Aliyeshtakiwa kwa kula, kulala Hoteli ya Serena bila kulipa afutiwa kesi

Muktasari:

  • Mahakama yaeleza kesi iliyofunguliwa haina ushahidi wa moja kwa moja wa kijinai

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Kariakoo imemfutia kesi na kumwachia huru mfanyabiashara aliyeshtakiwa kwa kujipatia huduma ya chakula na malazi katika Hoteli ya Serena kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa Denis Mfumbulwa (44) alidaiwa kujipatia huduma hizo zenye thamani ya Sh21.4 milioni bila kulipa, akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Mfumbulwa amefutiwa kesi Mahakama ikieleza shauri hilo si la jinai bali la madai.

Mfanyabiashara huyo mkazi wa Goba Kulangwa amefutiwa kesi leo Mei 15, 2024 na Hakimu Gladness Njau, shauri lilipoitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa baada ya upelelezi kukamilika.

Hakimu Njau amesema kesi hiyo si ya jinai bali ya madai kwa sababu haina ushahidi wa moja kwa moja wa kijinai.

"Kesi hii haina ushahidi wa kijinai, kwa sababu hiyo Mahakama inamuachia huru mshtakiwa. Hatuwezi kuendelea na usikilizwaji wa shauri hili kwa sababu lina sifa zote za madai, hivyo mlalamikaji kama utaona inafaa na upate haki yako, fungua kesi nyingine ya madai," amesema Hakimu Njau.


Ilivyokuwa awali

Kabla ya kuachiwa na Mahakama, mshtakiwa alikiri shtaka.

"Nakiri kutenda kosa hilo na niko tayari kumlipa mlalamikaji, hivyo naomba nafasi nizungumze naye," alidai mshtakiwa.

Mfumbulwa baada ya kueleza hayo, Hakimu Njau aliwapa nafasi mlalamikaji katika kesi hiyo, Desdery Dotto na mshtakiwa kuzungumza nje ya mahakama kwa muda.

Mahakama wakati ikitoa nafasi kwa mshtakiwa kuzungumza na mlalamikaji, pia nayo ilitumia nafasi hiyo kupitia kesi hiyo kwa undani.

Hakimu Njau aliyeahirisha kesi hiyo kwa muda kutoa nafasi ya majadiliano, waliporejea amesema amelipitia jalada la kesi hiyo na amejiridhisha kuwa si ya jinai bali ni madai.


Nje ya Mahakama

Baada ya uamuzi wa Mahakama, Dotto ambaye ni Meneja Mahusiano kwa Wateja, alidai yupo tayari kuendelea na kesi, hivyo anasubiri nakala ya hukumu ili afungue nyingine.

"Nitaenda kufungua shauri la madai ili nipate haki yangu, hapa nasubiri nakala za hukumu ili niendelee," amedai Dotto.

Kwa mara ya kwanza mshtakwia alifikishwa mahakamni hapo Mei 13, 2024 akikabiliwa na shtaka la kujipatia huduma kwa njia ha udanganyifu.

Alidaiwa Machi 6, 2022 hadi Machi 28, 2024 kwa nyakati tofauti katika Hoteli ya Serena iliyopo Mtaa wa Ohio, Wilaya ya Ilala, alijipatia huduma ya malazi na chakula yenye thamani ya Sh21.491 milioni bila kulipa.

Inadaiwa mshtakiwa baada ya kutumia huduma hizo, alitoweka kusikojulikana.

Karani wa mahakama, Bahati alidai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, huku akijua kitendo hicho ni kinyume cha sheria.