Anusurika kifo akigombea Sh1,000

Anusurika kifo akigombea Sh1,000

Muktasari:

  • Mwita Buruna (30), mkazi wa kijiji cha Rung’abure Wilaya ya Serengeti amelazwa hospitalini baada ya kuchomwa kisu tumboni katika ugomvi wa kugombea Sh1,000.

Serengeti. Mwita Buruna (30), mkazi wa kijiji cha Rung’abure Wilaya ya Serengeti amelazwa hospitalini baada ya kuchomwa kisu tumboni katika ugomvi wa kugombea Sh1,000.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Januari 19, 2021 mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba polisi wanaendelea kumsaka Matiko Bisako (40) mkazi wa kijiji cha Nyamerama kwa tuhuma za kumjeruhi mwenzake.

Mganga Mkuu wa Hospitali teule ya Nyerere, Tanu Warioba amesema majeruhi huyo anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.

Akisimulia tukio hilo lililotokea Januari 15, 2021 mwenyekiti wa kijiji cha Rung’abure, Joseph Meng’anyi amesema ugomvi kati ya wawili hao ulitokana na kupotea kwa simu ya kiganjani ya Burana  wakati wakinywa pombe za kienyeji katika moja ya vilabu vinavyouza pombe za kienyeji kijijini hapo.

“Ugomvi huo ulitokea baada ya Buruna kugundua kupotea kwa Sh1,000 aliyoificha ndani ya mfuniko wa simu ndipo akamtaka Bisako kumrejeshea fedha yake bila mafanikio,” amesema Meng’anyi

Kutokana na Bisako kugoma kumrejeshea fedha yake, Burana aliamua kuchomoa kadi ya miziki aliyokuwa anatumia Bisako kupigia muziki na hivyo kuibua malalamiko kutoka kwa wateja kutokana na burudani kukatika.

“Baada ya mzozo wa muda mrefu, Bisako alirejesha Sh1,000 aliyoichomoa kutoka kwenye mfuniko wa simu ya Burana huku wawili hao wakianza kutoleana maneno makali kabla ya kusukumana nje walikoendelea na ugomvi,” amesema Meng’anyi

Amebainisha kuwa katika ugomvi huo, Burana alichomoa kisu kidogo alichokuwa nacho bila kujua mwenzake alikuwa na kisu kikubwa zaidi ambacho alikitumia kumjeruhi na kutokomea kusikojulikana hadi sasa.