Aliyeua mtoto kulipiza kisasi ahukumiwa kunyongwa

File Photo

Njombe. Mahakama Kuu iliyoketi Njombe, imemhukumu adhabu ya kifo, Happiness Mkolwe baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua mtoto Jackson Kiungo, ikiwa ni kulipa kisasi kwa mama yake kuwa na uhusiano wa kimapenzi na na mumewe.

Inaelezwa kuwa Happiness, alimteka nyara mtoto huyo wakati akitokea saluni kunyoa nywele na baadae kumuua kwa kumziba pua na mdomo na alipofariki alikwenda kumchimbia shimo na kumzika.

Hukumu hiyo ilitolewa Ijumaa ya Desemba Mosi, 2023 na Jaji James Karayemaha wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea na nakala yake kupatikana katika mtandao wa mahakama jana baada ya kusikiliza mashahidi wanane na kupokea vielelezo vinane.

Miongoni mwa vielelezo vilivyopokelewa ni maelezo ya onyo aliyoyaandika Hapinness alipokuwa polisi na aliyoyaandika kwa mlinzi wa amani, ambako kote alikiri kufanya mauaji hayo na kuelezea namna alivyomuua Jackson.

Tukio hilo lilitokea Septemba 6, 2022 katika mtaa wa Mliwati, Kata ya Ihunga katika Wilaya ya Njombe mkoani Njombe na mwili wa marehemu ulipatikana siku mbili baadae baada ya wananchi kijijini hapo kuunganisha nguvu kumtafuta.

Jaji alisema ushahidi wa upande wa mashtaka unaonyesha marehemu ni mwathirika wa uhasama kati ya mshtakiwa na Happy Mwenda wakigombea mwanaume na mshtakiwa aliamua kumuua mtoto huyo ili kulipiza kisasi.

Baada ya kumuua, alirudi na nguo za marehemu nyumbani na kuzichoma moto.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji James Karayemaha alisema maelezo ya ungamo ya mshtakiwa na ushahidi wa mashahidi wanne unaleta muunganiko na maelezo ya mshtakiwa yanaeleza kila kitu hatua kwa hatua nini alikifanya hadi kumuua.

“Ninashawishika kuwa kutokana na ushahidi kwa ujumla wake uliotolewa mahakamani hauachi mashaka kwamba ni mshtakiwa na sio mtu mwingine aliyefanya kosa (la mauaji ya kukusudia) ambalo ameshitakiwa nalo,”alisema Jaji.

Jaji alisema kwa kutuliza akili yake na kwa kuzingatia maelezo yake mwenyewe ya ungamo inanifanya nifikie hitimisho lisilozuilika kuwa uwepo wa nia ovu umethibitishwa kama kifungu cha 200 cha kanuni ya adhabu kinavyotaka.

Kutokana na uzito wa ushahidi uliotolewa mahakamani uliomtia hatiani, Jaji Karayemaha alisema adhabu kwa kosa hilo ni moja tu, nayo ni adhabu ya kifo hivyo naye atanyongwa hadi kufa kutokana na kosa alilolifanya.

Alivyokiri kuua na kumzika

Katika maelezo yake, Septemba 6,2022 akiwa amemsindikiza Judita Kihaka kunyoa, alimkuta mtoto Jackson akimaliziwa kunyolewa katika saluni ya Robert Muhema hivyo yeye akaamua kutoka nje ya saluni hiyo kwa lengo la kumsubiri.

“Alitoka nje baada ya kumaliza kunyolewa na nilimuita na kuanza kumuuliza kuwa mume wangu Rogatus Maleka huwa anaendaga nyumbani kwao akanijibu ndiyo huwa anakuja. Nikamuuliza mara ya mwisho ni lini akasema ni Jumapili 5.9.2022”

“Nilienda naye eneo la kisimani na nilimvua nguo zake, nilimbana shingo yake na mguu wangu wa kulia na kuchukua nguo zake zote na kumziba pua na mdomo hadi alipokufa” alisema

 kwa lengo la kumkosesha hewa ili afe. Niliendelea kumbana kwa mguu wangu wa kulia hadi nilipoona hahemi.”

“Nilipoona hapumui ndipo nilipojua amekufa, baada ya kuona tayari ameshakufa nilichukua mti na kuchimba juu ya mapumba ya kupasulia mbao na kumchukua na kumfukia kwenye shimo nililochimba. Nilimlaza kifudi fudi na kumfukia.”

“Niliondoka na kurudi nyumbani kwangu nikiwa na nguo za Jackson muda huo ilikuwa saa 3:14 usiku. Nilipikia watoto wangu chakula na nilienda kwa rafiki yangu Judita Eliuteli kupiga stori na nilikaa hadi saa 5 nikarudi nyumbani kulala.”

“Asubuhi tarehe 7.9.2022 nilirudi hadi mahali nilipomfukia Jackson niliona pako sawa jinsi nilivyokuwa nimepafukia usiku tarehe 6.9.2022” alieleza Happiness huku akisema alirudi tena eneo alipomfukia yule mtoto akachimba shimo ili amfukie upya.