Adaiwa kumuua baba mdogo akimtuhumu kuchepuka mama yake
Muktasari:
- Tukio hilo ambalo limezua taharuki katika kijiji cha Uswaa, limetokea Novemba 7, mwaka huu, katika kitongoji cha Mbweera kijijini hapo, ambapo kijana huyo anadaiwa kumuua baba yake mdogo, akimtuhumu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mama yake mzazi.
Hai. Erick Mwanga (19), mkazi wa Kijiji cha Uswaa, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kumuua baba yake mdogo kwa kumkata shingo na kitu kinachodhaniwa kuwa ni panga, akimtuhumu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mama yake mzazi.
Tukio hilo ambalo limezua taharuki katika eneo hilo, limetokea Novemba 7, mwaka huu, katika kitongoji cha Mbweera kijijini hapo, wakati marehemu akiendelea na shughuli zake za kukata mbao.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amir Mkalipa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa amekamatwa na uchunguzi unaendelea.
"Ni kweli tukio hilo limetokea, mtuhumiwa amekamatwa na uchunguzi unaendelea," amesema DC Mkalipa
Akizungumzia tukio hilo, jana Novemba 8, 2023, Mwenyekiti wa Kijiji cha Uswaa, Jacobo Swai amesema marehemu akiwa kwenye shughuli zake za kukata mbao, alifuatwa na kijana huyo ambaye ni mtoto wa ndugu yake na ndipo alipochukua panga na kumkata shingo, jambo linalodaiwa kusababisha kifo chake papo hapo.
Mwenyekiti huyo amemtaja aliyeuawa kuwa ni Isawafo Mwanga (47) na kwamba mtuhumiwa amekamatwa na polisi na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea kufanywa.
"Ni kweli kuna tukio la mauaji limetokea Jumanne kijijini kwetu Uswaa, nilipigiwa simu kupewa taarifa na nilipofika eneo la tukio, nikamkuta marehemu kakatwa shingo, Polisi walifika wakahoji baadhi ya majirani na aliyekuwa akifanya kazi na marehemu, kisha wakaondoka na mwili huo huku mtuhumiwa akikatwa nyumbani kwao," amesema Swai na kuongeza;
"Chanzo cha tukio hilo inadaiwa kuwa, mama wa kijana huyu aligombana na mume wake na kwenda kuishi na marehemu, sasa inaonekana kitendo hicho kilisababisha uchungu kwa mtuhumiwa na kusababisha kufanya hayo."
Omben Mwanga ambaye ni kaka wa marehemu, amesema tukio hilo limewaumiza kama familia na kuwaacha na majonzi makubwa kwa kuwa anayedaiwa kuhusika na mauaji hayo ni mtoto wa ndugu yao.
"Tukio hili linaumiza sana, kwani huyu kijana ni mtoto wa ndugu yetu, anamuita marehemu baba mdogo, maana huyu marehemu na baba wa huyo kijana ni ndugu, inasikitisha sana," ameeleza Mwanga.
Akielezea chanzo cha tukio hilo kaka wa marehemu amesema: "Inaonekana kulikuwa na shida, na inasemekana alishatamka atamuua akidai huyo mdogo wangu alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mama yake mzazi, sasa hilo linaonekana ndilo limesababisha haya."
"Mama yake aliachana na baba yake na kuondoka kwenda kuishi kitongoji kingine, na siku za karibuni kijana huyu alikuwa rafiki wa karibu na marehemu na hata hiyo jana inasemekana alimfuata huko kazini kwake na wakawa wanazungumza, yeye akiwa amekaa na marehemu akiendelea na kazi, sasa na inaonekana alitafuta kuwa nae karibu ili kutekeleza hilo".
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Uswaa, Emmanuel Karim amelaani tukio hilo na kuekeza kuwa si tukio la kawaida kwa kuwa limehusisha watu wa familia moja.
"Tukio hili limetupa shida kidogo hapa mtaani maana siyo tukio la kawaida...inaumiza sana, na kulikuwa na shida, maana huyu kijana baba yake na mama yake walikuwa hawaelewani, na ikawa inasemekana marehemu ana mahusiano ya kimapenzi na mama mzazi wa kijana huyo, ambapo amemhamisha nyumbani na kwenda kupangishia nyumba kijiji kingine sasa shida ndiyo ikaanzia hapo," amesema.
Ameongeza kuwa "...kujichukulia sheria mkononi ni jambo baya, na kwa ujumla yule ni mtu mzima mambo yale yalikuwa hayamuhusu, angevumilia aone mwisho itakuwaje, au angechukua hatua ya kibusara kuwaeleza wazee ili waweze kushughulikia hilo."
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Machame, Uroki, Roy Swai amesema tukio hilo linahusishwa na visasi, ambapo kijana Erick alikuwa akimtuhumu marehemu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mama yake.
"Tukio hili limekaa kifamilia na ukiliangalia limekaa kulipiza kisasi, maana inadaiwa mama wa huyu kijana mtuhumiwa aliondoka nyumbani na kwenda kuishi na marehemu, sasa inaonekana kitendo kile hakikumfurahisha huyu kijana, na hivyo kumuua mchepuko wa mama yake ambaye ni baba yake mdogo,"
"Na jana wakati marehemu akiendelea na shughuli zake, kijana huyu alifika na kukaa nae karibu, na kulikuwa na panga kali lililokuwa pembeni sasa wakati ameinama anaweka mchoro wa mbao, kijana huyo akamkata,” amesema.
Diwani huyo amesema kijana huyo amekamatwa na kwamba anashikiliwa na polisi wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.
Hata hivyo alipotafutwa kamanda wa polisi mkoani hapa, Simon Maigwa kuthibitisha tukio hilo alipigiwa simu mara kadhaa na hakupokea simu na wala kujibu chochote.