Ashikiliwa mauaji ya mhitimu SUA
Muktasari:
- Jeshi la Polisi linamshikilia mwanamume mmoja kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mhitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kozi ya sayansi ya mazingira, Magreth Mashuwe (22) ambaye mwili wake uliokotwa kwenye mashamba ya chuo hicho.
Morogoro. Jeshi la Polisi linamshikilia mwanamume mmoja kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mhitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kozi ya sayansi ya mazingira, Magreth Mashuwe (22) ambaye mwili wake uliokotwa kwenye mashamba ya chuo hicho.
Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Ralph Meela alisema jana kuwa wanamshikilia mwanamume huyo ambaye naye ni mhitimu wa SUA kozi ya misitu kutokana na uhusiano wa kimapenzi na marehemu ambaye katika siku za hivi karibuni walikuwa na hali ya kutoelewana.
Alisema baada ya kumhoji mtuhumiwa alidai kabla ya tukio hilo marehemu alimuaga kuwa anakwenda Kihonda kutafuta kazi aliyoahidiwa na tajiri mmoja ambaye hakumfahamu.
“Kutokana na hilo tuna mashaka na mtuhumiwa kwa sababu yeye kama mpenzi wake walikuwa wakiishi chumba kimoja kama mke na mume kwa nini hakupata wasiwasi baada ya kuona mpenzi wake hajarudi, mpaka tulipomkamata ndio anatueleza hayo?” alihoji Meela.
Alisema pamoja na mashaka hayo, zipo sababu nyingine zinazolifanya Jeshi la Polisi limshikilie, ikiwa ni pamoja na hali ya uhusiano wao siku chache zilizopita kabla ya mauaji hayo.
Mkuu huyo wa upelelezi alisema pamoja maelezo hayo, bado Polisi wanaendelea na uchunguzi na kwamba uchunguzi wa kidaktari ulibaini mhitimu huyo alivunjwa shingo.
Mwili wa mhitimu huyo uliokotwa Desemba 14 baada ya kuonekana na msamaria mwema ambaye baadaye alitoa taarifa polisi. Mwili wa marehemu huyo umeshakabidhiwa kwa wazazi wake kwa ajili ya mazishi.
Mkuu wa Chuo anasemaje?
Makamu mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda alikiri marehemu kuwa muhitimu wa chuo hicho na kamba uongozi na wanajamii wa Sua wamepokea kwa masikitiko makubwa mauaji hayo na kulaani vikali.
Hata hivyo, alitoa wito kwa wanafunzi kuacha tabia zinazoweza kuwaweka kwenye hatari badala yake waishi kama wanafunzi.
“Kwa sasa tunaliachia Jeshi la Polisi liendelee na uchunguzi zaidi na wao ndio wenye mamlaka ya kusema nini chanzo cha mauaji haya, kama kuna waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria. Kiukweli kama chuo tumehuzunika,” alisema Profesa Chibunda.
Aliwashauri wanafunzi waliohitimu kuendelea kuishi mikononi mwa wazazi huku wakiendelea kutafuta ajira, ili waepukane na hatari zinazoweza kuwapata kwa kukaa nje ya wazazi ambako si sehemu salama.