Aliyepotea kiutata akutwa amelazwa MOI

Muktasari:
- Shilla ambaye ni kazi wa Goba Mpakani Dar es salaam na mtaalamu wa Tehama katika hoteli ya Johari Rotana, alitangazwa kuwa amepotea na alikuwa akitafutwa na ndugu na jamaa zake tangu Oktoba 15, 2023.
Dar es Salaam. Kufuatia taarifa za kupotea kwa Reuben Emmanuel Shilla (33) zilizosambaa katika mitandao ya jamii ziku mbili zilizopita, mtu huyo amekutwa akiwa amelazwa Taasisi ya Mifupa (MOI) baada ya kupata ajali kwa kugongwa na gari.
Shilla ambaye ni kazi wa Goba Mpakani Dar es salaam na mtaalamu wa Tehama katika hoteli ya Johari Rotana, alitangazwa kuwa amepotea na alikuwa akitafutwa na ndugu na jamaa zake.
Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 18, Mkuu wa idara ya ulinzi katika hoteli ya Johari Rotana, Theodory Stanley amesema Shilla hakuonekana kazini tangu Jumapili Oktoba 15, alipoondoka kazini.
Amesema siku hiyo alimpigia simu kujua kama ataingia kazini na alisema yuko njiani, laakini baada ya muda alipotafutwa tena akawa hapatikani.
Amesema siku iliyofuata Jumatatu asubuhi mke wake alipiga simu akimuulizia mume wake kwa kuwa hakurudi nyumbani na wao ndio walipoanza kukapata wasiwasi.
“Tulijaribu kumtafuta kwenye simu lakini hatukumpata, tulimjulisha mke wake hata huku hayupo tukaanza kuwatafuta ndugu zake ili kuweza kuungana na kumtafuta.
“Tulimpata kaka yake na alipokuja tukashauriana ikabidi kwenda kutoa taarifa kituio cha polisi Goba, baada ya hapo tukaanza kunzunguka vituo vya hospitali na vituo vya polisi,” amesema.
Pamoja na jitihada hizo Stanley amesema siku ya Jumatatu hawakufanikiwa siku ya Jumanne wafanyakazi mbalimbali waligawanyika na kwenda hospitali mbalimbali na kwenye vituo hadi jioni pia hawakufanikiwa.
“Tuliwasiliana na vyombo mbalimbali vya habari na kusambaza taarifa kwenye mitandao ya kijamii, ilipofika saa moja usiku daktari mmoja wa taasisi ya Mifupa (MOI) alipiga simu akieleza kuwa kuna mtu tunamwona kwenye picha tulimpokea Jumapili usiku aliletwa kutoka Kimara hospitali naona kama ni yeye.
“Tulimuagiza Meneja Rasilimali watu kwenda kuimuangalia alipofika alituthibitisha kuwa ni yeye lakini pia nilipiigiwa simu na mtu ambaye walikuwa pamoja wakati anapa ajali na giri liendalo hadraka,” amesema.
Kwa mujibu wa Stanley mtu huyo ambaye hakumtaja jina alimueleza kuwa wakati anapata ajali walikuwa pamoja eneo la Kimara na aligonga na kioo cha gari hilo na kupoteza fahamu.
Shuhuda huyo pia alimueleza kuwa walipelekwa wote Hospitali ya Kimara lakini yeye baada ya masaa manne alitibiwa na kuruhusiwa ila hajui nini kilichoendelea nyuma.
“Leo tumeenda kumtembelea bado hana fahamu hata hospitali tulipoenda kumtembelea na hajui alipo, hajui kilichotokea hivyo anaendelea na matibabu Moi,” amesema.
Kuhusu taharuki Stanley amesema kama ofisi walipata taharuki, wakawa wanafanya ufuatiliaji taratibu lakini, walipoona siku zinazidi kwenda bila mafanikio ndipo waliposhauriana kuweka wazi tukio hilo.
Meneja Mawasiliano MOI, Patrick Mvungi, amethibitisha kupokelewa kwa mgonjwa huyo, huku akieleza kuwa kutokana na changamoto aliyopata haruhusi kuzungumza.
Alipotafutwa kaka wa Shilla, hakuwa tayari kuzungumza badala yake alijibu kwa ujumbe mfupi wa maneno kuwa anamuhudumia mgonjwa.