojia hiyo huongeza uwezo wa kujifunza, lakini anapoitumia kufanya kazi yote kwa niaba yake, hupunguza nafasi ya kukuza fikra na ubunifu.
"Ubongo wa mtoto hukua kwa kufanya mazoezi ya kufikiri na kutatua changamoto. Ukimwachia akili unde ifanye kila kitu, unampokonya fursa hiyo muhimu," amesema.
Mhadhiri wa Saikolojia, Neema Msuya, amesema kazi za nyumbani zimekuwa sehemu muhimu ya kujenga nidhamu ya kujifunza na uwezo wa kujitegemea.
"Mtoto anayepata jibu tayari bila kupitia mchakato wa kulitafuta hupata alama nzuri, lakini si lazima awe amejifunza. Baadaye anaweza kushindwa kwenye mitihani inayohitaji kufikiri mwenyewe," amesema Msuya.
Msimamo wa Serikali
Akizungumza na Mwananchikuhusu matumizi ya teknolojia hiyo katika elimu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema Serikali ilitambua mapema mabadiliko yanayoletwa na teknolojia hiyo na ndiyo maana imeandaa nyaraka za kuongoza matumizi yake nchini.
"Mkakati wa matumizi ya Tehama kwenye elimu upo na mwongozo wa matumizi ya akili unde upo. Nyaraka hizi tayari zipo na zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara," amesema Profesa Nombo.
Amesema mwongozo huo umeweka bayana namna akili unde inavyopaswa kutumika katika mfumo wa elimu bila kuathiri malengo ya kujifunza na unasisitiza matumizi yanayoheshimu haki na maadili, ikiwa ni pamoja na kuzuia vitendo vya kunakili kazi za watu wengine.
"Isichukue nafasi ya mwalimu wala isichukue nafasi ya mwanafunzi. Tunataka itumike kama mwezeshaji katika kujifunza na kujifundishia. Pamoja na manufaa ya akili unde, matumizi yake lazima yaongozwe na maadili ili kulinda uadilifu wa elimu. Hatutaki mwanafunzi atumie akili unde kunakili kazi za wengine au kuwasilisha kazi ambayo hajaielewa," amesema.
Kufuatia hilo, Profesa Nombo amesema walimu wanapaswa kuboresha namna wanavyowapima wanafunzi ili kuhakikisha wanapata ujuzi unaokusudiwa na mitaala.
Amesema mbinu za zamani za utoaji wa kazi zinaweza kutoa nafasi kwa wanafunzi kutumia akili unde kuandika majibu bila kuelewa maudhui.
"Walimu wanapaswa kuboresha namna ya kufanya tathmini ya kazi za wanafunzi ili kuhakikisha mwanafunzi ndiye anayejifunza na kupata ujuzi, si kufanyiwa kazi na akili unde," amesema.
Ameongeza kuwa tathmini zinapaswa kulenga kupima uwezo wa mwanafunzi kufikiri, kuchambua na kutatua matatizo badala ya kunakili taarifa.
Hata hivyo, Profesa Nombo amesema pamoja na maendeleo ya teknolojia, msingi wa elimu haupaswi kupotea. Hivyo, wanafunzi wanapaswa kuendelea kutumia vitabu, kuandika kwa mkono na kufanya uchambuzi wao wenyewe badala ya kutegemea teknolojia katika kila hatua ya kujifunza.
"Lazima tuhakikishe matumizi ya teknolojia yanafanyika kwa usahihi. Mwanafunzi bado anatakiwa kutumia kitabu, kalamu, kuandika kwa mkono na kutumia akili yake kuchambua mambo," amesema Profesa Nombo.