Alama za Edward Lowassa zisizofutika

Muktasari:

  • Agosti 26, 1953, msimamizi wa machinjio ya mifugo, Monduli, Arusha, Ngoyai Lowassa, alipata mtoto wa kiume. Akamwita Edward. Hivyo, Edward yumo kwenye rika la Baby Boomers.

Katika mgawanyo wa rika za watu (demographic cohort), Karne 20 ina rika tano. Ya kwanza ni Kizazi Kikuu (Greatest Generation). Hawa ni watu waliozaliwa kuanzia mwaka 1901 mpaka 1927.

Kizazi hiki kilipitia joto la Vita ya Kwanza ya Dunia na kinaishia kipindi ambacho nchi za Magharibi zilikumbwa na mdororo mkubwa wa kiuchumi (Great Depression). Kinachofuata ni Kizazi cha Ukimya (Silent Generation). Hawa ni watu waliozaliwa mwaka 1928 mpaka 1945.

Watu wa Kizazi cha Ukimya walizaliwa kipindi cha mdororo mkubwa wa kiuchumi kisha wakaingia kwenye Vita ya Pili ya Dunia. Wakati wao historia inaonyesha kasi ya uzazi ilikuwa ndogo hasa Magharibi kwa sababu ya misukosuko ya kiuchumi na vita.

Rika la tatu linaitwa Kizazi cha Kishindo (Baby Boomers Generation). Watu waliozaliwa kuanzia mwaka 1946 mpaka 1964. Kipindi hiki dunia ilipokea watoto wapya wengi. Dunia imeondoka vitani. Wanajeshi wengi wamerejea nyumbani. Watoto wengi walizaliwa.

Baada ya Boomers wanaingia Kizazi X (Generation X) ambao ni uzao wa mwaka 1964 mpaka 1980. Rika la tano ni Kizazi cha Milenia (Millennials Generatio) au pia huitwa Kizazi Y. Hawa walizaliwa mwaka 1981 mpaka 1996.

Generation Z (Kizazi Z), huchukua miaka minne ya Karne 20 na kukamilisha muongo mzima wa kwanza wa Karne ya 21, yaani kuanzia mwaka 1997 mpaka 2010. Hivyo, rika la mwisho ambalo ni Kizazi Z, humezwa na watu wengi waliozaliwa Karne ya 21.

Hatima ya Lowasa Chadema

Namtafuta Edward

Agosti 26, 1953, msimamizi wa machinjio ya mifugo, Monduli, Arusha, Ngoyai Lowassa, alipata mtoto wa kiume. Akamwita Edward. Hivyo, Edward yumo kwenye rika la Baby Boomers.

Siku ya uzao ilikuwa Jumatano. Ilikuwa inatimia miaka 210 tangu uzao wa mwanasayansi mahiri wa Ufaransa, Antoine Lovoisier, ambaye ni mkemia kinara wa Karne ya 18, aliyefanya mapinduzi makubwa ya kemikali ikiwemo uzalishaji wa oksijeni ya kimaabara.

Edward ni mtoto wa nne kuzaliwa. Baba wa Edward, mbali na kuwa mkuu wa machinjio katika Serikali ya kikoloni, vilevile alikuwa akifanya kazi kama tarishi wa Wakoloni katika Wilaya ya Monduli, Arusha.

Mwaka 1961, Edward aliandikishwa elimu ya msingi kwenye Shule ya Monduli. Hivi sasa shule hiyo inaitwa Moringe, ikibeba jina la Waziri Mkuu wa zamani na mbunge wa Monduli, Edward Moringe Sokoine.

Sokoine alifariki dunia Aprili 12, 1984 kwa ajali gari. Miaka 11 baadaye, Edward Ngoyai alichaguliwa kuwa mbunge wa Monduli. Kisha miaka 21 tangu kifo cha Sokoine, Edward Ngoyai alikuwa Waziri Mkuu.

Hivyo, mpaka sasa, Monduli imefanikiwa kuweka rekodi ya kuwa na wabunge wawili waliopanda ngazi hadi kuwa mawaziri wakuu. Wote majina yao ni Edward. Wa kwanza ni Moringe Sokoine, wa pili Ngoyai Lowassa.

Akiwa Shule ya Msingi Monduli (Moringe), Edward Ngoyai alidhihirisha kipaji chake cha sanaa ya muziki. Kutokana na umahiri wake wa sanaa, Edward alichaguliwa kuwa kiongozi wa bendi ya muziki shuleni. Akidumu kwenye uongozi wa bendi mpaka alipohitimu darasa la nane mwaka 1967.

Edward alipata ufaulu mzuri kwenye mitihani yake ya kumaliza elimu ya msingi. Alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Arusha, alikosoma kuanzia mwaka 1968 kabla ya kuhitimu kidato cha nne mwaka 1971.

Mitihani ya kidato cha nne, Edward alifanya vema na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Juu ya Milambo, Tabora, kuanzia mwaka 1972 mpaka 1973 alipohitimu kidato cha sita. Kama kawaida, Edward alipata ufaulu mzuri, hivyo kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwaka 1974 alianza masomo ya Shahada ya kwanza ya Sanaa ya Tamthiliya, alihitimu mwaka 1977. Kuhusu masomo, alijiunga Chuo Kikuu cha Bath, kilichopo Bath, Somerset, UK, alikosoma shahada ya uzamili ya Masomo ya Maendeleo. Alihitimu shahada yake mwaka 1984.

Waziri wa zamani, Edward Lowasa akionyesha fomu ya kuwania nafasi ya uras 2015 kwa tiketi ya Chadema.

Safari ya ukuu

Kupaa ngazi za uongozi hadi juu kabisa ya mfumo wa nchi, haikuwa kuchipua kama uyoga. Edward alijiunga na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Tanu miaka ya 1970, na alikuwa mmoja wa vijana wa mwanzo nchini waliobadili kadi, kutoka Tanu kwenda CCM.

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilizaliwa Februari 5, 1977, baada ya vyama Afro Shiraz Pary (ASP) na Tanganyika African National Union (Tanu), kuungana. Kisha, Umoja wa Vijana Tanu ulikufa na kuzaliwa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM). Edward alihama na mabadiliko.

Pamoja na chama, vilevile kutokana mfumo wa chama kimoja uliokuwepo, uliofanya jeshi kuwa sehemu ya chama (Tanu baadaye CCM), Edward alijiunga pia na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alipokea mafunzo na kufuzu.Novemba 1978, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ilipotangaza vita dhidi ya Idd Amin Dada, baada ya Uganda kuiteka sehemu ya mkoa wa Kagera na kuitangaza kuwa mali yao, Edward alikuwa sehemu ya hazina ya nchi kijeshi.

Mwaka 1989, Edward aliteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC). Nafasi hiyo akiitumikia mpaka mwaka 1990, alipopangiwa majukumu ya kitaifa.

Rais Mwinyi alipokuwa anaanza muhula wake wa pili wa uongozi, alimteua Edward kuwa mbunge, kisha akamfanya kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, akishughulika na Bunge pamoja na Mahakama.

Kipindi hicho nchi ilikuwa ya chama kimoja na kwa sababu ya masharti ya Muungano, Rais Mwinyi alikuwa anatokea Zanzibar, hivyo Waziri Mkuu ilikuwa lazima atoke Bara, ambaye alibeba hadhi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, halafu Rais wa Zanzibar alitambulika kama Makamu wa Pili wa Rais.

Huduma ya Edward kwenye Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, ilidumu kwa miaka mitatu. Mwaka 1993, Rais Mwinyi alimbadilisha na kumhamishia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, ambayo alidumu nayo mpaka mwisho wa urais wa Mwinyi mwaka 1995.

Ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza uliohusisha mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1995, Edward alifanya jaribio la kunasa tiketi ya CCM ya kuwa mgombea urais. Hata hivyo alikwama kwenye mchujo wa Kamati Kuu, baada ya hapo aligombea ubunge jimbo la Monduli na kushinda.

Lowasa kujiunga Chadema

Ujio wa Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, ulikuwa na mabadiliko kidogo. Mkapa alimweka Edward kando ya Baraza la Mawaziri. Edward alikuwa mbunge wa benchi la nyuma kwa miaka miwili, yaani mwaka 1995 mpaka 1997.

Mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri ambayo Mkapa aliyafanya mwaka 1997, yalimrejesha Edward barazani. Mkapa alimteua Edward kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Umaskini.

Uchaguzi Mkuu 2000, Edward alirejea Monduli kugombea ubunge. Alishinda kwa wastani mkubwa wa kura, kisha Rais Mkapa katika muhula wake wa pili wote, alimfanya kuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo.

Edward alikuwa nguzo kuu ya mbio za urais za Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, Uchaguzi Mkuu 2005. Baada ya uchaguzi, Jakaya alimteua Edward kuwa Waziri Mkuu. Alihudumia uwaziri mkuu kwa miaka miwili na miezi miwili, kabla ya kulazimika kujiuzulu.

Kashfa ya mkataba wa mradi wa kufua umeme wa dharura kati ya Tanesco na Kampuni ya Richmond, ndio iliyosababisha Edward aachie ngazi baada ya kutajwa kuhusika na kutoa ushawishi wa kuipendelea Richmond ili ipate zabuni.

Kuanzia Februari 7, 2008 alipojiuzulu, Edward alikuwa mbunge wa benchi la nyuma kwa muda, kisha akarejea kwenye uongozi wa Bunge, alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Uhusiano wa Kimataifa, aliyokwenda nayo mpaka Bunge lilipovunjwa Septemba 2015.

Aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk John Pombe Magufuli akiagana na Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Hayati Edward Lowassa baada ya kuutangazia umma rasmi kwamba anarudi nyumbani.  Kushoto ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa walipokutana katika Ofisi Ndogo za Makao makuu ya CCM mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam Ijumaa March 1, 2019. PICHA NA IKULU


Msuli mkubwa kisiasa

Edward alikuwa miongoni mwa waliowania  tiketi ya kuwa wagombea urais vijana ndani ya CCM. Alikuwa  kijana na mwenye msuli mkubwa zaidi mwaka 1995. Ushahidi wa nguvu ya Edward upo ndani ya mchakato wenyewe na baada ya kumalizika.

Rais wa Kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alishutumiwa kuwa ndiye aliyeingilia kati kumzuia Edward kugombea urais. Hata jina la Edward lilipokatwa, vijana wa UVCCM walisimama imara kuhoji uhalali wa kuenguliwa kwake.

Mwalimu Nyerere katika mkutano na vyombo vya habari baada ya kukamilika kwa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM, alilazimika kutoa ufafanuzi kuwa sio yeye aliyemkata, isipokuwa ulikuwa uamuzi halali wa Kamati Kuu CCM.

Ufafanuzi huo aliutoa baada kuulizwa swali kuhusu maneno kwamba ni yeye ndiye alishinikiza kwa jina la Edward kuondolewa. Alisema: “Nadhani watu wanamwonea tu Edward kutaka kulizungumzia hilo jambo mara kwa mara. Hata vijana walihoji kwenye Halmashauri Kuu kwa nini Edward aliondolewa, na Kamati Kuu ilitoa majibu ya kuridhisha.”

Hoja kwamba Mwalimu Nyerere ndiye aliyeshinikiza jina la Edward kuenguliwa kwenye mbio za urais CCM, ilipata nguvu zaidi kwa sababu kipindi cha mchakato Mwalimu alihudhuria mkutano wa Kamati Kuu wakati hakuwa mjumbe. Mwalimu alijitetea kuwa alihudhuria Kamati Kuu kwa mwaliko maalumu ambao hakuona msingi wa kuukataa.

Hiyo ni hoja yenye kuthibitisha kuwa Edward alikuwa mgombea mwenye nguvu mwaka 1995, ndio maana kitendo cha jina lake kukatwa kilisababisha rabsha kuanzia ndani ya chama mpaka nje kwenye uso wa vyombo vya habari.

Uchaguzi Mkuu 2005, Edward hakugombea urais. Akaongoza kampeni za Jayaka. Chini ya uongozi wake, Jakaya alipita kama kimbunga kuanzia ndani ya chama. Jakaya alipata tiketi ya CCM mbele ya mwanasiasa mahiri aliyekuwa na wasifu mkubwa, Dk Salim Ahmed Salim.

Kisha, kwenye uchaguzi wa jumla, Jakaya alishinda urais kwa kura zaidi ya asilimia 80. Hiyo pia ni uthibitisho wa nguvu kubwa ya Edward kisiasa. Karata zake zilimfanya Jakaya kuukwaa urais kwa urahisi mno. Kila hatua ilikuwa nyepesi. Edward akiwa mwenyekiti wa kampeni.

Edward alipojiuzulu uwaziri mkuu Februari 7, 2008, kuna waliotabiri kwamba ingekuwa mwisho wake kisiasa. Hata hivyo, kishindo chake kwenye Uchaguzi Mkuu 2015, kimeacha taswira isiyofutika katika uso wa siasa za nchi tangu uhuru wa Tanganyika na Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jinsi Edward alivyotawala mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM na alivyogeuka kinara wa jumla wa safari ya kuuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kipimo cha jinsi ambavyo alikuwa na nguvu kubwa.

CCM ilibidi waucheze mpira mgumu kupitia mgombea wake, Dk John Magufuli, kuweza kumshinda Edward. Kwa ushindi wa jumla ambao CCM iliupata, mwisho kabisa ni matokeo ya Jakaya kuchanga karata kikamilifu.

Sababu ya CCM kulazimika kucheza mpira mgumu ni Edward kuamua kuhamia Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), ambacho kilimpa tiketi ya kugombea urais. Kampeni zilikuwa za kishindo.

Kitendo cha Edward kugombea urais kupitia Chadema, kilimfanya aweke rekodi ya kuwa mpinzani aliyepata wastani mkubwa zaidi wa kura za kiti cha Rais. Vilevile alisababisha CCM ipate wastani mdogo katika historia. Edward alipata karibu asilimia 40, Magufuli wa CCM alikusanya asilimia 58.

Kabla ya hapo, mgombea urais wa upinzani aliyekuwa na rekodi ya wastani mkubwa wa kura ni Augustino Mrema, alipotembea na tiketi ya NCCR-Mageuzi mwaka 1995. Mrema alipata asilimia 28 na mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa, alivuna asilimia 61.

Machi 2019, Edward aliishitua nchi alipohama ghafla kurejea CCM, kisha alipokelewa na aliyekuwa Mwenyekiti, Dk Magufuli, ambaye pia alikuwa Rais wa Tanzania. Tangu Edward aliporejea CCM, amegeuka adimu kwenye majukwaa ya kisiasa.

Lowasa arudi CCM

Ujenzi wa shule za sekondari za kata nchi nzima ni wazo lililochakatwa Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Edward. Hivyo, nchi inapojivunia matokeo makubwa ya idadi nzuri ya vijana wa Kitanzania kupata elimu ya sekondari, sifa zirejee kwa Edward.

Edward alipokuwa Waziri wa Maji, alivunja mkataba na kuifukuza nchini kampuni ya City Water ya Afrika Kusini, iliyokuwa imeingia ubia na Serikali kwa ajili ya kutoa huduma za maji kwenye Jiji la Dar es Salaam. Kampuni hiyo ilifungua kesi mahakamani na Serikali ilishinda, kuonyesha Edward alivunja mkataba wa kufuata sheria.

Mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria hadi mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Tabora ni ushindi wa kihistoria wa Serikali. Edward ndiye aliyebeba wazo na kujenga ushawishi kwenye Baraza la Mawaziri, kisha bungeni. Wananchi wa Shinyanga, Simiyu na Tabora wanavyonufaika hivi sasa na maji ya Ziwa Victoria, ni alama ya Edward isiyofutika.

Edward aliwahi kusimulia jinsi alivyopata upinzani kwenye Baraza la Mawaziri ili kufanikisha mradi huo wa maji ya Ziwa Victoria. Alisema, hata aliyekuwa Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye, aliukataa mradi huo. Ni Jakaya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Rais Mkapa, waliouelewa na kuunga mkono.

Alama nyingine ya Edward ni Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom). Jakaya alipoingia ofisini alifanya uamuzi wa kutoa majengo na eneo la CCM, Kizota, Dodoma ili kijengwe chuo. Edward kwa nafasi yake ya uwaziri mkuu alikuwa msimamizi mkuu wa utekelezaji wa ujenzi hadi kuanza kwa Udom.

Udom kinatajwa kuwa chuo kikuu kikubwa zaidi Afrika. Hivi sasa nchi ina wahitimu wengi wa shahada mbalimbali kutoka Udom, na maelfu wanaendelea kusoma na kudahiliwa. Hiyo ni alama nyingine isiyo rahisi kufutika kuhusu Edward.

Ipo kumbukumbu ya kuuzwa kwa bustani ya Mnazi Mmoja kwa mfanyabiashara aliyekuwa na asili ya Asia. Edward alipokuwa Waziri wa Ardhi, ndiye aliyepinga uuzwaji huo. Alitoa hotuba bungeni kujenga hoja ya kuuzwa Mnazi Mmoja.

Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikerwa mno na ubinafsishaji wa Mnazi Mmoja. Katika moja ya hotuba zake, alihoji: “Mnauza mpaka bustani?”. Leo hii, Mnazi Mmoja inapoendelea kuwa mali ya umma, ni alama isiyofutikwa ya Edward, kupitia uamuzi alioufanya alipokuwa Waziri wa Ardhi.


Endelea kufuatilia Mwananchi na mitandao yetu kwa habari zaidi.