Aliyemfumua nyuzi mgonjwa apewa siku 14 kujitetea

Aliyemfumua nyuzi mgonjwa apewa siku 14 kujitetea

Muktasari:

  • Baraza la Madaktari Tanganyika limemwandikia notisi ya uchunguzi wa awali na kutoa siku 14 kwa tabibu wa kituo cha afya Kerenge kilichopo Korogwe, Jackson Meli kuwasilisha kwa maandishi utetezi wake.

  

Dar es Salaam. Baraza la Madaktari Tanganyika limemwandikia notisi ya uchunguzi wa awali na kutoa siku 14 kwa tabibu wa kituo cha afya Kerenge kilichopo Korogwe, Jackson Meli kuwasilisha kwa maandishi utetezi wake.

Kabla ya baraza hilo, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) lilianza kumwajibisha Meli kwa kumsimamisha kazi hapo Septemba 4 baada ya kumfumua nyuzi mgonjwa wa ajali aliyekosa fedha za kuchangia huduma.

Taarifa iliyotolewa leo, Septemba 8 na Msajili wa Baraza la Madaktari Tanganyika, Dk David Mnzava imesema hatua hiyo imezingatia kanuni za uendeshaji wa mashauri  ya udaktari, udaktari wa meno na afya shirikishi.


Amesema baraza limepokea kwa masikitiko shauri hilo la uvunjifu wa maadili ya kitaaluma na limethibitishiwa na ofisi ya mganga mkuu wa mkoa.

“Baraza linaendelea na hatua za kimaadili kwa mujibu wa sheria ya udaktari, udaktari wa meno na afya shirikishi baada ya mtuhumiwa kukutwa na hatia,” amesema Dk Mnzava.


Msajili huyo amesema baraza linasisitiza wanataaluma wote kuzingatia kanuni za maadili ya utendaji wakati wote wanapotekeleza wajibu wao.

Aidha baraza limehimiza wanataaluma na wakuu wa vituo vya kutolea huduma za afya kuwasilisha taarifa za wagonjwa wasio na uwezo wa kuchangia matibabu kwa maofisa ustawi wa jamii katika vituo na maeneo husika kwa ajili ya ushauri wa kitaalamu kuhusu huduma za msamaha.

Tukio Mlei kumfumua nyuzi mgonjwa lilitokea Julai katika Kituo cha Afya Kerenge kilichopo Tarafa ya Magoma wilayani  Korogwe huko Tanga na video inayomwonyesha akifanya hivyo kusambaa mitandaoni.