Akimbia toka Tanga hadi kilele Mlima Kilimanjaro kwa saa 65

Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro, Kamishna msaidizi wa uhifadhi, Angela Nyaki (kushoto) akimpongeza Gaudence Lekule baada ya kushuka kutoka mlima Kilamanjaro, ambapo alibeba ujumbe wa utunzaji wa mazingira katika mikoa ya ukanda wa Pwani ili kulinda barafu ya Mlima Kilimanjaro.
Muktasari:
- Lekule mwenye umri wa miaka 37, ambaye ni muongoza watalii, alianza safari hiyo Agosti 21 mwaka huu, akikimbia kutokea mkoani Tanga hadi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, akiwa na ujumbe wa kuihamasisha jamii kutunza mazingira ili kuweza kuinusuru barafu ya mlima huo, na kuiambia dunia kuwa mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika, upo Tanzania.
Moshi. Mtanzania Gaudence Lekule ambaye anashikilia rekodi ya kupanda Mlima Kilimanjaro na kushuka kwa saa 8, ameweka rekodi nyingine ya kutumia saa 65 kutoka Tanga ambako ni ni mita sifuri kutoka usawa wa bahari, hadi katika kilele cha mlima huo wenye urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari.
Lekule mwenye umri wa miaka 37, ambaye ni muongoza watalii, alianza safari hiyo Agosti 21 mwaka 2023; akikimbia kutokea mkoani Tanga hadi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, akiwa na ujumbe wa kuihamasisha jamii kutunza mazingira ili kuweza kuinusuru barafu ya mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika.
Akizungumza katika lango la Marangu mara baada ya kushuka kutoka mlimani, Lekule amesema mbali na ujumbe wa kutunza mazingira, pia alilenga kuitangazia dunia kuwa, Mlima Kilimanjaro upo Tanzania.
“Nilianza safari kutoka Tanga Agosti 21 na nilifika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro saa saba usiku wa uamkia Agost 24, hivyo nilitumia saa 65, na nilikuwa na malengo makubwa mawili ambayo ni kuhamasisha utunzaji wa mazingira ili kuilinda barafu ya Mlima Kilimanjaro, na kuiambia dunia kuwa Mlima Kilimanjaro upo nchini Tanzania na si pengine”
Ameongeza kuwa “Nilikuwa nahamasisha watu wa Tanga ambako ni ukanda wa Pwani kutunza mazingira, kwani uharibifu wa mazingira katika maeneo hayo, kumetajwa kuathiri barafu ya Mlima Kilimanjaro, hivyo watu wa maeneo ya Pwani wakilinda mazingira watakuwa wameulinda mlima huu”.
Akizungumzawakati wa kumpokea kijana huyo, Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Angela Nyaki, amesema Lekule ameiheshimisha hifadhi hiyo na kuitangaza vyema kitaifa na kimataifa.
“Lekule ameitangaza hifadhi na lengo kubwa lilikuwa ni kuionyesha dunia mlima huu uko Tanzania, lakini kuanzia kwake Tanga kulitaka kuionyesha jamii kuwa, uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa barafu ya Mlima Kilimanjaro, unaanzia ukanda wa Pwani, kwani tafiti zinaonyesha kuwa muingiliano wa hali ya hewa ya Pwani unaleta faida na hasara za kuyeyuka kwa barafu hiyo”.
Amesema tafiti zinaonyesha kuwa, barafu ya Mlima Kilimanjaro imepungua kutoka kilometa za mraba 20 iliyokuwepo miaka ya 1980, hadi kufikia kilometa za mraba 1.07 kwa sasa na kwamba juhudi za utunzaji wa mazingira zitasaidia kulinda na kuinusuru barafu hiyo.