Aliyekuwa kocha Simba asomewa mashtaka upya

Muktasari:
- Kocha wa makipa wa timu ya Simba, Muharami Sultan (40) na wenzake watano wamesomewa upya mashtaka nane katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Dar es Salaam. Kocha wa makipa wa timu ya Simba , Muharami Sultan (40) na wenzake watano wamesomewa upya mashtaka nane likiwemo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin Hydrochloride zenye uzito wa kilo 27.1 pamoja na utakatishaji wa fedha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mbali na Zuberi wengine ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zubery Seif, Said Matwiko mkazi Magole, Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54) mkazi wa Kisemvule ambaye ana undugu na mtuhumiwa Muharami, John John maarufu Chipanda (40) mkazi wa Kitunda ambaye jukumu lake kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy na Sarah Joseph.
Washtakiwa hao wamesomewa upya mashtaka hayo leo, Septemba 23,2023 na Wakili Yusuph Aboud mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Mathias baada Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwafutia mashtaka matano yaliyokuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio chini ya kifungu cha 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Aboud akisoma hati ya mashtaka alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu, kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride na utakatishaji fedha.
Alidai katika shtaka la kwanza linalowakabili washtakiwa wote inadaiwa kuwa tarehe tofauti kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 maeneo tofauti ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani washtakiwa waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride.
Katika shtaka la pili inadaiwa kuwa Oktoba 27, 2022 katika eneo la Kivule wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam mshtakiwa hao kwa pamoja walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye uzito wa kilo 27.10.
Katika shtaka la tatu inadaiwa kuwa Novemba 4, 2023 washtakiwa, Zuberi Zungu na Mtwiko katika eneo la Kamegele Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, walikuwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye uzito wa Kilogramu 7.79.
Pia katika shtaka la nne, tano, sita na saba ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili mshtakiwa Kambi inadaiwa kuwa Aprili 15, 2021 katika Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam alinunua magari manne aina ya TATA yenye jina Safia Group of Companies Ltd huku akijua mali hizo zilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Katika shtaka la nne inadaiwa kuwa Aprili 20,2021 mshtakiwa Kambi alinunua gari aina ya TATA yenye jina Safia Group of Companies Ltd akijua mali hiyo ilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
"Upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea hivyo aliiomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," alidai Aboud.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Mathias aliwataka washtakiwa hao kutojibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba10,2023 kwa ajili ya kutajwa.