Baba aua mtoto wa kambo, amzika kwenye shimo la takataka

Muktasari:

  • Alimdanganya mkewe mtoto ameenda shuleni baada ya kubanwa aliwaongoza polisi hadi alipomzika.

Songea. Ni mauaji ya kikatili, ndivyo unavyoweza kuelezea kitendo cha mkazi wa eneo la Peramiho katika Manispaa ya Songea, Richard Mgina, kumuua mtoto wake wa kambo aliyekuwa akisoma shule ya chekechea na kuzika mwili wake kwenye shimo la takataka.

 Kutokana na mauaji hayo, Jaji James Karayemaha wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Songea amemhukumu Mgina aliyemdanganya mkewe kuwa mtoto alikuwa ameenda shule kumbe alishamuua, kunyongwa hadi kufa kwa kosa lake hilo.

Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 5, 2024 na nakala yake kupatikana leo katika mtandao wa Mahakama ambapo Jaji alisema kwa kuzingatia ushahidi kwa ujumla wake, ameshawishika hakuna mtu mwingine aliyemuua Paul Haule isipokuwa Richard Mgina.

Awali, mama wa marehemu alikuwa ameolewa na shahidi wa sita wa Jamhuri, Bathromeo Haule na kupata naye watoto wawili ambao ni Paul na Sarah Haule, lakini waliachana na kuolewa na mshtakiwa ambaye naye walifanikiwa kupata mtoto mmoja, Chine Mgina.

Siku ya tukio Februari 21, 2021, shahidi wa pili ambaye ni mama wa marehemu, alieleza alimwandaa mwanaye huyo na akamruhusu kwenda shule ya chekechea iliyopo shule ya msingi Kilimani, naye akaenda Hospitali ya Peramiho ambako ndipo anafanya kazi.

Baadaye kwenye saa 3:00 asubuhi, alijulishwa kuwa mwanaye Sara alikuwa mgonjwa sana na baada ya kupata ruhusa alikwenda nyumbani kumchukua na kumwahisha hospitali ya Peramiho akisindikizwa na mumewe ambaye ni mshtakiwa.

Mtoto wao huyo alilazwa wodi namba 8 ambayo ni ya wagonjwa wa dharura, lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya ambapo alihamishiwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) ambapo mama yake alilazimika kulala na mwanaye wodini.

Baba mzazi wa Sara ambaye ni shahidi wa sita, Bathromeo Haul alijulishwa juu ya kulazwa kwa mwanaye huyo na Jumatano ya Februari 22, 2023 saa 12:00 jioni alikwenda hospitalini kusaidiana na mzazi mwenzake kumuuguza mtoto wao huyo.

Kwa kuwa tayari baba wa marehemu alikuwa hospitali, Februari 23,2023 mkewe huyo wa zamani akaamua kwenda nyumbani kuijulia hali familia yake, lakini alipofika nyumbani hapo saa 12:00 asubuhi, alishangaa mlango ukiwa umefungwa.

Kulingana na ushahidi wa upande wa mashtaka, mama huyo alijitahidi kumuita Paul Haul (marehemu), lakini hakuitikia wito huo na alipomuuliza mumewe (mshtakiwa) mtoto yuko wapi, alimjibu kuwa tayari alikuwa amekwenda shule.

Mke alivyomtilia shaka mumewe

Kwa vile ilikuwa ni asubuhi sana, mkewe alitilia shaka jibu la mumewe kwa kuwa ilikuwa ni mapema sana kwa mwanaye kwenda shule, kwani kwa kawaida huwa anakwenda saa 1:00 asubuhi.

Baada ya kumaliza alichokuwa anakifanya, mama huyo aliamua kurejea hospitali na kumweleza mzazi mwenzake juu ya mashaka aliyonayo na baadaye mshtakiwa alimtaarifu mkewe huyo kuwa Paul amepotea, hivyo mke akaamua kwenda shule kuulizia.

Shahidi huyo wa pili wa Jamhuri anaeleza kuwa baada ya kufika shule na kuulizia, alielezwa na mwalimu wa darasa, Leah Segesela ambaye ni shahidi wa nane wa Jamhuri kuwa mtoto wake alikuwa hajafika shuleni kwa siku mbili, yaani Februari 22 na 23,2023.

Kutokana na taarifa hiyo, mshtakiwa pamoja na watu wengine ambao ni shahidi wa tatu, Gervas Kayombo na shahidi wa sita, Bathromeo Haul ambaye ni baba mzazi walianza kumtafuta marehemu na pia wakamjulisha mwenyekiti wa kijiji, Raymond Mvulla.

Siri ya mauaji ilivyofichuka

Wakati wakiendelea kumtafuta marehemu bila mafanikio, taarifa za kupotea kwa mtoto huyo zilitolewa katika kituo cha Polisi Peramiho ambao walielekeza utafutaji uendelee na endapo itapita saa 24 warudi polisi, ndio mama akarudi polisi Februari 25,2023.

Pamoja na Polisi kuongeza nguvu ya kumtafuta, hakupatikana popote ambapo mama wa mtoto akawadokeza polisi kuwa ana mashaka mumewe ana mkono na kupotea kwa mwanaye, hapo polisi wakaamua kuwashikilia wote wawili mume kwa mahojiano.

Wakati akihojiwa katika mahojiano yasiyo rasmi (orally) na shahidi wa kwanza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Mohamed Ngonyani, mshtakiwa alikiri amemuua mtoto wao huyo na kumtupa katika kisima kilichopo kwa shahidi wa tatu, Kayombo.

Makachero wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na ASP Ngonyani walikwenda siku hiyo hiyo katika eneo hilo na huko walikuta watu wengi wakiwamo baadhi ya mashahidi katika kesi hiyo na kutafuta mzamiaji aliyeingia kisimani, lakini mwili wa mtoto haukupatikana.

ASP Ngonyani akawamuru makachero wake na yeye mwenyewe warudi kituoni na kumhoji mtuhumiwa huyo kwa kina kuhusu ni wapi alipouficha mwili wa marehemu baada ya kuukosa eneo la mwanzo alilolieleza yeye mwenyewe kwa hiyari yake.

Hapo ndipo mwanamume huyo akaanza kuwaeleza polisi kuwa alikuwa ameuzika mwili huo katika shimo la takataka jirani na nyumba yao, walimchukua na kwenda naye eneo la tukio ambapo mshtakiwa aliwaonyesha mahali alipomzika.

Shimo hilo lilifukuliwa na baada ya kufika chini kidogo walikutana na mfuko wa sandarusi (sulphate bag) ambao ndani yake kulikwa na mwili wa mtoto na baada ya uchunguzi ilithibitisha ni mwili wa Paul Haul na pia baba mzazi akautambua mwili huo.

Ripoti ya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huo, Tupokigwe Brown aliyekuwa shahidi wa tisa, ambayo ilipokelewa mahakamani kama kielelezo PE2 ilionyesha sababu za kifo ni kukosa hewa baada ya kukabwa, lakini kilichochangia zaidi ni majeraha kichwani.

Muuaji alivyojitetea kortini

Katika utetezi wake baada ya Mahakama kumuona ana kesi ya kujibu, mshtakiwa huyo alikanusha mashtaka dhidi yake na kwamba ameshukiwa tu kwa sababu ni baba mlezi.

Alijitetea mbele ya Jaji James Karayemaha, mshtakiwa huyo alidai asubuhi ya Februari 21,2023, marehemu alikweda shule, lakini hakurudi na kutokana na mazingira hayo, yeye alitoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji na majirani ambao walimsaidia kumtafuta.

Alisema Februari 25,2023 alikwenda Polisi Peramiho baada ya mtu aliyemtaja kuwa ni Elisha Mhagama kumjulisha kuwa mkewe alikuwa amekamatwa na Polisi na kwamba alipofika katika kituo hicho cha Polisi naye alikamatwa na kuwekwa mahabusu.

Alikanusha kuwahi kukiri kufanya mauaji hayo na kwamba mwili wa marehemu Paul (mtoto) ulipatikana baada ya mkewe  kukamatwa na sio kwa sababu ya kukamatwa kwake yeye na mwili wake ulipatikana akiwa njiani kwenda Polisi.

Hukumu ya Jaji Karayemaha

Katika hukumu yake, Jaji Karayemaha alisema hakuna ubishi kuwa ushahidi uko wazi kwamba marehemu alinyongwa hadi kufa na kabla ya kufikia hatua hiyo, alipigwa kichwani na kumpa majeraha kichwani na shingoni yaliyosababisha kifo chake pia.

Jaji alisema swali ambalo Mahakama ilitakuwa kulijibu ni kwamba ni nani hasa alimuua marehemu na kwamba ushahidi uliotolewa unamlenga mtu mmoja tu, naye ni mshtakiwa ingawa hakuna ushahidi wa kushuhudia akifanya mauaji hayo ya kikatili.

Kulingana na Jaji, shahidi wa pili ambaye ni mkewe aliieleza mahakama kuwa wakati mtoto wao anatangazwa kutoweka, alikuwa chini ya uangalizi wa mshtakiwa wakati yeye (mama wa marehemu) akiwa hospitali akimuuguza mtoto mwingine, Sarah Haule.

Shahidi huyo ndiye aliyemweleza kuwa mtoto amekwenda shule na tangu siku hiyo yaani Februari 23,2023 mtoto huyo hakuonekana tena hadi siku mbili baadaye wakati mshtakiwa alipowaongoza polisi hadi jirani na nyumba yake na mwili kupatikana.

Jaji alisema kwa kuwa ni mshtakiwa mwenyewe alijitolea kukiri na kueleza baada ya kumuua mtoto huyo alimzika katika shimo la taka jirani na nyumba yao, ninachukua uamuzi wa kijasiri kuwa ni kukiri kwake kuliwezesha mwili kupatikana.

Mbali na hilo, lakini Jaji akasema mshtakiwa ndiye mtu wa mwisho kuwa na marehemu kwa hiyo ni kanuni ya kisheria kuwa mtu wa mwisho kuonekana na mtu mwingine akiwa hai na baadaye mtu huyo akaonekana ameuawa, yeye atahusika na mashtaka hayo.

Ni kutokana na ushahidi huo, Jaji alisema anamtia hatiani mshtakiwa kwa kosa hilo la mauaji ya kukusudia na kumhukumu kunyongwa hadi kufa. Pamoja na kunyongwa huko, bado kitendawili kinabakia vichwani mwa watu, nini kiini cha kufanya mauaji hayo?