Aliyefungwa miaka 30 kwa kukiri shtaka la bangi ashinda rufaa

Muktasari:

 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru Adam Abdallah baada ya kushinda rufaa yake.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemwachia huru Adam Abdallah, aliyekuwa amehukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 30, jela baada ya kupatikana na hatiani kusafirisha kilo 23 za bangi.

Uamuzi huo wa kumwachia huru mshtakiwa huyo umetolewa leo Jumatano, April 3, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi, aliyepewa mamlaka ya ziada kwa ajili ya kusikiliza rufaa aliyoikata Abdallah kupinga hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani.

Mrufani huyo alihukumiwa kifungo hicho na Mahakama hiyo mwaka 2023, baada ya kukiri shtaka lake wakati kesi yake ikiwa katika hatua ya usikilizwaji ushahidi wa upande wamashtaka.

Abdallah baada ya kuhukumiwa kifungo hicho, alikata rufaa kupinga hukumu hiyo yote yaani hatiani na adhabu aliyopewa huku akiwasilisha hoja kuwa hukumu hiyo ilikuwa na mapungufu kisheria, kutokana na kutokufafanua kuwa alikiri nini.

Mahakama Kuu katika hukumu yake imekubaliana na sababu hiyo ya rufaa ya Abdallah, na kutengua hatia na adhabu iliyotolewa dhidi yake na Mahakama ya Wilaya.

Hakimu Msumi amesema hukumu hiyo, kasoro za kisheria kutokana na kutokufafanua kuwa nini ambacho mrufani (mshtakiwa) alikiri.

Amesema ingawa upande wa mjibu rufaa (Jamhuri) wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo ulidai ni kweli mshtakiwa alikiri shtaka lake, lakini haukutoa kielelezo chochote mahakamani kuonyesha mrufani amekiri kitu gani.

"Mahakama ya Wilaya ya Kisarawe, ilimtia hatiani mshtakiwa baada ya kukiri kosa lake, lakini hakukuwa na maelezo ya kukiri kwake kulikuwa kwa namna gani.  Kulitakiwa kuwe na maelezo yanayoonyesha kukiri kwake," amesema Hakimu Msumi na kuamuru:

"Kwa sababu hiyo, adhabu ya kifungo cha miaka 30 alichokuwa amepewa Abdallah nakifuta na naondoa adhabu aliyokuwa amepewa, hivyo namwachia huru."

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, upande wa mjibu rufaa uliomba kuwa kama Mahakama hiyo itakubali kuwa hiyo ilikuwa ni kasoro basi tiba yake iamuru kesi hiyo isikilizwe upya.

Hata hivyo, Hakimu Msumi amelikataa ombi hilo akisema kama akitoa amri kesi hii ianze kusikilizwa upya, uamuzi huo utawapa fursa upande wa mashtaka kurekebisha makosa yao.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Abdallah alikuwa anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 23, 2021 katika kijiji cha Boga kilichopo wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani.

Alidaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa alikutwa akisafirisha kilo 23.18 za bangi, kinyume cha sheria.

Ilidaiwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa kituo cha Polisi, alifikishwa mahakamani Januari 27, 2021 na kusomewa shtaka linalomkabili.

Lakini wakati kesi hiyo inaendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka, Januari 5, 2023, mshtakiwa aliomba kukumbushwa shtaka lake kwa kusomewa upya na aliposomewa, alikiri kuwa ni kweli.

Kutokana na maelezo hayo ya kukiri, mahaka hiyo ilimtia hataini na kuhukumiwa adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 30 jela.

Hata hivyo, Abdallah baadaye alikara rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupinga hukumu hiyo yote, yaani hatia na adhabu.