Utata kupotea, kukutwa mochwari ya polisi mwili wa Robert

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lasema lawatuhumu Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob na mwanaharakati, Godlisen Malisa kwa kusambaza taarifa za uongo.

Dar es Salaam. Utata umegubika kifo cha Robert Mushi, aliyepotea na baadaye mwili wake kugundulika ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Polisi Kilwa Road, wilayani Temeke.

Licha ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kusema Mushi aligongwa na gari na kufariki alipofikishwa katika Hospitali ya Amana, baadhi ya wananchi, wakiwamo Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob na mwanaharakati, Godlisen Malisa, wamelieleza gazeti hili kuwa kifo hicho kimegubikwa na utata.

Hata hivyo, jeshi hilo limesema linawasaka Jacob na Malisa kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo na uzushi kwenye mitandao ya kijamii, zinazolenga kujenga chuki na taharuki kwa wananchi dhidi ya taasisi hiyo.


Walichosema Boniface, Malisa

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 23, 2024, Jacob amesema katika taarifa yake hajataja kama Jeshi la Polisi limempiga, ila ameandika maiti imepatikana Hospitali ya Rufaa ya Kilwa Road.

"Binafsi naona jeshi hapo linajihami tu, sijasema wamempiga, isipokuwa tumeelezea mazingira yalivyokuwa yamegubikwa na shaka ndani yake," amefafanua na kuongeza kuwa anasubiri hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi yake.

Kwa upande wake Malisa, amesema taarifa walizochapisha zina ukweli na ndugu wa marehemu wanadai kwa maelezo yao walipofika hospitali hiyo kuulizia maiti imepelekwa na nani walijibiwa na Polisi.

"Mtu huyo aliyeripotiwa ni ndugu yake Boniface na ni kweli taarifa ya kupotea kwake iliripotiwa kwenye mitandao ya kijamii na Polisi. Pili, huyu mtu alikutwa amefariki baada ya kupotea na mwili wake ulipatikana Hospitali ya Kilwa Road, hizo zote ni taarifa za kweli," amesema.


Maelezo ya Polisi

Kamanda Muliro amesema Aprili 11, 2024 saa 10 alfajiri, askari polisi wa usalama barabarani, alipewa taarifa na mwananchi kuwa eneo la taa za kuongozea magari za Buguruni, wilayani Ilala mtu mmoja mwanamume aliyekuwa akivuka barabara eneo la Kimboka kuelekea Chama aligongwa na gari ambalo halikusimama.

"Mtu huyo alipata majeraha makubwa kichwani, kifuani na eneo la chini la mgongo na kisigino cha kulia. Eneo hilo lina watu wengi ambao wanakesha kwa biashara mbalimbali na walishuhudia tukio hilo," amesema.

Amesema mtu huyo alipelekwa na polisi Hospitali ya Amana, lakini baada ya kumfikisha madaktari walibaini alikuwa tayari amekwishafariki dunia.

"Kwa sababu chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Amana kilikuwa hakina nafasi ilishauriwa akahifadhiwe kwenye Hospitali ya Jeshi la Polisi iliyopo Barabara ya Kilwa, Temeke ambayo inatoa huduma hata kwa raia," amesema.

Kamanda Muliro amesema Aprili 21, 2024, ndugu wa marehemu walipatikana na wakautambua mwili, kwani hakuwa na kitambulisho wala simu.

Amesema taratibu za mwisho za mazishi zinafanywa ili akazikwe.


Mochwari Amana

Mwananchi lilipozungumza na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Dk Bryceson Kiwelu kujua iwapo mochwari huzidiwa kiasi cha miili kuhamishwa, amesema:

"Hapana, hatuna hiyo changamoto kwa sasa ila awali tulikuwa nayo, baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kufungwa kupisha ukarabati wa mochwari yao.”

"Baada ya kufungwa miili iliongezeka Amana, lakini pia kuna wale wanaookotwa na Polisi na kuletwa, ilitulazimu kununua jokofu lingine jipya la ziada.

"Kwa sasa hatuna changamoto ya maiti kukaa nje au kupeleka popote. Kwa sababu Muhimbili ni Hospitali ya Taifa maiti zinazookotwa zinatakiwa kupelekwa kwenye maeneo ilikookotwa," amesema.

"Temeke wanashughulikia eneo lao, sisi Amana ni Ilala, Kinondoni, Mwananyamala kwa hiyo tuko vizuri lakini hata Polisi wana Kituo chao cha Ukonga wana mochwari na wanahifadhi, hakuna changamoto," amesema Dk Kiwelu.


Namna ndugu walivyomtafuta

Baadhi ya wanafamilia walisema, walizunguka kwa muda mrefu maeneo tofauti kumtafuta bila mafanikio kuanzia Sikukuu ya Idd el Fitri, Aprili 10 hadi jana Aprili 23 walipoona mwili wake katika Hospitali ya Polisi ya Rufaa ya Kilwa Road, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam katika Kituo Kikuu cha Polisi, Gunda Asheri, anayeishi Tabata Segerea, amesema Mushi ni shemeji yake ambaye ni mdogo wa mke wake.

“Tulimtafuta tangu Aprili 10, 2024 siku ya Sikukuu ya Idd el Fitri. Ni siku ambayo alitoweka na hakuonekana. Tulikuwa tunahangaika hospitali mbalimbali na vituo tofauti vya polisi kutafuta taarifa zake kwa kuwa tulikuwa hatuelewi wapi alikoelekea," amesema.

Amesema wakiwa wanamtafuta, jana kuna taarifa ilitoka kupitia chombo kimoja cha habari kuhusu mwili kuokotwa eneo la Matumbi Darajani.

Asheri amesema taarifa hiyo ilimsukuma afuatilie kujua pengine angekuwa  ndugu yao wanayemtafuta.

"Tulipofika Matumbi katika ufuatiliaji, tukaelezwa mwili umechukuliwa na Jeshi la Polisi, kwa haraka tukaenda Kituo cha Polisi Buguruni. Tuliulizia tukajibiwa hakuna kitu kama hicho," amesema.

Amesema hawakukata tamaa, wakaenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, na  walipofika mochwari hawakuona mwili huo.

"Tulirudi eneo la tukio kuongea na watu wanaozoa mchanga, tuliambiwa doria wanafanya Polisi wa Tabata. Tukaenda Kituo cha Polisi Tabata tulikuta taarifa za ndugu yetu, walituambia mwili upo Kilwa Road Hospitali ya Polisi," ameeleza Asheri.

Amesema baada ya hapo walifunga safari hadi hospitali hiyo ambako walihojiwa na kuruhusiwa kuingia mochwari sehemu ya kutambua miili.

"Tulionyeshwa mwili wa kwanza kuokotwa Matumbi tukaona sio lakini kwa kuwa tulikuwa tumetafuta sana, tukaona tujiridhishe na miili mingine. Tukawa tunafungua jokofu moja hadi jingine, tukajiridhisha na tukaona ule mwili na kuutambua kwa sababu tunamjua," ameeleza.

Amesema walishangazwa kuona kwenye mitandao ya kijamii ikichapishwa taarifa ya ndugu yao.

"Tunaona kinachoendelea mitandaoni ni kutuchafua familia na Jeshi la Polisi, inaonekana kama sisi tumeripoti taarifa hizo, lakini hatuhusiki na chochote," amesema.

Amesema Mushi alikuwa akijishughulisha na biashara na walikuwa wakifanya kazi pamoja eneo la Kariakoo.

"Mushi alikuwa mfanyabiashara wa simu kwa hiyo kipindi cha sikukuu alikuja kwa sababu alikuwa anatengeneza simu, alifunga ofisi yake saa 10 jioni," amesema.

Mushi alikuwa anaishi Kimara Korogwe na ameacha familia ya mke na watoto watatu.

"Njia aliyokuwa anatumia mara nyingi kupita ni Majichumvi -Korogwe au barabara kubwa ya Morogoro," amesema.


Kauli kuwasaka kina Jacob

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema linamsaka Jacob na Malisa kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo na uzushi kwenye mitandao ya kijamii, zinazolenga kujenga chuki na taharuki kwa wananchi dhidi ya taasisi hiyo kutokana na kifo hicho.

Wawili hao wanatuhumiwa kusambaza taarifa za kifo cha Robert Mushi jina maarufu (Baba G), ambaye picha zake zimeambatanishwa kwenye machapisho mtandaoni ikielezwa alipotea Aprili 11, 2024 na baadaye mwili wake kugundulika katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Polisi ya Kilwa Road.

Akizungumza kwenye mkutano na vyombo vya habari, Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema kitendo cha wawili hao kuchapisha taarifa za kifo hicho na kulihusisha Jeshi la Polisi, ni kosa kisheria na katu hakivumiliwi.

"Kutokana na taharuki iliyotengenezwa na kujengwa kwa makusudi kwenye posti zao walionyesha nia ya wazi ya kutengeneza chuki dhidi ya Polisi na Serikali kwa wananchi kuwa mtu huyo aliyepata ajali alikuwa ameuawa na Polisi. Kitendo hicho ni kosa kisheria na hakivumiliki na lazima jeshi lichukue hatua za kisheria dhidi ya wahusika ikiwa ni pamoja na kuwakamata, kuwahoji kwa kina na kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo.’’