UDOM yathibitisha kifo cha mwanafunzi anayetajwa mitandaoni

Mwanafunzi, Nusura Hassan Abdalla enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Baada ya kusambaa kwa taarifa juu ya mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya masomo ya sanaa katika Elimu (BAED), Nusura Hassan Abdallah, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimevunja ukimya juu ya kifo hicho.

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kimethibitisha kufariki dunia kwa mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya Sanaa katika Elimu, katika Ndaki ya Insia na Sayansi ya Jamii, NusuraHassan Abdallah ambaye tangu mwanzoni mwa wiki taarifa zake zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya jamii.

 Bila kutaja sababu za kifo chake, taarifa zilizotolewa na kitengo cha masoko na mawasiliano  Ijumaa Mei 5, 2023 imesema Mei 3, 2023 menejimenti ya chuo hicho ilipokea taarifa kutoka kwa mwanafunzi anasoma naye kuwa amepokea taarifa kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa mjomba wake Nusura akimjulisha kuwa mwanafunzi huyo amefariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Faraja iliyopo Himo mkoani Kilimanjaro.

Hata hivyo, taarifa hiyo imesema hadi kufikia Aprili 27, 2023 Nusura alionekana chuoni akiendelea na masomo.

"Tukizingatia kwamba masomo yanaendelea menejimenti ya chuo ikifanya juhudi za ziada na kufanikiwa kumpata dada yake Nusura anayeishi Uchira mkoani Kilimanjaro ambaye alithibitisha kutokea kwa kifo cha mdogo wake," imesema.

Imesema taarifa zaidi zinaonyesha kuwa mwili wa marehemu ulisafirishwa Mei 3, 2023 kutoka Moshi hadi nyumbani kwao Iramba mkoani Singida.

Imesema menejimenti ya chuo hicho imesikitishwa sana na msiba huo na inatoa pole nyingi kwa familia ya marehemu Nusura.