Polisi yaanza uchunguzi kifo tata cha mwanafunzi Udom

Mwanafunzi, Nusura Hassan Abdalla enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Jeshi latangaza kuanza uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi. Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime ametoa taarifa hiyo leo Jumamosi Mei 6, 2023.

Dodoma. Jeshi limetangaza kuanza uchunguzi wa kifo cha mwanafuzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania David Misime ametoa taarifa hiyo leo Jumamosi Mei 6, 2023.

 Taarifa za kifo cha Nusura Hassan Abdallah zimekuwa na utata kama kilitokea Dodoma au Kilimanjaro katika Hospitali ya Faraja.

Hata hivyo Misime amesema kuwa taarifa hizo zinazohusisha kifo hicho na ajali illiyotokea jijini Dodoma Aprili 26, 2023 ikimhusisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi (Afya), Dk Festo Dugange, zinafanyiwa uchunguzi.

Awali ilielezwa kuwa kifo chake kilitokana na kipigo kutoka kwa mpenzi wake wakiwa Kilimanjaro.

"Polisi Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kuona taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii na sababu zinazotolewa, wameshaanza uchunguzi kwa watu mbalimbali, hospitalini alikotibiwa binti huyo ambapo amesema wanashirikisha Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na wadau wengine wa haki jinai," inasema sehemu ya taarifa ya Polisi.

Jeshi hilo limetoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa zilizosahihi na zenye ukweli asisite kutoa taarifa hizo ili kuharakisha uchunguzi wa tukio hilo.

Kwa mujibu wa Misime uchunguzi wa tukio hilo ukikamilika taarifa kamili ya kilichobainika kitatolewa kwa umma na kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.