Prime
Bodaboda adaiwa kuuawa kwa risasi akidai Sh1,500
Musoma. Dereva wa bodaboda mkazi wa mtaa wa Makoko Manispaa ya Musoma, Morice Ally (30) amefariki dunia baada ya kupigwa risasi wakati akibishania chenji ya Sh1,500 kwenye kituo cha mafuta.
Dereva huyo na watu wengine wanadaiwa kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu katika kituo cha mafuta (jina limehifadhiwa) kilichopo barabara ya Majita Manispaa ya Musoma wakisubiri kujaziwa mafuta kwenye vyombo vyao vya usafiri.
Kwa mujibu wa mashuhuda bodaboda huyo alipigwa risasi tumboni na kusababisha utumbo kutoka nje kisha kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Nyerere kwa matibabu na baadaye alifariki dunia.
Katibu wa bodaboda Manispaa ya Musoma,Shukran Mtaki alisema tukio hilo lilitokea Septemba 1, 2023 saa 2.35 usiku katika kituo hicho.
Alisema Morice aliomba kuwekewa mafuta ya Sh3,500 kisha akatoa Sh5,000 na alipodai kurudishiwa chenji, ndipo muhudumu wa kituo hicho alidai kumuwekea mafuta ya Sh5,000.
"Alipoomba chenji yule muhudumu akadai ameweka mafuta ya hela yote wakaanza kuvutana na wakajikuta wanarushiana ngumi ndipo mlinzi wa kituo alipofika kwenye eneo hilo na kumvuta bodaboda wakatoka nje kidogo ya kituo," alidai Mtaki.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Iddi Malima alidai baada ya mlinzi kumtoa katika eneo hilo, alianza kumpiga makofi hali iliyosababisha vurugu ambazo baadae zilimfanya mlinzi huyo kufyatua risasi zilizompata marehemu na kumjeruhi.
"Baada ya mlinzi kumfyatulia risasi marehemu akawageukia watu waliokuwapo eneo hilo na kuwatishia huku akisema yeyote atakayemsogelea atamshughulikia. Mlinzi huyo aliwasiliana na polisi waliofika eneo la tukio haraka," alidai Malima.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Dismas Kisusi alipozungumza na Mwananchi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema jeshi hilo linawashikilia watu watatu kwa mahojiano zaidi.
Hata hivyo, Kisusi alisema chanzo cha ugomvi huo ni baada ya dereva bodaboda kukaidi agizo la kutoka kituoni hapo ili apishe watu wengine wapate huduma.
"Kulikuwa na foleni ndefu ya watu kwaajili ya kupata huduma pale na huyu bodaboda baada ya kujaziwa mafuta alibaki palepale akiwa anaongea na bodaboda mwenzake anayesemekana ni ndugu yake, sasa muhudumu akawaambia wapishe na bodaboda akakaidi wakaanza kuzozana hadi kupigana," alisema.
Alifafanua kuwa baada ya kutokea ugomvi, mlinzi wa kituo hicho Yusuph Gamba (65), alifika kwenye eneo la ugomvi na kumtoa bodaboda huyo hali ambayo pia ilisababisha kuzuka kwa ugomvi kati ya bodaboda na mlinzi huyo.
"Walipigana hadi nguo za mlinzi zikachanika ndipo mlinzi huyo akakimbilia silaha kwa mlinzi mwenzae na akampiga risasi mgongoni na kutokea tumboni na kusababisha utumbo kumwagika," alisema kamanda huyo.
Aliwataja watu wanaoshikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi ni Yusuph Gamba na mlinzi mwenzake, Majuto James na muhudumu wa kituo hicho, Joshua Majaliwa.
Alisema bodaboda huyo alifariki baada ya kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya rufaa ya Mwalimu Nyerere alikokimbizwa muda mfupi baada ya kupigwa risasi.
Baadhi ya bodaboda walisema foleni hiyo ilitokana na uhaba wa mafuta mjini Musoma hivyo kusababisha mafuta hayo kupatikana kwenye kituo kimoja pekee.
"Mjini hapakuwa na mafuta hivyo wengi wakawa wanakwenda kwenye kile kituo kupata mafuta sasa foleni ikawa ndefu sana mtu unaalazimika kusubiri kwa muda mrefu," alisema Musa William.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda hakupatikana kuzungumzia uhaba wa mafuta baada ya simu yake kuita bila kupokelewa huku Ofisa Biashara mkoa wa Mara, Gambaless Timotheo, alisema yeye sio msemaji.
Meneja wa Mamlaka ya Huduma za Nishati na Maji (Ewura) Kanda ya Ziwa, George Mhina, alipotafutwa kuzungumzia uhaba huo aliomba kupewa muda kwa yupo barabarani.