Alivyopoteza kizazi, miguu na vidole tisa

Saturday October 02 2021
alivyopoteapic

Huu ndio mwonekano wa mikono ya msichana Asia Patrick, baada ya kukatwa vidole vyote na kubakiwa na kidole kimoja. Anatumia kidole hicho kufanya shughuli za upambaji.

By Florence Majani

Dar es Salaam. Ni ndoto ya kila mwanamke kubeba ujauzito, kuzaa na hatimaye kumpakata mtoto wake.

Ndivyo ilivyo kwa kila mwanamke anayetamani kuwa siku moja atakuja kuitwa mama.

Ndoto hiyo alikuwa nayo pia msichana Asia Patrick (21), lakini kwa sasa imezima mithili ya mwanga wa mshumaa katika upepo mkali.

Lakini si kuzimika tu, Asia ametoka kuwa msichana mrembo hadi kuwa mlemavu mwenye kidole kimoja tu, baada ya vyote tisa mkononi kukatwa sambamba na miguu yake yote miwili.

Hata hivyo, ulemavu huo haujawa kikwazo kwake. Kidole kimoja hichohicho Asia bado anaweza kukitumia kufanya kile ambacho unaweza usiamini kama anaweza kukifanya. Ni kipi na kwa vipi? Fuatilia simulizi yake iliyo na simanzi lakini ikigubikwa na matumaini maishani.

Uhusiano, mimba hadi ulemavu

Advertisement

Asia ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanne wakazi wa Buzuruga, Mwanza na kwa kuwa hakufanikiwa kuendelea na elimu ya sekondari, alijikuta katika uhusiano wa kudumu na Rashid Musa tangu mwaka 2018.

Mwaka huohuo, akiwa na miaka 18, Asia alifanikiwa kupata ujauzito, ambao aliutunza akiwa na matarajio ya kujifungua salama na kupakata mtoto wake wa kwanza.

Kwa bahati mbaya, mwanzoni mwa Aprili mwaka huo, akiwa na ujauzito wa miezi mitano, akiwa eneo la nyumbani kwao Buzuruga, alipata ajali ya kuanguka kutoka mlimani hadi chini. Kwa wakazi wa Mwanza wanafahamu maisha ya milimani yalivyo.

“Kama ujuavyo, makazi yetu huku Mwanza baadhi yapo milimani kutokana na uwepo wa miamba, na nyumbani kwetu kupo kilimani na tumezungukwa na mawe, nilianguka kwa bahati mbaya na nikapoteza fahamu,” anasema Asia.

Anasema, baada ya kuzinduka alijikuta katika kituo cha afya cha jirani, ambako alipatiwa matibabu ya awali na kuambiwa kuwa mimba yake imeonyesha dalili ya kuharibika, hivyo akazuiwa kufanya kazi ngumu na kuinama, lakini akaruhusiwa kurudi nyumbani.

“Baada tu ya kuruhusiwa kurudi nyumbani, nilipata maumivu makali ya tumbo, nikaona dalili za damu kutoka. Nikarudi tena hospitali. Nikapimwa na kuambiwa mimba imeharibika lakini ili nisafishwe, nahitaji kulipa Sh 150,000,” anasema huku akijaribu kukumbuka.

Anasema hakuwa na fedha hizo na akaruhusiwa kurudi nyumbani akiwa katika hali ya maumivu makali hadi baada ya siku mbili mmoja wa majirani zake, alipojitolea kumpa fedha na ushauri wa dawa ya kutumia itakayosaidia kumsafisha.

“Kati ya majirani niliokuwa nao akatokea mama mmoja akaniambia Asia kwa nini unateseka, akanipa Sh30,000 akaniambia tuma mtu akakununulie vidonge, mimi sikujua ni vidonge gani kwa sababu aliandika yeye na akamtuma mtoto akavinunue dukani, lakini baada ya kunywa maumivu yalizidi na nikajikuta katika hospitali ya Sekou Toure,” anasema.

Anasema alilazwa hospitalini hapo kwa siku mbili na kwa mujibu wa wazazi wake, hali ikazidi kuwa mbaya na akatakiwa kufanyiwa upasuaji na hivyo akahamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Asia anaeleza zaidi kuwa alipofika Bugando, madaktari walimfanyia uchunguzi na kushauri kuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kukiondoa kizazi, kwani kimeoza kabisa na kikiachwa anaweza kupoteza maisha.

Anakumbuka ilikuwa Aprili 17, 2018 alipofanyiwa upasuaji wa kuondoa kizazi chake na baada ya hapo akahamishiwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa ajili ya uangalizi maalumu.

“Nikiwa ICU nilianza kuona vidole vyangu vya miguu na mikono vinavimba, vinasambaa na kuanza kuwa vyeusi, baadaye ule uvimbe ukapasuka na kutoa maji. Baada ya maji, vikatoa usaha na harufu,” anasimulia Asia.

Anasema miguu yote miwili kuanzia vidoleni hadi karibu na goti ilivimba na kutoa maji, ngozi ikaanza kudondoka na usaha ukachuruzika.

“Nilikuwa na maumivu makali sana na si hivyo tu, nilihitaji sindano kwa kila baada ya saa moja, ambayo iligharimu Sh500,000 kwa ajili ya kuzibua mishipa iliyoziba. Lakini familia yangu ni duni, hatukuweza kumudu hizo gharama,” anasema.

Baadaye miguu na mikono iliendelea kuoza na kubaki mifupa mitupu, kwani ngozi iliisha hadi ukiugonga mfupa kwa kisu huyasikii maumivu.

“Nakumbuka Mei 21, 2018, nilifanyiwa upasuaji wa kukata miguu yangu yote na vidole tisa,” anasema na kuongeza: “Niliumia sana na sikuwahi kufikiria nitakuwa katika hali hii.”

Lakini anasema licha ya kukatwa miguu hiyo, baada ya muda mguu wa kushoto uliendelea kuoza na ikabidi arudishwe tena hospitali na mguu huo ukakatwa tena juu zaidi.

Anasema baada ya upasuaji huo wa pili wa viungo, alianza kupona lakini hakuruhusiwa kutoka hospitali kwa sababu hakuwa na fedha za kulipa gharama za matibabu.

“Nilikaa hospitali tangu Aprili, 2018 hadi Agosti 17, 2018 ndipo nilipotoka baada ya mama kupata msaada wa fedha za kulipa deni la hospitali kutoka kwa wasamaria,” anasema.

Baada ya Asia kuruhusiwa kurudi nyumbani, alianza maisha mapya bila viungo akitegemea msaada wa mama yake, kula, kuoga, kujisaidia, kuvaa na kila shughuli muhimu ya mwili wake, kwani hakuwa na miguu yote na mikononi, akibakiwa na kidole gumba kimoja tu.

“Nilikuwa ni mtu wa ndani tu, kwa sababu nyumbani kwetu ni Buzuruga milimani na nyumba yetu ipo kwa juu sana, nilikuwa mtu wa kukaa ndani, kuoga ndani, kula ndani, ukitaka kuota jua nje, inabidi kubebwa na kuwekwa mlangoni ndio ulione jua,” anasema.

Apata msaada

Anasema kwa bahati nzuri mama yake Asia, alikutanishwa na Flora Lauwo, ambaye anasaidia watu wenye ulemavu na kuanzia hapo alipata msaada wa viungo bandia.

“Kupitia mitandao ya kijamii ya Mamii (akimaanisha Flora Lauwo) nilisaidiwa na wasamaria wema, ambao walinichangia fedha na nikanunuliwa miguu bandia Februari 2019,” anaongeza.

Anasema baada ya kupona, Flora alimchukua na kuanza kumpa mafunzo ya kuremba wanawake katika saluni yake.

“Nakumbuka siku hiyo nilikwenda kazini kwake, akaniambia; Asia hebu jaribu kushika hii brashi, alipoona naweza angalau kushika brashi bila vidole, akaniambia niende kesho kuanza mafunzo,” anasema huku akionyesha tabasamu usoni lililochanganyika na huzuni.

Alianza mafunzo na kufanikiwa kufuzu upambaji, lakini bado akapata changamoto ya ajira.

“Ni kweli watu wanauona uwezo wangu, lakini wanasita kuniajiri kwa sababu wanapata wasiwasi iwapo nitataka kujisaidia, nikiumwa ghafla na pia ili nimpambe mtu, natakiwa kukaa kwenye kiti kwa sababu siwezi kusimama kwa muda mrefu,” anasema na kuongeza: “Maumivu ya miguu bado yananisumbua, hasa ninapotembea muda mrefu au kusimama, pia mara kadhaa miguu hunichubua na kusababishia vidonda.”

Akizungumzia zaidi suala la ajira, Asia anasema aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Martin Shigela alichukua kiasi cha fedha katika ofisi yake kwa ajili ya kumfungulia saluni.

“Lakini zile fedha zilikuwa ndogo na hazikukidhi kufungua saluni na pia kutokana na hali yangu, nilihitaji sana kuajiri watu watakaonisaidia ikiwamo kusuka,” anasema na kuongeza:

“Nina uwezo, nimejikubali, nitafanya chochote, licha ya maumivu makali niliyonayo.”

Anita Samson wa Shirika la Wadada Solution la jijini Mwanza, kwa kushirikiana na Pathfinder Inernational wanafanya kazi na vijana na kuwasaidia kuwapa elimu ya afya ya uzazi kwa kuepuka mimba za utotoni ambazo zinahatarisha maisha yao.

“Tumefanya kazi na Asia, na kumpa stadi za maisha, ikiwamo elimu ya ujasiriamali ili aweze kusonga mbele,” anasema.

Daktari azungumza

Madaktari wa Hospitali ya Bugando na Sekou Toure hawakuweza kupatikana kuzungumzia sakata la Asia baada ya Mwananchi jana kufika katika hospitali hizo na kujibiwa kuwa kwa sasa madaktari waliokuwa wakishughulikia suala hilo ni vigumu kuwapata, hivyo wapatiwe muda zaidi kuangalia rekodi.

Hata hivyo, Mwananchi ilizungumza na Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama wa Hospitali ya Ekenywa, Lawrence Mpangala.

“Ingawa hatuna uhakika na dawa aliyopewa, lakini naona suala la uzembe hasa wa kuchelewa kupata matibabu umesababisha madhara kwa huyu binti,” anasema.

Anasema, daktari alitakiwa aanze kumpa huduma ili aokoe maisha yake kwanza kisha suala la hela lingefuata baadaye.

Kwa kuchelewa kupata matibabu, huenda Asia alipata maambukizi katika mfuko wa kizazi, hali iliyosababisha kizazi kuharibika hadi kuondolewa.

Dk Mpangala anasema: “Maambukizi katika mfuko wa kizazi, yaani ‘sepsis’ huenda ndicho chanzo cha tatizo la ‘gangrene’ lililosababisha miguu na vidole kukatwa.”

Advertisement