Akutwa amekufa akidaiwa kubakwa

Thursday January 14 2021
By Mwandishi Wetu

Misungwi. Mkazi wa kijiji cha Sanjo wilayani hapa Mkoa wa Mwanza, Flora Ndabigaye (27) amefariki dunia baada ya kudaiwa kubakwa.

Mwanamke huyo aliyekuwa akiishi na watoto wake watatu alikutwa takribani mita 17 nje ya nyumba yake akiwa ameuawa usiku wa Januari 11 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Dk Emmanuel Samwel wa hospitali ya Wilaya ya Misungwi aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, aliukuta ukiwa na mbegu za kiume kwenye sehemu zake za siri.

Akizungumza na gazeti hili, mtaalamu huyo alisema mwili huo ulikutwa na alama shingoni, kitendo kinachoashiria alikabwa na kukosa hewa.

“Mwili ulikuwa na michubuko shingoni inaonekana alibanwa akakosa hewa, lakini pia ulikuwa na viashiria vyote vya kubakwa,” alisema Dk Samwel.

Naye Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro alisema jana kuwa wanafuatilia tukio na kuwa wanawashikilia watu wawili mkazi wa Ngara, Mussa Enock (23) ambaye inadaiwa amekiri kuhusika na kitendo cha kumbaka mwanamke huyo.

Advertisement

Mwingine anayeshikiliwa katika tukio hilo ni Abisai Juma (22) maarufu Selemani, ambaye ni mkazi wa Tabora ambao kwa pamoja walikuwa wakiishi nyumba jirani na mama huyo.

Alisema mtuhumiwa namba moja Enock alidai kwamba walikubaliana na Flora wakafanye mapenzi lakini baadaye alimdai fedha ilihali hakuwa nazo hivyo akalazimika kutumia nguvu kutimiza haja zake.

“Huyu Abisai, juzi kati hapa alikuwa amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kubaka mwanafunzi, aliachiwa kwa dhamana wote tutawafikisha mahakamani uchunguzi ukikamilika,” aliongeza Kamanda Muliro kuhusu watu hao wawili ambao wote inasemekana wanafanya kazi ya kuchunga ng’ombe.

Mmoja wa watoto wa marehemu mwenye umri wa miaka minane (jina limehifadhiwa) anayesoma darasa la pili, Shule ya Msingi Nyanhomango, alisema walikuwa wanaishi na mama yao na wadogo zake wawili wenye umri kati ya miwili na minne.

“Usiku tulipomaliza kula mama alituambia tukalale, asubuhi hatukumuona mama na tulifikiri amekwenda kuchota maji kisimani tulipotoka nje tulikuta amelala nje ndipo tulienda kuwaeleza majirani,” alieleza mtoto huyo.

Alisema baba yao anafanya kazi katika mgodi wa dhahabu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Kaimu mtendaji wa kijiji cha Sanjo, Yohana Paschal alisema baada ya kupata taarifa ya tukio hilo katika kitongoji cha Nyasubi alisema walianza kufanya uchunguzi kwa kufuatilia nyayo.

Baada ya kufuatilia nyayo hizo zilionyesha kuingia nyumba ya jirani ambako walikuwa vijana hao wawili wanaofanya kazi ya kulisha ng’ombe.

“Tuliwavua nguo tukabaini Mussa alikuwa bado alikuwa na mbegu za kiume kwenye sehemu zake za siri,” alieleza Paschal.


Advertisement