Mapya kifo cha mwanafunzi Udom, familia yakoleza utata

Baba wa Merehemu Nusura, Mzee Hassan Abdallah akiwa na Mama wa Marehemu Amina Abdallah wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu kifo cha mtoto wao mkoani Singida jana. Picha na Dotto Mwaibale

Singida/Dodoma. Wakati Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ikitia mguu katika uchunguzi wa kifo cha Nusura Hassan Abdallah, wazazi wake wameibuka pia kukizungumzia huku wakiibua maswali zaidi.

Nusura, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alifariki dunia Mei mosi katika Hospitali ya Faraja iliyopo Himo mkoani Kilimanjaro, huku mazingira ya kifo hicho yakizua utata baada ya kuhusishwa na ajali iliyotokea Dodoma, ikimhusisha pia Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange.

Wakati tukio zima likiendelea kugubikwa na sintofahamu, wazazi wa binti huyo hawakuwa wamezungumza chochote, achilia mbali baba yake mkubwa, Ali Selemani aliyeibua maswali matano.

Jana, baba na mama mzazi wakiambatana na binti yao (dadake Nusura) walijitokeza mbele ya waandishi wa habari mjini Singida kuzungumzia kifo hicho kinachodaiwa kutokea Aprili 29 mwaka huu.

Tofauti na maswali yaliyoibuliwa na baba mkubwa wa marehemu, wazazi hao pia wameibua mengine juu ya kifo hicho ambacho kimeendelea kuzua mjadala.

Katikati ya sintofahamu hiyo, THBUB imesema itafanya uchunguzi huru katika mikoa ya Singida, Kilimanjaro na Dodoma kwa madhamuni ya kujua ukweli wa tukio hilo.


Kauli ya wazazi

Hassan Abdallah, baba mzazi wa marehemu akiambatana na mkewe, Amina Shaban na binti yao Kuruthumu Hassan walikutana na waandishi wa habari nyumbani kwao Uwanja wa Ndege, eneo la Sabasaba mkoani Singida, wakieleza kushangazwa baada ya kukuta “mwili wa binti huyo umevalishwa kanzu.”

Nusura alikuwa anasoma Shahada ya kwanza ya Sanaa katika Elimu, katika Ndaki ya Jinsia na Sayansi ya Jamii.

Walieleza pia kushangazwa jinsi wanavyoendelea kusikia mchumba wa marehemu ambaye wanakiri kumtambua, akiendelea kuvinjari uraiani bila kuchukuliwa hatua hata kuhojiwa.

Pia, kukutwa na matapishi kwenye moja ya nguo za binti yao na namna alivyoumwa bila kupewa taarifa hadi walipopokea kifo.

Familia hiyo ilizungumza jana ikiwa ni siku moja tangu gazeti hili kufika kijiji cha Kikonge, wilayani Iramba ulipozikwa mwili wa Nusura na kuzungumza na wanafamilia wengine, akiwemo baba mkubwa wa marehemu aliyejitambulisha kama Ali Seleman ambaye alidai kifo hicho kina utata na yeye akahoji maswali matano.

Miongozi mwa maswali hayo ni je, Nusura alikuwa na mchumba? Alitokaje Dodoma ghafla kwenda Kilimanjaro? Kwa nini hawakusachi nguo zake wapate tiketi aliyosafiria? Kwa nini ahusishwe na ajali nyingine Dodoma? Kwa nini mdogo wake alikubali kumzika bila kufanya uchunguzi?

Wakati Mzee Ali akihoji hayo, jana wazazi wake Nusura walijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari kuhusu kifo hicho, huku wakijitenga na ajali iliyotokea Dodoma wakidai hadi Aprili 26, mwaka huu walikuwa na mawasiliano na mtoto wao.

Baba wa marehemu Nusura, Mzee Hassan Abdallah alisema wao kama familia hawana kitu chochote cha kuhusisha kifo hicho na mtu mwingine zaidi ya kuomba aliyejitokeza kama mchumba wake ndiye ahojiwe.

“Tunachoweza kujiuliza ni jinsi gani huyo aliyekuwa na binti yetu bado yupo uraiani, hajahojiwa, hatujui kama atahojiwa, lakini hatukujua kuhusu uchumba huo, hakuja kwenye mazishi,” alisema Hassan.

Awali, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Amina Shaban, alisema Aprili 29 mwaka huu alimpigia simu mtoto wake Nusura, lakini iliita mara nyingi na haikupokelewa, kitendo kilichompa hofu kwani hakuwa na kawaida ya namna hiyo.

Mama huyo alisema siku iliyofuata aliendelea kumtafuta kwenye simu lakini hakupatikana, ndipo ikabidi afanye juhudi kutafuta namba ya simu ya rafiki yake ambaye pia ni mwanafunzi wa UDOM.

“Mwanafunzi huyo akaniomba nimpe nafasi amtafute halafu angenipa majibu, hakufanikiwa kumpata mwanangu, ndipo akaniomba nipokee namba ya mwanafunzi mwingine ambaye pia ni rafiki wa Nusura,” alisema Amina.

Alisema siku iliyofuata alimpigia mwanafunzi huyo ambaye alimjulisha mtoto wake hayupo alikwenda kwa mchumba wake aliyeko Marangu mkoani Kilimanjaro, ambaye kwa mujibu wa maelezo ya mama huyo alishaelezwa habari za uchumba huo.

Alisema mtoto wake, Nusura, wakati akiwa kwenye mazoezi ya vitendo (field), alipata mchumba (jina tunalihifadhi) ambaye ni Mwalimu kwenye shule ya sekondari iliyopo Marangu ambayo hata hivyo hakuitaja.

“Mwanafunzi huyo alisema, siku za hivi karibuni, Nusura alitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa mchumba wake huyo kupitia simu, kwamba anamhitaji haraka Marangu na mwanangu alimuonyesha ujumbe huo rafiki yake huyo wanayesoma naye, hata hivyo, mwenzake alihoji ni kwa nini anatumiwa meseji za aina hiyo,” alisema Amina.

Kwa mujibu wa mama huyo, licha ya rafiki yake kuhoji hayo, lakini Nusura alifunga safari kwenda Marangu, Kilimanjaro kwa ajili ya kuonana na mchumba wake huyo ambaye hata hivyo familia haimfahamu.

Alisema mbali na taarifa hiyo, kijana huyo hakuonekana hospitalini, hakuonekana msibani na wala haijajulikana hizo meseji alizomtumia zilihusu nini, lakini walishangazwa kukuta mwili umevishwa kanzu.

“Ndipo nikampigia simu huyo kijana ambaye kwa kweli hakuna mtu ambaye anamfahamu, hata kwa sura, ndipo akasema mwanafunzi alifika kwake lakini aliugua homa ya ghafla na kufariki dunia,” alisema


Mshangao wa dada

Akizungumza kwenye kusanyiko hilo, Dada yake na marehemu, Kuruthumu Hassan, alieleza kushangazwa mwili wa marehemu Nusura kupelekwa ukiwa umevalishwa kanzu wakati Nusura alikuwa ni mwanamke.

Kuruthumu alisema hadi sasa hawajashirikishwa kuhusu kifo cha ndugu yao huyo na hawajui matapishi na mabaki ya chakula waliyoyaona kwenye moja ya nguo za marehemu, ambayo wanazo taarifa yamepelekwa kwa mkemia.

“Kwa mtindo huu, tuna uhakika hatutapata sababu halisi iliyochangia kifo cha ndugu yetu kama hayo majibu ya wakemia hayajatufikia, lakini tunasikitishwa zaidi na kwa nini (anamtaja huyo mchumba wa mdogo wake), bado yupo uraiani, hajachukuliwa hatua zozote za kisheria,” alisema Kuruthumu.


Tume yajitosa

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Tume Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alisema takribani wiki mbili, tume imekuwa ikiona katika vyombo vya habari taarifa inayohusu ajali ya Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Ndugange iliyotokea Dodoma ikihusishwa na kifo cha mwanafunzi huyo.

Jaji Mwaimu alisema taarifa hizo zimenukuliwa kutoka Jeshi la Polisi, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, Mkoa wa Kilimanjaro na taarifa za wananchi kupitia mitandaoni.

Hata hivyo, alisema Tume inatambua uwepo wa vyombo vinavyoshughulikia masuala ya haki jinai, hususani Jeshi la Polisi na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kwamba Tume inavipa heshima vyombo hivyo katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Tume imeazimia kufanya uchunguzi huru kwa madhumuni ya kubaini ukweli kuhusu matukio hayo,” alisema mwenyekiti huyo.

Alipoulizwa watajikita katika maeneo yapi katika uchunguzi huo, alisema watafanya katika maeneo yote yaliyotajwa Dodoma, Kilimanjaro na Singida ili kupata ukweli hasa kwa kuzingatia kwamba yanasemwa mambo mengi kutoka maeneo tofauti na taarifa zinapishana.

Jaji alisema uchunguzi utaanza mara moja na mchakato unaendelea na mara watakapokamilisha watatoa majibu ili kuondoa sintofahamu katika jamii.