Alichosema kinara kidato cha nne 2021

Consolata Lubuva

Muktasari:

Mtahiniwa aliyeongoza kitaifa kwenye matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2021, Consolata Lubuva amesema ataongeza juhudi zaidi ili afikie ndoto yake ya kuwa daktari wa watoto.

Dar es Salaam. Mtahiniwa aliyeongoza kitaifa kwenye matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2021, Consolata Lubuva amesema ataongeza juhudi zaidi ili afikie ndoto yake ya kuwa daktari wa watoto.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Januari 15, 2022 nyumbani kwao mkoani hapa, Consolata amesema hakutarajia kuongoza kitaifa kwenye matokeo hayo bali ni kwa uwezo wa Mungu.

"Nitakwenda kusoma PCB ili niwe daktari niweze kuwasaidia watoto wadogo, napenda sana kuwasaidia watoto wadogo ili wakue vizuri," amesema mhitimu huyo aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa.

Consolata ameeleza kwamba siri ya mafanikio yake ni kumuomba Mungu, ushirikiano kutoka kwa walimu, wazazi na wanafunzi wenzake pamoja na jitihada zake binafsi.

Msichana hiyo amewashauri wanafunzi ambao hawajafanya vizuri kutokata tamaa bali waongeze juhudi zaidi kwenye masomo yao na kumwomba Mungu awasaidie.

"Nikikutana na Rais Samia, kwanza nitampongeza kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke, pili, nitamwambia nitaongeza juhudi zaidi kwa sababu ametupa mfano bora kwamba wanawake na sisi tunaweza," amesema mhitimu huyo huyo wakati akizungumza na Mwananchi.