Atuhumiwa kumuua mwanaye kwa kumzamisha kwenye ndoo ya maji

Mama aliyejulikana kwa jina la Johari (19) (mwenye Sweta) mkazi wa Mawelewele, Manispaa ya Iringa akiwa chini ya ulinzi baada ya kutiwa mbaroni kwa tuhuma za kumuua mwanaye kwa kumzamisha kwenye ndoo ya maji ya chooni. 

Muktasari:

  • Mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Johari Mbuma (19), mkazi wa Kigamboni Manispaa ya Iringa anashikiliwa na polisi akituhumiwa kumuua mtoto wake baada ya kumzamisha kwenye ndoo ya maji chooni.  

Iringa. Mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Johari Mbuma (19), mkazi wa Kigamboni Manispaa ya Iringa anashikiliwa na polisi akituhumiwa kumuua mtoto wake mwenye umri wa miezi saba kwa kumzamisha kwenye ndoo ya maji chooni kichwa chini miguu juu akiwa Mtaa wa Mawelewele.

Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 21, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amekubali kuwepo kwa tukio hilo, akisema uchunguzi unaendelea.

Video ambayo Mwananchi imeiona, inamwonyesha Johari akieleza tukio hilo baada ya kukamatwa na Polisi, akisema alitoka kwao na kwenda kwa rafiki yake na baadaye alipobanwa haja aliingia chooni ambako baada ya kumaliza, alimtumbukiza mtoto kwenye ndoo nyeupe iliyokuwa na maji.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mawelewele, Obedi Mtatifikolo amesema alipata taarifa Jumapili, Novemba 19, 2021 na alitoa taarifa polisi ambao walifika kuchukua mwili wa mtoto  huyo.

"Leo baadhi ya watu walimuona dada huyo na kutoa taarifa tena kwa mwenyekiti kuwa wamemuona aliyetupa mtoto, wakamleta na amekiri alufanya tukio hilo.

"Tulipo muhoji kwa nini alitekeleza tukio hilo alisema alikuwa anamazingira magumu," amesema Mtatifikilo.

Baadhi ya majirani wamesema walimuona Johari alipokuwa ameenda kwa rafiki yake, lakini kwa sababu hakuwepo, aliingia kwenye duka moja akanunua kofia ya mtoto baada ya hapo alienda chooni.

"Huko chooni ndio alimtumbukiza mtoto kwenye ndoo ya maji kichwa chini miguu juu," amesema mmoja wa majirani ambaye hakutaka jina lake liandikwe.

Tukio hilo limetokea ikiwa imepita siku chache baada ya baba wa mtoto kumuua mwanae kwa kumnyonga huku akimrekodi video, katika mtaa wa Mwangata, Manispaa ya Iringa.