Asilimia 75 ya wanawake hupata matibabu ya saratani katika hatua za mwisho
Muktasari:
- Asilimia 75 ya wanawake wanaofika katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi wanakutwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huo.
Mtwara. Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imeweka kambi ya matibabu katika Hospitali ya kanda ya kusini kwa siku tano ili kuweza kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi na hivyo kuanza matibabu mapema kabla ugonjwa haujafika hatua za mwisho.
Akizungumza na Mwananchi leo ikiwa ni siku ya pili Meneja Huduma za Kinga kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dakta Maguha Stephan alisema kuwa wengi wao hushindwa kupata tiba na hivyo kusababisha kupoteza maisha.
Alisema kuwa saratani ya mlango wa kizazi inaongoza kuwa na wagonjwa wengi ambapo kwa takwimu za mwaka 2022 zaidi ya asilimia 44 waligundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, asilimia 75 ya wanawake wanaofika katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi wanakutwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huo.
Dkt. Maguha alisema kuwa saratani ya matiti inashika nafasi ya pili kwa kuwa na wagonjwa wengi ambapo kwa takwimu za mwaka 2022 asilimia 18 ya wanawake waligundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ya matiti.
“Hapa tunapima Saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya matiti na tezi dume, wananchi wanapimwa damu ambapo ndani ya dakika 10 mtu anakuwa amepata majibu yake. Hivyo niwaalike mfike ili muweze kupata tiba na kinga dhidi ya saratani” alisema Dr Maguha.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo Kanda ya Kusini Dakta Jasmine Hamisi, amesema kuwa ujio wa madaktari bingwa wa uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa saratani katika hospitali hiyo, ni fursa nzuri kwa wananchi wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kufika na kufanyiwa uchunguzi huo ambapo unafanyika bila malipo.
Nae Said Nguyu mkazi Ufukoni Mtwara amesema kuwa amefika katika hospitali hiyo kuweza kupata vipimo vya saratani ya tezi dume baada ya kusikia matangazo juu ya ujio wa watalaamu hao.
“Nimekuja kupata vipimo saratani ya tezi dume hii kwetu ni fursa kubwa tunashukuru sana tunaipongeza serikali huu ni mkakati maalum wakuwezesha wananchi kuwa na afya njema ni vizuri ukaijua hali yako”
Kwa upande wa Sophia Said mkazi wa Newala yeye amesema: “Nilisikia kuwa kuna matibabu ya saratani, hii wangu imekuwa ni neema tunajua serikali inataka tuwe na afya njema hii kwetu itatusaidia na tunashukuru kwa hatua zote. Ningejua mapema, nisingekuwa na uoga ambao wengi wetu ndio unaotusumbua maana hatuna elimu.”