Aliyetoka jela kwa kesi ya kuua, atuhumiwa kuua tena mkewe

Baadhi ya waombolezaji wakiwa nyumbani kwa mama wa marehemu, Mariam Bulacha (42) anayedaiwa kuuawa na mume wake kwa kuchomwa visu mwilini. Picha na Daniel Makaka

Muktasari:

  • Jackson Kalamji (49) anayetuhumiwa kumuua mkewe, Mariam Bulacha (42), alitoka jela kwa msamaha wa Rais mwaka 2019, baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Mwanza. Polisi mkoani Mwanza wanamshikilia Jackson Kalamji (49) kwa tuhuma za kumuua mke wake, Mariam Bulacha (42) kwa kumchoma visu sehemu mbalimbali za mwili.

Kalamji ameingia kwenye sakata hilo ikiwa imepita miaka 19 tangu alipohukumiwa kwenda jela miaka 15 kwa kosa la kuua bila kukusudia, lakini aliachiliwa kwa msamaha wa hayati Rais John Magufuli mwaka 2019.

Aprili 15, 2024 Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alithibitisha jeshi hilo kumshikilia Kalamji, akisema tukio hilo limelotokea Aprili 13, 2024 kutokana na wivu wa mapenzi.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamanyili, Dominiko Kashonele amesema ugomvi wa wenza hao ulianzia kilabuni walipokuwa wanakunywa pombe, ambapo kila mmoja alimtuhumu mwenzake kuwa na uhusiano nje ya ndoa.

 “Mke na mume walikuwa wanakunywa pombe na ndipo ikaelezwa kuwa, mume alikuwa uhusiano na mwanamke wa pale walipokuwa wanakunywa. Wakati huo mume huyo naye akatuhumu mkewe kuwa na bwana mwingine, ndipo ugomvi ukaanzia pale.”

“Wakaambiwa na watu waliokuwa eneo hilo waondoke waende nyumbani, wakaondoka,” amesema.

Kashonele amesema walipofika nyumbani ugomvi uliendelea na ndipo mume alimchoma mkewe kisu.

“Mariam alipata upenyo wa kukimbilia nje kuomba msaada majirani lakini alianguka chini na mume alifika na kuendelea kumchoma kisu hicho maeneo mbalimbali ya mwili, kisha akajisalimisha kituo cha Polisi cha Kata ya Nyakalilo,” amesema.

Amesema wananchi waliwapigia simu na kuwataka kwenda kuangalia kilichotokea.

“Tukaenda kweli tukamkuta yule mama ameanguka chini anavuja damu basi sasa ndio tukaanza kufanya mawasiliano,” amesema.

Naye kaka wa marehemu, Manyala Kibiti aliyekuwepo siku ya tukio, amesema walipofika nyumbani kwa dada yake alimkuta amelala nje ya nyumba.

“Nilipoingia ndani ya nyumba nikakuta damu nyingi zaidi, nikadhani labda aliuawa ndani, halafu baadaye akawekwa nje, lakini inaonekana alikuwa amejikongoja kutoka nje,” amesema.

Kesi ya kwanza

Mwananchi Digital imefika katika Kijiji cha Mwamanyili wilayani Sengerema ilipo familia ya Jackson na marehemu Mariam, ambako ndugu wanasema Jackson alishatumikia kifungo kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Kaka wa mtuhumiwa, Ndalahwa Kalamuji amesema mwaka 2005 mdogo wake alikutwa na hatia ya kuua bila kukusudia akiwa na rafiki yake, Yohana Ntonelwa ambapo wote wawili walihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.

Ndalahwa amesema mdogo wake akiwa na rafiki yake huyo walimuua bibi wa mke wa Yohana katika Kijiji cha Buswelu Kata ya Nyanzande baada ya mke wake kurudi kwa bibi yake kutokana na tofauti zao kwenye ndoa.

 “Siku kadhaa wawili hao walifunga safari kwenda kijiji cha Buswelu Kata ya Nyenzenda kama kusalimia na kurudisha upendo kwa mke wa Yohana Ntonelwa ili arudi nyumbani, lakini waligonga mwamba, ndipo walipochukua jukumu la kumshambulia bibi huyo hadi kupoteza maisha na mke wa Yohana alijeruhiwa kwa kukatwa mkono.

Amesema, wawili hao walipofikishwa mahakamani walikutwa na hatia ya kuua bila kukusudia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kila mmoja.

“Walianzia Gereza la Kasungamile na baadaye kuhamishiwa Gereza kuu la Butimba yote yapo Mwanza lakini, walitolewa kwa msamaha wa Rais wa awamu ya tano (John Magufuli) wakiwa wamebakiza miezi mitatu kumaliza kifungo chao,” amesema.


Baada ya kutoka jela

Baada ya kutoka jela, mwaka 2020 alimuoa Mariam ambaye hadi umauti unamkuta hakubahatika kuzaa mtoto na mtuhumiwa, ingawa alikuwa na watoto saba aliozaa na mwanaume mwingine.

Kaka wa mtuhumiwa ameendelea kusimulia kuwa, baada ya ndugu yao kutoka jela maisha ya wanafamilia yalikuwa mashakani kwa kuwa alikuwa na vurugu na wakati mwingine kuwatishia kuwaua.

 “Sisi kama familia tunaomba vyombo vya dola visimwachie tena kutokana na vitendo vyake visivyofaa kwenye jamii waendelee kuwa naye ili wananchi waishi kwa amani,” amesema Ndalahwa.

Magdalena Clement, ambaye ni shemeji wa mtuhumiwa amesema kuna kipindi walikosa amani, kutokana na vitisho vya kuuawa vilivyokuwa vinatolewa na Jackson kwa baadhi ya wanakijiji na hata wanafamilia.

“Ilifika hatua alikuwa ananiambia kuwa kuishi uraiani ni shida sana, nimekonda natamani kurudi jela ili nikashike wadhifa wangu wa mnyampala,” amesema Magdalena.

Naye mama mzazi wa marehemu Mariamu, Chausi Mashamba amesema tukio la mwanaye kuuawa limesitisha familia yake akiomba vyombo vya dola kuchukua hatua stahiki.

“Mwanangu tumeshamzika, alikuwa msaada kwangu sasa hayupo ameuawa kinyama inauma na inasikitisha,” amesema Mashamba.

 Idadi ya wafungwa wanaorudia makosa baada ya kutoka jela yaongezeka

Kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi wa ufanisi wa utekelezaji wa programu za urekebu kwa wafungwa ya mwaka 2022/2023 iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere idadi ya wafungwa wanaorudia makosa baada ya kutoka gerezani imeongezeka kwa asilimia 1.5 kwa kipindi cha kati ya mwaka 2019 hadi 2023.

Ripoti hiyo ilibaini licha ya programu urekebu kutekelezwa, bado idadi ya wafungwa waliokuwa wanarudia makosa waliongezeka, ikitaja mwaka 2019 wafungwa 3,239  walirudia makosa huku, mwaka 2020 idadi hiyo iliongezeka kufikia 3,384.

Ilipofika mwaka 2021 idadi ya wafungwa waliorudia makosa ilishuka hadi 3,235 na kuongezeka tena kufikia 4,013 mwaka 2022 na mwaka 2023 idadi hiyo ilikuwa 3,262.

 “Ongezeko la wafungwa wanaorudia makosa kunathibitisha kuwa kuna ongezeko la wafungwa waliotoka gerezani lakini wanaendelea kurudia kufanya makosa yaleyale. Aidha, ukaguzi ulibaini kuwa kiwango cha wafungwa waliokuwa wanarudia kufanya makosa yaleyale baada ya kuachiwa huru ni wale waliofungwa vifungo vifupi,”imesema ripoti hiyo na kuongeza,

“Kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, asilimia 59.22 ya wafungwa waliorudia makosa yao walikuwa na kifungo chini ya mwaka mmoja, asilimia 24.65 walikuwa na kifungo cha miaka mmoja hadi mitatu, asilimia 10.1 walikuwa na kifungo cha miaka mitatu hadi mitano.

"Asilimia 3.09 walikuwa na kifungo kati ya miaka mitano hadi 10, asilimia 0.37 walikuwa na kifungo cha miaka 10-15, asilimia 2.22 walikuwa na kifungo cha miaka 15-20, asilimia 0.32 walikuwa na kifungo cha miaka 20-30 na asilimia 0.01 walikuwa na kifungo zaidi ya miaka 30,”