Aliyejirusha ghorofani azikwa Dar, Mchungaji asema…

Muktasari:

  • Mwili wa Joel Misesemo aliyejirusha katika jengo la ghorofa la Derm Plaza lililopo Makumbusho, jijini Dar es Salaam, umezikwa makaburi ya Kinondoni jijini humo.

Dar es Salaam. Safari ya mwisho hapa duniani ya Joel Misesemo imehitimishwa kwa mwili wake kuzikwa katika makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

 Mwili wa Misesemo aliyekuwa mshereheshaji (MC) na mtaalamu wa masuala ya ushauri umezikwa leo Ijumaa, Mei 26, 2023 na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji.

Misesemo alifikwa na mauti alfajiri ya Mei 23, 2023 kwa kujirusha kutoka ghorofani ya jengo la Derm Plaza lilipo Makumbusho jijini humo.

Safari hiyo ya mwisho ya Misesemo aliyezaliwa Agosti 29, 1984, Ushetu mkoani Shinyanga imeanzia Kanisa la Kipentekoste Dar es Salaam (DPC) Kinondoni, ambapo ilifanyika Ibada na waombolezaji kupata fursa ya kuuaga mwili wake.

Katika mahubiri yake, Mchungaji Abel Majaliwa amesema, sio jambo zuri kwa mtu kukaa na matatizo bila kushirikisha au kuomba ushauri kwa watu kwani matokeo yake huwa ni mabaya.

Amasema ni vyema watu kutambua kila mmoja ni mshauri wa mwenzake kwa hiyo, “tusikubali kukaa na matatizo, tuyaweke wazi, tukubali kushauriwa ili kuepusha matokeo yasiyo mazuri.”

“Kila mtu ni mshauri katika nafasi yake na hakuna mtu ambaye hajawahi kumshauri mtu,” amesema Mchungaji Majaliwa

Pia amesema kama kanisa inabidi kutambua kifo cha Joel ni mipango ya Mungu na sio amejiua kwa makusudi kama taarifa nyingine zinavyoeleza.

Marehemu ameacha mke ambaye hawakubahatika kupata mtoto. Hata hivyo, analea watoto zaidi ya 10.