Alichokisema Malisa baada ya kuachiwa kwa dhamana

Mwanaharakati na Mkurugenzi wa Taasisi ya GH Foundation, Godlisten Malisa akizungumza muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana leo Juni 8, 2024. Picha na Florah Temba
Muktasari:
- Alikamatwa Juni 6 jijini Dar es Salaam, aliachiwa jana kwa dhamana mkoani Kilimanjaro, baada ya kuhojiwa na maofisa wa polisi akituhumiwa kwa makosa matatu
Moshi. Mwanaharakati, Godlisten Malisa ameachiwa kwa dhamana, huku akisema misukosuko anayoipata, haitamrudisha nyuma kwenye harakati za kutetea haki za wananchi, kwa kile alnachoeleza kuwa yupo sahihi na anachokifanya.
Malisa aliyekamatwa Juni 6 jijini Dar es Salaam, aliachiwa jana kwa dhamana mkoani Kilimanjaro baada ya kuhojiwa na maofisa wa Polisi, akituhumiwa kwa makosa matatu aliyotenda kupitia akaunti yake ya Instagram, likiwemo la kutoa taarifa bila kibali kupitia mitandao ya kijamii.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 8, 2024 muda mfupi baada ya kutoka polisi, Malisa amesema anachokifanya ni kutetea haki za watu.
‘’Unapotimiza jukumu kisha ukakutana na upinzani, maana yake haitakiwi kurudi nyuma bali kuongeza kasi juhudi zaidi katika kupigania haki za Watanzania,’’ amesema na kuongeza:
“Kimsingi, ukiangalia mashtka yote yanayonikabili mawili yalikuwa yanatetea haki ya watu kuishi na moja ni haki za walimu kulipwa mishahara yao. Sasa nikirudi nyuma kuna maelfu walioko nyuma yangu na wao watarudi nyuma, nikisonga mbele basi waliopo nyuma watapata ujasiri wa kuendelea mbele.’
Amesema hawezi kurudi nyuma kwa sababu anachokifanya, ana imani nacho na dhamira yake inamweleza kuwa hajakosea.
‘’Nawashukuru wote walioniombea katika kipindi hiki niliposhikiliwa,”amesema Malisa ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya GH Foundation.
Kwa mujibu wa wakili wa Malisa, Hekima Mwasipu mteja wake alihojiwa na maofisa polisi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na kuachiwa kwa dhamana ya wadhamini wawili waliosaini Sh20 milioni.
Amesema Malisa alifikishwa Moshi akituhumiwa kwa makosa matatu ikiwamo kuchapisha taarifa za uongo kwenye ukurasa wake wa Instagram, kwamba Paul anayedaiwa kumuua Beatrice Minja alikuwa ni mfanyakazi wa Profesa Adolf Mkenda (Waziri wa Elimu) na pia tukio la mwanafunzi anayedaiwa kuuliwa kwa kuchapwa na walimu Moshi.
Mwanaharakati huyo, alikamatwa na kusafirisha Moshi Juni 6 muda mfupi baada ya kesi inayomkabili pamoja na Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob kuahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Malisa na Jacob walifikishwa katika mahakama hiyo, wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo, kinyume cha sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Wakili Mwasipu amesema baada ya kufika Moshi mteja wake alihojiwa na polisi mkoa wa Kilimanjaro kuhusu kuchapisha taarifa za uongo kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Mwasipu amesema Juni 7, Malisa alihoji kuhusu tuhuma ya taarifa alizochapishwa katika mtandao wa instagram juu ya tukio la mwanafunzi anayedaiwa kuuliwa kwa kuchapwa na walimu Moshi.
Lakini jana wakili huyo alisma Malisa alihojiwa na maofisa wa upelelezi wa makosa ya jinai, akithumiwa kutoa taarifa bila kibali kwenye akaunti yake ya Instagram kuhusu walimu waliokuwa wanasahihisha mitihani ya kidato cha nne mwaka huu kutolipwa posho zao.
“Hakuhojiwa kwa muda mrefu sana, wamempa dhamana na atatakiwa kuripoti tena kituoni hapo Juni 18,”amesema Mwasipu.
Hata hivyo, Mwasipu alisema baada ya kuachiwa kwa dhamana usiku wa kuamkia Juni 8, Malisa alipelekwa moja kwa moja katika hospitali ya KCMC baada ya kuugua ghafla, akisumbuliwa na maumivu ya kichwa, kifua, kizunguzungu na tumbo.
“Tulipopata dhamana usiku saa sita tulimpeleka hospitali ya KCMC moja kwa moja kwa sababu alikuwa akilalamika maumivu ya kichwa, kifua, kizunguzungu na tumbo, alipatiwa matibabu na tulirudi saa 10 alfajiri, kwa sasa anaendelea vizuri, “amesema Mwasipu.