Utata kifo cha Nusura, ni giza nene kijijini

Mwanafunzi, Nusura Hassan Abdalla enzi za uhai wake.

Iramba. Vumbi linazidi kutimka kwenye sakata la kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Nusura Abdallah baada ya ndugu kutilia shaka uharaka wa mazishi yake na kuibua maswali matano.

Wakati umma ukiendelea kupaza sauti ukitaka majibu ya uchunguzi wa kifo hicho, mwanamume anayedaiwa kuwa mpenzi wa mwanafunzi huyo na aliyempeleka Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, ameruka viunzi kulizungumzia.

Vilevile, kwa nyakati tofauti jana viongozi wa taasisi za wanafunzi walisita kuzungumzia sakata hilo linaloendelea na uchungzi.

Wakati hayo yakiendelea, Ofisi ya Rais Tamisemi imetoa taarifa kwa umma ikikanusha taarifa za mitandaoni kuwa Naibu Waziri Dk Festo Dugange amejiuzulu wadhifa wake ili kupisha uchunguzi wa sakati hilo.

“Taarifa hiyo ni uzushi na wananchi wanaombwa kuipuuza, kwani Dk Dugange hajajiuzulu wadhifa wake huo. Bado ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi na Mbunge wa Wang’ingombe mkoani Njombe anaendelea na matibabu Hospitali ya Benjamin Mkapa,” ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Nteghenjwa Hosseah, msemaji wa ofisi hiyo.

Msingi wa madai hayo ni taarifa za mitandaoni zilizohusisha kifo cha Nusura na ajali aliyopata Dk Dugange, taarifa ambazo tayari zinachunguzwa na Polisi, Ofisi ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na vyombo vingine vya haki jinai.

Uchunguzi huo unafanyika, licha ya awali jeshi hilo mkoani Dodoma kukanusha taarifa zilizokuwa zinasambaa kuwa katika ajali hiyo Dk Dugange alikuwa na mwanamke ambaye alifariki dunia.

Maswali matano

Mbali na uchungizi huo,  Mwananchi limezungumza na baba mkubwa wa marehemu aliyejitambulisha kama Ali Seleman, alidai kifo hicho kina utata na yeye ana maswali matano yanayomuumiza kichwa.

Alidai siku ya mazishi yalifika magari matano yakiwa na mwili wa marehemu na waombolezaji na baada ya mazishi wakaondoka.

“Mmmm, kuna utata. Ukiniuliza naweza kusema kifupi hapa ndipo alipozikwa, lakini maswali mengi nitashindwa kuyajibu. Baba wa huyu mtoto ni mdogo wangu tumbo moja, lakini msiba ulivyofika hadi tunazika bado sielewi,” alidai  Ali.

Ali (67) anaishi Kitongoji cha Mtakuja kijijini Kikonge, kwenye eneo la familia huku mdogo wake (baba wa Nusura) yeye akiishi Mtaa wa Kiwanja cha Ndege, mjini Singida ambako msafara wa kusindikiza mwili wa Nusura ulianzia.

Mzee Ali anadai yapo maswali matano ambayo angetamani kuyajua kuhusu msiba wa binti huyo, lakini kwa namna ilivyo ameshindwa na amekosa mtu wa kumjibu, kwani yeye na mdogo wake walikaa muda usiozidi saa moja walipofika hapo kuzika, kisha wakaondoka na msafara wote.

Miongozi mwa maswali hayo ni je, Nusura alikuwa na mchumba? Alitokaje Dodoma ghafla kwenda Kilimanjaro? Kwa nini hawakusachi nguo zake wapate tiketi aliyosafiria? Kwa nini ahusishwe na ajali nyingine Dodoma? Kwa nini mdogo wake alikubali kumzika bila kufanya uchunguzi?

“Hili la kufanya uchunguzi wa mwili lilikuwa muhimu, lakini hadi tunamzika mimi sikuwa najua kuhusu utata, baadaye ndiyo wanakijiji nasikia wanasema. Mwanzo nilipokea taarifa kwamba Nusura amefariki ghafla na baadaye mdogo wangu akasema tuandae malalo wanakuja kuzika huku,” anadai.

“Lakini siku ya kumsitiri ulikuja msafara wa magari kama matano hivi, walifikia eneo la kaburi kama unavyojua mdogo wangu hana mji hapa, ile wamemaliza kuzika akasema hakuna arobaini na msiba ndio umekwisha hapo. Mimi sina simu nizungumze naye, kwa hiyo hadi nitafute nauli nikamhani huko mjini,” alidai

Hata hivyo, anadai aliambiwa msiba ulitokea Moshi ambako anasema wapo ndugu wachache huko na kwamba mdogo wake (baba mzazi wa marehemu) alifanya kazi kwa miaka mingi katika Kiwanda cha Sukari TPC.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtakuja, Omari Said ambaye anaishi jirani na lilipo kaburi la binti huyo, alidai mazingira ya msiba tangu awali yalishaonyesha utata na hata mazishi yenyewe yaliwaacha wenyeji na sintofahamu.

Said anadai    mara baada ya kupokea taarifa za msiba, hakukuwa na maelezo zaidi wala mtu aliyetoka mjini ambaye angeweza kuwasimulia mkasa mzima isipokuwa waliombwa kutafuta vijana wachimbe kaburi kwa ajili ya maziko.

“Basi niliita vijana na Mzee Ali akatuonyesha mahali pa kuchimba, wale wenzetu walikuja na magari kama matano au sita hivi wakazika na muda huo huo wakaondoka wote, tukabaki sisi ambao tangu mwanzo hatukuwa tunajua kitu,” alisema.

Hata hivyo anasema alimfahamu binti huyo wakati wa uhai wake, kwani amewahi kufika hapo mara kadhaa kwa shangazi yake ambayo ni nyumba ya tatu kutoka anapoishi mwenyekiti huyo na kwamba alikuwa na taarifa kuwa anasoma Dodoma.

Kiongozi huyo anasema kuna mkanganyiko wa taarifa kwa kuwa awali waliambiwa Nusura alifikwa na mauti akiwa Dodoma, lakini ghafla wakapata taarifa alikuwa Moshi, hivyo hawajafahamu mazingira halisi.


Mpenzi wa Nusura aingia mitini

Jitihada za Mwananchi kumtafuta mwanamume anayetajwa kama mpenzi wa Nusura (jina tunalo), anayetajwa na uongozi wa Hospitali ya Faraja kuwa ndiye aliyempeleka hapo ziligonga mwamba baada ya kutoa miadi isiyotekelezeka.

Mei 7, mwaka huu, mwanamume huyo, aliyetajwa kuwa na umri wa miaka 47 aliahidi kuonana na mwandishi wa gazeti hili mjini Moshi, akitokea Arusha lakini alipotafutwa muda aliotaja alisema amebanwa kikazi hivyo, hataweza na kusisitiza kuwa hataki kuzungumzia suala hilo kwenye simu.

Alisisitiza anataka kuonana na mwandishi kwa ana kwa ana kwa kuwa hakuwa na uhakika kwamba kweli ni mwandishi
Mei 8, 2023 alipotafutwa tena kama alivyoahidi, pia ilishindikana na kuahidi tena siku iliyofuata (jana) jijini Arusha.

Mwandishi alipomfuata Arusha na kumpigia simu kujua alipo ili amfuate kwa mahojiano, alimweleza kuwa hayupo tena Arusha, bali yuko njiani anaelekea Singida kuwapeleka ndugu wa waliofiwa.


Nyumbani Singida

Katika Mtaa wa Kiwanja cha Ndege kwenye nyumba ya kawaida, masufuria yamejaa nje kuashiria kulikuwa na pilika za chakula cha kusanyiko. Hata hivyo inakuwa vigumu kuwapata wazazi wa Nusura, kwani sharti la hapo ni kutokusema kitu kwa sasa kwa madai kuna vyombo vinachunguza.

Hata hivyo mdogo wake anayeitwa Ummukulthum anatoka nje na kuzungumza kwa ufupi: “Tumempoteza mtu muhimu ambaye tulimtarajia kuwa msaada kwa siku za usoni, ni dada yangu tumezaliwa pamoja yeye akiwa mtoto wa tatu, baba hawezi kusema hadi hapo vyombo vya uchunguzi vitakapomaliza kazi yao.”

Binamu wa marehemu, Seleman Segu ambaye ni mtoto wa shangazi ya marehemu Nusura, anasema kuwa kilichoficha ukweli wa msiba wa dada yake si aliyefariki, bali uharaka wa kumzika.

Seleman anaeleza kuwa taarifa za msiba zilitolewa kwa haraka wakati huo naye alikuwa Moshi, lakini alipokwenda kufuatilia kwa ndugu wakasema tayari wamesafirisha na siku ya pili anafunga safari kurudi nyumbani akaambiwa wamezika mchana huo.

“Muulize mtu yeyote, mimi nilimwambia mjomba kwamba tulichofanya si chema, hili jambo tungejua ukweli wake kama pangefanyika uchunguzi kidogo wa mwili kabla ya kuzika, haya maswali tusingeulizwa lakini mjomba wangu dini imemkaa sana, ndiyo maana kila kitu kwake ni ndiyo tu,” anasema.

Seleman anasema taarifa zilimkuta akiwa TPC Moshi akifuatilia haki zake baada ya kupunguzwa kazini, lakini anasema mbali na mahusiano mazuri yaliyokuwepo baina yake na dada yake huyo, hakuwahi kusikia kama alikuwa na mchumba.

Gazeti hili lilifanya jitihada za kumpata Hassan Abdallah, baba mzazi wa marehemu, ikiwemo kufika nyumbani kwake, mjini kati eneo maarufu la Stendi ya Zamani, mkoani Singida bila mafanikio.

Kabla ya kwenda, mwandishi alipata taarifa kuwa hakuwa tayari kuzungumza jambo hilo, ambalo hakuliamini.

“Nilipofika hapo nilipokewa na mtu aliyeomba nikaribie ndani wakati anakwenda kuwaita wenyeji.  Ndipo alifika msichana anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 19 hadi 20 aliyenidadisi kwa maswali mengi, kisha akasema haitawezekana kuwaona wenyeji.

Sasa wewe kama si ndugu huwezi kumuona mzee, kwani anatakiwa kutosema jambo lolote kuhusu msiba,” alisema binti huyo  aliyeeleza kuwa marehemu ni dada yake.

Safari ya kijijini

Umbali wa kurusha jiwe kutoka katika nyumba ndogo ya matofali ya udongo upande wa magharibi, kuna tuta ambalo pembeni kuna miti minne iliyochomekwa katika kila kona.
Haihitaji kuambiwa lakini kwa mila za Kiafrika hili ni kaburi, tena ni la muda usiozidi wiki moja katika eneo ambalo lina kaburi moja pekee, chini ya mti unaojulikana kwa lugha ya wenyeji ‘msugala’.

Safari ya kufika hapo ilikuwa ni kushuhudia mahali ulipolala mwili wa Nusura. Watu wawili wamefika hapo – Baba mkubwa wa marehemu na mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtakuja kijiji cha Kikonge wilaya ya Iramba mkoani Singida.

“Ni hapa hapa ndipo tulipomsitiri binti yetu, inaumiza mioyo lakini kwenye ukoo bado kuna maswali makubwa matano hayana majibu, hata hivyo mtoaji ni Mungu na anayetwaa ni yeye kwa wakati wake, acha iwe hivyo,” anasema mmoja wao.

Safari hadi Kikonge

Ili kufika katika kijiji cha Kikonge ambacho ni kikubwa, yakupasa kujifunga mkanda na hasa ukiwa mgeni na mazingira ya usafiri wa eneo husika.

Anzia Singida mjini, popote ulipo waulize wenyeji wakupeleke stendi ya Mkombozi, imeitwa hivyo kwa sababu ukuta wake unapakana na Shule kongwe ya Msingi Ukombozi. Usafiri wa hapa ni gari ndogo aina ya Noah.

Kwa hakika jifunge mkanda, ni mateso na adhabu kwa mgeni, lakini ni wanaishi sawa na msemo wa wahenga hiari yashinda utumwa, kwani burudani ya muziki inatosha kuwaburudisha na kuwaliwaza.

Watu wazima ndani ya Noah tulikuwa 17, watoto wawili, juu mizigo usipime. Safari inaanzia Mkombozi tunazunguka kupitia Sekondari ya Senge kisha kutokeza Uhasibu. Kumbuka njia hiyo inatusaidia kuwakwepa askari wa usalama barabarani.

Mbele kidogo anaongezeka abiria ambaye anakwenda kukaa juu ya mizigo kukamilisha idadi ya watu 20 kwenye gari hilo lenye uwezo wa kubeba watu wanane wanaomjumlisha dereva.

Sikiliza, tunakaa hivi, dereva mbele amekaa na watu wazima wawili na mtoto mmoja ambayo jumla yao ni wanne, yeye akiendesha kwa kukaa upande, sehemu ya pili wamekaa wanne, sehemu ya tatu wanne wakimpakata kijana wa darasa la nne au tano lakini viti vyao vimelazwa ili kupisha watu wanne kukaa nyuma sehemu ya mizigo.

Mtu mmoja amejikunja akisimama sehemu ya kati na kulalia mwegemeo wa viti vya nyuma huku mwingine akikaa juu ya gari kulinda mizigo.

Ni kweli kuwa barabara si ya lami lakini haina mashimo kama maeneo mengine, lakini mwendo wa gari hiyo unaweza kuomba maji. Tunatumia dakika 87 kufika kituoni na anayeshuka ni mimi peke yangu, gari likielekea Ndola ambako ndiko mwisho wa safari.

Ili usijazane hivyo, yakupasa kupanda pikipiki hadi Kaselya (mahali alipozikwa Isack Sima, daktari aliyeuawa kwa mapanga wilayani Tarime wiki iliyopita) .

Katika eneo hilo, Noah zinabeba watu 10 tu lakini gharama yake ukijumlisha na usafiri wa pikipiki ni sawa na nauli ya basi kutoka Singida kwenda Mwanza.


Subira Tahliso, Udoso

Gazeti hili lilipomtafuta Rais wa Shirikisho la Vyama vya wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Maria Thomas kuhusu sakata hilo na ukimya wao, alisema kwa kifupi “tunasubiri uchunguzi (wa Polisi, DPP na mkemia mkuu wa Serikali) na hatuwezi kutoa kauli yoyote kwa sasa.”

Naye Rais wa Chama cha Wanafunzi Udom, Udoso, Tryphone Mwinuka alipoulizwa kuhusiana na kifo cha mwanafunzi mwenzao, alisema hawawezi kutoa tamko tofauti na lililotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Udom, Profesa Lughano Kusiluka.
 

“Taarifa zozote zinazohusiana na masuala ya uhusiano na matangazo kuna idara maalumu ambazo zinatoa taarifa kwa umma, lakini msemaji mkuu ni Makamu Mkuu wa Chuo na tamko lake lilishaonekana kupitia barua ya ofisa uhusiano, hata taarifa zetu sisi wanafunzi nazipeleka kwa makamu,” alisema Mwinuka.

Ilivyokuwa hospitali

Taarifa kutoka hospitali hiyo zilizomnukuu daktari aliyemhudumia, Peter Minja zilieleza mwanafunzi huyo alifikishwa hospitalini hapo Mei 1, mwaka huu kati ya saa 2 na 3 usiku na mpenzi wake akiwa mahututi.

Kwa mujibu wa daktari huyo, vipimo vya awali vilionyesha sukari ilikuwa juu katika kiwango kisicho cha kawaida, huku akiwa na upungufu wa damu na kwamba alifariki dunia wakati madaktari wakiendelea na jitihada za kukokoa maisha yake.

Hata hivyo, pamoja na maelezo hayo, mitandao ya kijamii imekuwa ikihusisha kifo hicho na ajali iliyotokea usiku wa Aprili 26, mwaka huu jijini Dodoma, huku wengine wakikihusisha na kipigo, masuala ambayo yanachunguzwa.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alipotafutwa tena jana ili kufahamu maendeleo ya uchunguzi huo, aliwataka wananchi kuendelea kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho uchunguzi unaendelea na uchunguzi ukikamilika umma utajulishwa matokeo.