Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyedai kutekwa akienda kuuza kuku sokoni, aishia kifungo cha maisha

Muktasari:

  • Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Morogoro, imetupilia mbali rufaa ya James Luko aliyepinga hukumu ya kifungo cha maisha jela, baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha bila shaka kuwa alikutwa na kilo 108 za bangi katika eneo la Lugenge, Morogoro.

Arusha. Licha ya kudai alitekwa akiwa njiani kwenda kuuza kuku sokoni, kushikiliwa katika nyumba ya wageni na baadaye kubambikiwa kesi ya dawa za kulevya, James Luko ameshindwa kujinasua na kifungo cha maisha jela.

Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Morogoro, imetupilia mbali rufaa yake ya kupinga hukumu hiyo baada ya kuridhika kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa alikutwa ndani ya kibanda akiwa amelalia magunia sita yaliyokuwa na kilo 108 za bangi.

Katika hukumu iliyotolewa jana Julai 10, 2026, Jaji Stephen Magoiga amesema hakukuwa na sababu ya kuingilia uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Morogoro, ambayo ilimhukumu kifungo cha maisha baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.

Mahakama pia ilisema madai ya mrufani kwamba alitekwa njiani alipokuwa akienda sokoni kuuza kuku, akapelekwa katika nyumba ya wageni na baadaye kulazimishwa kugonga alama ya kidole gumba kwenye nyaraka asizozijua, yalibaki kuwa madai yasiyoungwa mkono na ushahidi wowote.


Msingi wa kesi

Upande wa mashtaka ulidai kuwa Julai 8, 2025, katika eneo la Lugenge, mkoani Morogoro, maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) walifanya operesheni kufuatia taarifa kutoka kwa mtoa taarifa.

Kwa mujibu wa ushahidi, maofisa hao walifika eneo hilo na kukuta vibanda vitatu vilivyodaiwa kutumiwa na watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, kisha wakaanza kuvikagua kimoja baada ya kingine.

Mahakama ilielezwa kuwa katika kibanda cha tatu, James alikutwa amelala juu ya mifuko sita ya salfeti iliyokuwa imejaa majani makavu, ambayo baadaye yalithibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ni bangi yenye uzito wa kilo 108.


Utetezi

Katika utetezi wake, James alidai kuwa Julai 7, 2025, akiwa safarini kwenda Soko la Nyandira kuuza kuku, alifika eneo la Kibaoni ambako alikutana na watu wawili waliokuwa ndani ya gari.

Alidai watu hao walimuuliza bei ya kuku watano aliokuwa amebeba na baadaye wakamwomba awasindikize hadi sokoni na akiwa ndani ya gari, alidai aliulizwa kama anamfahamu mtu anayeitwa "Masta", lakini akajibu hamjui.

Alidai walipokaribia sokoni, mmoja wao alimnyooshea bastola huku mwenzake akielekea upande mwingine, kabla ya kumpeleka katika nyumba ya wageni ya Jehova, ambako alishikiliwa hadi Julai 9, 2025.

Aliiambia mahakama kuwa siku hiyo alipelekewa karatasi, akapigwa na kulazimishwa kuweka alama ya kidole gumba kwenye nyaraka ambazo hakujua zilikuwa na maudhui gani na kuwa aliendelea kushikiliwa hadi Agosti 4, 2025, alipofikishwa mahakamani.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, Mahakama ya Hakimu Mkazi ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha maisha jela.


Rufaa

Akiwa hajaridhishwa na hukumu hiyo, James alikata rufaa akiwa na sababu saba, ikiwemo madai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa kukosekana idhini ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Sababu nyingine ni kwamba alishikiliwa kwa siku 27 kabla ya kufikishwa mahakamani kinyume cha sheria, upekuzi ulifanywa bila kibali, ushahidi wa shahidi huru haukuwa wa kuaminika, mnyororo wa utunzaji wa vielelezo ulikuwa na mapungufu na kwamba alibambikiwa kesi hiyo.


Uamuzi wa Mahakama

Akitoa uamuzi, Jaji Magoiga alisema hoja ya kushikiliwa kwa siku 27 kabla ya kufikishwa mahakamani haiwezi kubatilisha kesi kwa kuwa kuchelewa huko hakukuonyesha kuwa mrufani alipata madhara katika utetezi wake.

Amesema wakati huo uchunguzi wa kisayansi ulikuwa bado unaendelea na ripoti ya maabara ilikuwa haijakamilika, hivyo mazingira ya kesi hayakuonyesha kuwa haki za mrufani zilikiukwa kwa kiwango cha kuifanya kesi kuwa batili.

Mahakama pia ilitupilia mbali hoja kwamba upekuzi ulifanywa bila kibali, ikisema sheria inaruhusu upekuzi wa dharura pale maofisa wanapopokea taarifa ambazo zinaweza kufanya ushahidi upotee ikiwa watasubiri kupata kibali.

Kuhusu shahidi huru, Jaji amesema sheria haihitaji awe kiongozi wa eneo, bali mtu huru aliyeshuhudia mchakato wa upekuzi na ambaye ushahidi wake ulionekana kuwa wa kuaminika.

Aidha, alikataa hoja kwamba cheti cha kukamata hakikuonyesha bangi ilitoka kwenye kibanda cha tatu, akisema ushahidi wa mashahidi pamoja na alama ya kidole gumba ya mrufani kwenye nyaraka za ukamataji ulithibitisha uhusiano wake na vielelezo hivyo.

Jaji amesema ushahidi wa upande wa mashtaka kuhusu ukamataji, utunzaji wa vielelezo na matokeo ya uchunguzi wa maabara uliunda mnyororo usiovunjika uliothibitisha bila shaka kuwa bangi iliyokamatwa ilikuwa mikononi mwa mrufani.

"Utetezi wa mrufani ulikuwa ni kukanusha tu bila kuibua shaka ya msingi dhidi ya ushahidi mzito uliotolewa na upande wa mashtaka," amesema Jaji Magoiga

Kutokana na sababu hizo, Mahakama ilihitimisha kuwa hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ilikuwa sahihi, hivyo ikatupilia mbali rufaa hiyo.