Anayedaiwa kuuawa kwa risasi na askari wa Kinapa azikwa
Octavian Temba, kijana aliyeuawa na waoadaiwa askari wa Kinapa na mgombo
Muktasari:
- Wakati vilio na simanzi vikitawala kwenye maziko ya kijana, Octavian Temba (38) anayedaiwa kuuawa kwa risasi na askari wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), baadhi ya waombolezaji wamesema wataunda kamati ya wazee kwenda kumwona Rais Samia Suluhu Hassan, kumpelekea malalamiko yao juu ya unyanyasaji wa raia wanaoishi kando mwa hifadhi za Taifa unaofanywa na baadhi ya askari wa hifadhi hizo.
Moshi. Wakati vilio na simanzi vikitawala kwenye maziko ya kijana, Octavian Temba (38), anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), baadhi ya waombolezaji wamesema wataunda kamati ya wazee ya kepeleka malalamiko kwa Rais Samia Suluhu Hassan, juu ya unyanyasaji wa raia wanaoishi pembezoni mwa hifadhi za Taifa unaofanywa na baadhi ya askari wa hifadhi.
Waombolezaji hao wameyasema hayo leo Jumanne wakati wa mjaziko ya Temba yaliyofanyika katika kijiji cha Komela, Kata ya Marangu Magharibi, Wilaya ya Moshi.
Temba anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi kichwani na askari wa Kinapa Mei 9, mwaka huu wakati akikata majani kando ya hifadhi hiyo ya Kinapa.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro tayari linawashikilia askari wawili na mgambo mmoja wa hifadhi hiyo kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Hata hivyo, mamia ya waombolezaji waliokuwepo kwenye ibada ya maziko iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Uomboni, wamesema matukio ya watu kupigwa risasi yamekuwa yakijirudia mara kwa mara.
Innocent Shirima amesema mauaji hayo hayapaswi kufumbiwa macho, Serikali inapaswa kuchukua hatua ili kuyakomesha.
"Damu ya kijana huyu aliyelala hapa haitaenda bure, kupigwa kwake risasi ya kichwa kisa kukata majani, haitaenda bure," amesema Shirima.
Naye George Kombe amesema binadamu wamegeuka wanyama wakali, hawaoni shida kuwaua binadamu wenzao bila huruma.
“Maadili yameporomoka kwenye jamii hadi kwenye majeshi yetu, kilichofanyika hiki hapa tunaomba mfanye 'reform' ya majeshi yetu, sidhani kama walichofundishwa ndio hiki wanachokifanya, nitoe pole kwa familia kwa haya yaliyotokea lakini damu hii iliyomwagika ikawe wino wa kurekebisha yale yote yaliyofanyika yasijirudie tena," amesema.
Akizungumzia msiba huo, Katibu wa Mbunge wa Vunjo, Gulatone Masiga amesema mauaji kama hayo sio mara ya kwanza kutokea, hivyo ameiomba Serikali iandae mpango kamambe wa kujenga na kurejesha mahusiano ya ujirani mwema yanayoonekana kulegalega hivi sasa.
"Eneo hili la hifadhi linazungukwa na vijiji 19, tunaomba mpango wa kujenga mahusiano ya ujirani mwema kati vijiji hivi, mahusiano yarejee kwa sababu hifadhi hizi za Taifa, zipo kwa manufaa ya wote, isiwe laana kama ambavyo inaenda kuonekana,” amesema Masiga.
Naye Diwani wa Vunjo, Filbert Shayo amesema isifikie hatua ikaonekana wanyama kama nyani, kima, tumbili wana thamani kuliko binadamu kutoka na mauaji yanayofanyika kila mara.
"Kwa sasa wananchi wanatasfri nyani, kima wamekuwa na thamani kuliko wao, niiombe serikali ijitahidi kusikia watu wanayosema maana vitu vimeumbwa kwa ajili ya mwanadamu, mwanadamu hajaumbwa kwa ajili ya mti au nyani," amesema diwani huyo.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Dismas Temba amesema mauaji yaliyofanyika kwa ndugu yao yamekatisha ndoto zake zote kwa sababu alikuwa bado kijana familia ilimuhitaji na Taifa pia.
"Ndugu yetu aliuawa kwa kupigwa risasi tarehe Mei 9 mwaka huu, muda wa saa tatu asubuhi wakati alipoenda kukata majani msituni, tunalaani kitendo hiki cha kikatili na cha kinyama alichofanyiwa, tunaomba vyombo husika vihakikishe haki yake inapatikana," amesema Temba.
Akihubiri wakati wa ibada ya mazishi, Paroko wa Parokia ya Uomboni, Padri Adelard Iman amesema kifo cha kijana huyo kinaumuumiza kila mmoja kwa namna kilivyotokea.
"Maisha ya hapa duniani ni mafupi na ni ya muda, suala hili la msiba ni jambo zito, ni gumu na halielezeki, kwa namna ambavyo kifo hiki kimetokea, inaumiza sana kama ilivyosemwa kauawa kwa kupigwa risasi, tunampa pole sana mke wake, watoto wake na wazazi wake na wale wote walioguswa na msiba huu," amesema paroko huyo.