Asasi zakumbushwa kufanyia utafiti vitendo vya ukatili
Moshi. Taasisi zinazopinga vitendo vya kikatili ikiwamo ubakaji na ulawiti mkoani Kilimanjaro zimeshauriwa kufanya utafiti wa kina kufahamu kinachosababisha ongezeko la vitendo hivyo ili kuvidhibiti.
Ushauri huo umetolewa leo Julai 24, 2023 wakati mwenendo wa matukio ya vitendo hivyo yakiripotiwa kwenye vyombo vya habari yakionekana kuongezeka badala ya kupungua.
Katibu wa baraza la wazee mkoani Kilimanjaro, Godson Mshana ambaye ni mjumbe wa Smaujata amesema kwenye kikao cha taasisi hizo kujadili maendeleo na ukatili, kilichofanyika manispaa ya Moshi, kwamba bila utafiti, kazi ya ukatili itakuwa ni safari ndefu
“Ni kweli bila kufanya utafiti wa kina na kujua nini kinafanya ukatili ongezeke, tukabaki kupiga kelele tuu na kukemea kazi hii ya kupinga ukatili itakuwa ngumu na hazitakuwa na mafanikio,” amesema Mshana.
Amesema tafiti inaleta majibu ambayo ni kamili, tukifanya kama wanachofanya wanasayansi na kupata majibu, kazi ya kupinga ukatili itakuwa rahisi.
“Sasa tukifanya tafiti tukajua kwamba ukatili unatoka hapa, tunapojua unatokea sehemu fulani hapo unapotokea ndipo tunapodili napo, mfano ukijua ukatili unafanywa na huyo hapa, huyo ndiye tutadili naye,” amesema.
Mwenyekiti wa Smaujata mkoa wa Kilimanjaro, Stanley Urasa amesema lengo la kikao hicho ni kupata mrejesho wa wajumbe waliokwenda katika Siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika mkoani Dodoma hivi karibuni.
Pia, amesema mpango kazi wa mwaka huu kwa mkoa na wilaya wa kuendelea na mapambano dhidi ya ukatili bila kusahau kuweka vitega uchumi ili kufanya kazi kwa ufanisi.