Aliyejirusha ghorofani kuzikwa Ijumaa

What you need to know:

  • Joel aliyekuwa akifanya shughuli za ushehereshaji juzi alijirusha kutoka ghorofa ya saba ya jingo hilo hadi chini, huku mapaka sasa, hakuna taarifa zozote zenye kuonyesha sababu za yeye kufanya hivyo.

Dar es Salaam. Mwili wa marehemu Joel Misesemo aliyejirusha katika jengo la ghorofa la Derm Plaza lililopo Makumbusho, unatarajiwa kuzikwa Ijumaa katika makaburi ya Kinondoni jijini humo.

Joel aliyekuwa akifanya shughuli za ushehereshaji juzi alijirusha kutoka ghorofa ya saba ya jengo hilo hadi chini, huku mpaka sasa, hakuna taarifa zozote zenye kuonyesha sababu za yeye kufanya hivyo.

Akizungumza leo Jumatano Mei 24, 2023 nyumbani kwa marehemu maeneo ya Mwananyamala Mtaa wa Igusule, baba mzazi wa marehemu, Mattson Misesemo, amesema kwamba, kutokana na hali mbaya ya mwili wa mtoto wake, maziko yatafanyika keshokutwa.

Akielezea namna alivyopata taarifa za kifo cha mtoto wake huyo, baba wa marehemu amesema alizipata kutoka kwa mtoto wake mkubwa anayeishi mkoani Kigoma licha ya yeye kuishi Makumbusho jijini humo.

Hata hivyo alipoulizwa kama kuna chochote kilichokuwa kinamsibu mtoto wake kabla ya kufikwa na umauti Misesemo mesema:

"Ninachojua mtoto wangu alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi kwa muda mfupi lakini alipata matibabu na kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

"Pia Joel hajawahi kunitaarifu changamoto yeyote kuhusu maisha yake kwani alikuwa anaishi na mke wake vizuri na sijui nini kilimpata hadi akaamua kujirusha ghorofani, roho inaniuma sana na kifo hiki," amesema baba huyo.

Baadhi ya majirani waliomzungumzia marehemu akiwemo Baja Hanun kwamba waliishi naye vizuri kwa miaka nane katika mtaa huo.

"Joel alikuwa ni mtu wa watu, alijichanganya na kuongea na kila mtu hapa mtaani; tumepata mshtuko mkubwa sana kuondokewa na mtu ambaye alikuwa mtu wa watu," alisema.

Rahma Saidi alisema wanachokijua marehemu enzi za uhai wake katika ghorofa ambayo umauti ulimkuta alikuwa akienda kufanya mazoezi kipindi alivyokuwa mgonjwa.

Mmoja wa wanafamilia aliyejitambulisha kwa jina la Janeth Andendekise, amesema alilelewa na Joel tangu mwaka 2016 alipopata matatizo ya kuumwa mguu na alikuwa akimuita babu.

"Baada ya wazazi wangu kufariki nilipitia changamoto mbalimbali za kimaisha ikiwemo kuumwa lakini nilipokutana na Joel alinipokea na kukubali kuishi na mimi tangu mwaka 2016 mpaka nilipoweza kwenda kupanga kwangu," amesema Janeth.

Hata hivyo amesema mara ya mwisho kuzungumza naye ilikuwa Jumatatu akiwa visiwani Zanzibar anapofanya shughuli zake za biashara na kumtaarifu kuwa amepata mchumba na yupo mbioni kwenda kumtambulisha.

"Wakati naongea na babu (Joel) alionekana na utofauti kwamba kuna kitu hakipo sawa lakini kila nilipomuuliza aliniambia yupo vizuri mpaka pale bibi (mke wa Joel) alipokuja kuniambia ukweli kwamba alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kupooza na waliogopa kuniambia na jana ndipo nilipopata taarifa ya msiba wake," amesema Janeth.

Janeth amesema marehemu alikuwa ni mtu wa kusikiliza matatizo ya watu wengine lakini mgumu kusema ya kwake jambo ambalo anahisi kuna kilichokuwa kinamsumbua na kuamua kuchukua maamuzi hayo.

Amesema marehemu hakuwahi kufanikiwa kuwa na mtoto na alikuwa akiwalewa watoto wa watu wengine wanne waliopitia matatizo mbalimbali.