Ajiua kwa kujirusha toka ghorofa ya saba

What you need to know:

  • Joel Misesemo mkazi wa Mwananyamala anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 na 40 amefariki baada ya kujirusha kutoka ghorofa ya saba kwenye jengo la Derm Plaza lililopo Makumbusho.

Dar es Salaam. Katika tukio la simanzi na kushangaza, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Joel Misesemo anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 na 40, mkazi wa Mwananyamala; amejirusha kutoka ghorofa ya saba katika jengo la Derm Plaza lililopo Makumbusho, kitendo kilichomsababishia mauti.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo Jumanne Mei 23 2023, imeeleza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa marehemu alionekana katika jengo hilo saa 11:40 alifajiri ambapo alimweleza mlinzi wa zamu kuwa anaenda kufanya ibada kwenye msikiti uliopo ghorofa ya 15 ndani ya jengo hilo.

Hata hivyo muda mfupi baadaye mtu huyo alijirusha kutoka ghorofani, mifumo ya kamera katika jengo hilo, inamuonesha akijirusha kwa makusudi kutoka ghorofa ya saba kupitia dirishani.

“Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi, Jeshi la Polisi limepata gari la marehemu aina ya Suzuki T142 DRM lililokuwa limeegeshwa kwenye katika eneo hilo, na limehifadhiwa kituo cha Polisi Oysterbay,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia imeeleza uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kujua chanzo na sababu za tukio hilo.

Matukio kama hayo yamekuwa yakijirudia ambapo Mei, 2022 tukio kama hilo lilitokea ambapo mtu mmoja aliyejulikana kwa kwa jina la John Mahundi, mkazi wa Magomeni Kota alikutwa amefariki baada ya kujirusha kutoka gorofa ya saba.