Alama mbili alizoacha Dk Norah Msuya
Hatoonekana tena kimwili na wala sauti yake haitosikika tena katika kumbi za Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Dar es Salaam, akimwaga,” desa na utirio’.
Hata hivyo, atabaki katika fikra za wanafunzi wake, wahadhiri na hata wanasheria wenzake.
Sio kukumbukwa kwa fikra pekee, ameacha urithi mkubwa kwa pengine watakaotaka kumuona au kumsikia.
Hawa watalazimika kumuona au kumsikia kuputia maandiko aliyoyachapisha katika majarida mbalimbali ya ndani na yale ya nje.
Huyu ni Dk Norah Msuya, aliyekuwa mhadhiri chuoni hapo. Alifariki usiku wa Agosti 3 kwa ajali ya gari, iliyogharimu pia maisha ya nduguze watatu.
Ni ajali iliyoibua hisia za walio wengi. Moja ya ajali zilizoweka rekodi za kupoteza sio tu watu wengi, lakini wanaozaliwa tumbo moja. Hata hivyo, kwa Dk Norah pengo lake linagusa wengi na pengine ndio sababu ya kuandika taazia hii.
Aacha alama
Ni msomi ambaye kuondoka kwake duniani kumeacha alama mbili muhimu za kukumbukwa, ikiwamo ushiriki wake katika utafiti mwingi wa mambo yanayokwaza haki za wanawake na watoto.
Nyingine ni ulezi kwa wanafunzi wake, ambao baadhi wanasema kwao alikuwa zaidi ya mama.
Akiwa amejinasibu kama mtetezi wa wanawake na watoto,Dk Norah alibobea zaidi katika utafiti wa sheria za kimataifa, utawala, haki za binadamu na sheria za mashirika.
Alijiunga na Mzumbe mwaka 2005 akiwa na shahada ya uzamivu kwenye sheria, elimu aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha KwaZulu Natal cha nchini Afrika kusini.
Mwaka 2011 alitoka kampasi kuu ya Mzumbe Morogoro kuhamia kampasi ya Dar es Salam.
Safari yake katika fani ya sheria, ilianzia Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam alikopata shahada ya awali ya sheria na kuendelea na shahada ya uzamili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Ukiondoa kazi ya uhadhiri, alikuwa pia wakili wa mahakama kuu na mahakama nyinginezo za chini. Alikuwa mchambuzi wa mara kwa mara wa majarida ya kimataifa na mjumbe wa bodi ya wahariri ya jarida la ‘Dignity linalotolewa na Chuo Kikuu cha Rhode Island cha nchini Marekani.
Katika utetezi wa haki za watoto, Dk Norah atakumbukwa kama mratibu na mwanzilishi wa taasisi ya msaada wa kisheria na elimu kwa wanawake na watoto (Tanzania Legal Aid Organization for Women and Children).
Uongozi Mzumbe unavyomkumbuka
Akimzumgumzia Dk Norah enzi ya uhai wake, Mkuu wa Chuo cha Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam, Profesa Cyriasus Binamungu, anasema marehemu alikuwa akifundisha masomo ya sheria katika programu mbalimbali za biashara pamoja na utawala.
“Kwenye utumishi wake alikuwa ni nguzo sana katika kubeba mzigo wowote ule kwenye programu zetu zote za sheria. Wanafunzi wake watamkumbuka sana alikuwa ni mbobezi katika kuangalia ni jinsi gani tamaduni zetu zinavyosimama kama kigingi kwa maendeleo ya kinamama.
“Alikuwa amebobea zaidi katika hilo, akichunguza tamaduni zetu ambazo ni potofu zinavyosimama kama vikwazo vya utekelezaji wa haki na kuondokana na ubaguzi kati ya kinamama na kinababa kwani alijikita kwenye hilo na ilikuwa ndio centre (eneo lake) yake,”anasema.
Mhadhiri mwenzake, Dk Coretha Komba anasema Dk Norah alikuwa mchapakazi na mtu anayefanya kazi kwa weledi mkubwa.
“Ni mtu mwenye uchangamfu, aliyehakikisha kila mtu ana furaha na hata akipewa kazi, huifanya kwa moyo wake bila kinyongo,” anaeleza.
Kama mama kwa wanafunzi
Akimzungumzia Dk Norah, Evelyne Urassa, mwanafunzi chuoni hapo, anasema mwalimu huyo alikuwa zaidi ya mzazi kutokana na ufundishaji wake,
”Alikuwa zaidi ya mzazi, alikuwa rafiki na alituchukulia kama tulivyo. Alinifundisha sheria ya utawala, sikuwahi kujinza sheria lakini alinifundisha somo hilo hadi nikawa najiuliza kwa nini sikuanza kusoma sheria,”anasema.
Anaeleza kwamba mbali na ufundishaji wa kumfanya mtu aelewe kile anachofundisha, pia alihakikisha kila mtu anaijua sheria namna atakavyoitumia kwenye utendaji wake wa kazi.
Mwanafunzi huyo anasema hadi anakamilisha muhula wa pili ambao alihitajika kufanya utafiti, alitamani Dk Norah ndiye amsimamie kutokana na moyo wake wa kuhitaji mtu afanikiwe katika kile anachojifunza.
“Wanafunzi wote tumeumia, ilifika hatua anatushirikisha masuala yanayomuhusu hili jambo halikuwa dogo hasa kwa nafasi yake kubwa aliyonayo,”anasema.
Naye kiongozi wa darasa alilofundisha Dk Norah somo la utawala wa sheria, Nemes Patric anasema, mwalimu huyo alikuwa na sura mbili katika maisha ya wanafunzi.
“Ni mtu ambaye hakutukatia tamaa, sisi ndio wanafunzi wa kwanza Chuo cha Mzumbe hapa Tegeta hatujawahi kuandika utafiti wetu na kuutetea, lakini kipindi ambacho tunaandika tunamtumia alikuwa akiutumia muda wake nyumbani kwake na kutusaidia pia,”anasema.
Anasema Dk Norah alikuwa mzazi na mtu wa kuonyesha namna ya kutatua changamoto.
“Maneno yake ya mwisho kabla ya kututoka akiwa kwenye kipindi, kwanza alichelewa kuingia darasani akatuambia wanangu msijali kila kitu kitakuwa sawa, kila anapoingia darasani alikuwa ni mwalimu wa kututia moyo kwamba hata tukifanya vibaya hapo si mwisho wetu, yeye yupo kutusaidia,’’anaeeleza.
Kwa upande wake, Ahmed Tundu ambaye ni mwanafunzi wa Dk Norah, anasema kifo cha mwanatalamu huyo kwake ni kidonda kisichopona kwa namna ambavyo walipata mlezi wa kuwapa ufunuo wa maisha.
Machapisho yake
Mama wa watoto wawili, Dk Norah ameacha chungu ya maandiko ya kisomi, yakiwamo yanayohusu namna mila na tamaduni zinavyokuwa kigingi kwa haki na maendeleo ya wanawake, eneo ambalo inaelezwa kuwa alibobea mno.
Mojawapo ya kazi za kukumbukwa ni tazmili (thesis) yake ya shahada ya uzamifu aliyoipa jina la: ‘’ Harmful Cultural and Traditional Practices: A Roadblock in the Implementation of the Convention on the Elimination of Discrimination against Women and the Maputo Protocol on Women’s Rights in Tanzania
Utafiti huu uliomwingiza katika orodha ya wasomi wa sheria katika ngazi hiyo kubwa ya elimu, uliangazia kwa kina namna baadhi ya mila na desturi zinavyokuwa kikwazo cha utekelezaji wa haki za msingi za wanawake.
Alibaini kuwapo kwa sheria kadhaa zinazomkandamiza mwanamke na hata kunapokuwa na jitihaza za kutaka kuzibadiisha, jitihada hizo hukumbwa na vikwazo vikubwa vya kimila. Utafiti huo alisimamia na Profesa Nomthandazo Ntlama.
Baadhi ya maandiko yake mengine ya kitafiti na kisomi aliyochapisha katika majarida mbalimbali ni pamoja na ‘Tanzania's obligation under international human rights treaties: a case study of women and children's rights (2010), Tradition and Culture Misconceptions and Abuses Fuel Trafficking of Women and Children in Africa katika jarida la Tuma L. Rev.2016 na ‘ The analysis of child marriage and thirdparty consent in the case of Rebeca Z. Gyumi v Attorney General Miscellaneous Civil Case no 5 of 2016 Tanzania High Court at Dar es Salaam, aliouchapisha kwenye jarida la De Jure 2019.
Machapisho mengine ni Tradition and culture in Africa: Practices that facilitate trafficking of women and children, aliotoa kwenye jarida la A Journal of Analysis of Exploitation and Violence 2017, Concept of culture relativism and women’s rights in sub-Saharan Africa’ katika jarida la Journal of Asian and African Studies- 2019.
Mengine ni Traditional" juju oath" and human trafficking in Nigeria: A human rights perspective- 2019; ‘Advocating positive traditional culture to eradicate harmful aspects of traditional culture for gender equality in Africa -2020; ‘Child marriage: An obstacle to socio-economic development in sub-Saharan Africa-2020.Dk Norah akishirikiana na Darlene Mutalemwa na Harold Utouh waliuchapisha utafiti unaosomeka, Soft Skills as a Problem and a Purpose for Tanzanian Industry: Views of Graduates hiyo ikiwa ni mwaka 2020 kwenye jarida la Journal Economic Insights.