Watu 700 wana TB Bukombe

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Dk Deograsia Mkapa akizungumza na Mwananchi ofisini kwake kuhusu magonjwa hatarishi kiuchumi na namna ya kujikinga nayo. Picha na Ernest Magashi

Muktasari:

Kati yao wanaume ni 459 na wanawake 241, chanzo kikitajwa ni kufanya kazi sehemu yenye vumbi kwa muda mrefu yakiwemo maeneo ya migodini.

Bukombe. Watu 700 Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamegundulika kuwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) kwa mwaka 2022.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake leo Jumamosi Mei 6, 2023, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dk Deograsia Mkapa amesema kati yao wanaume ni 459 na wanawake 241, akitaja chanzo ni kufanya kazi sehemu yenye vumbi muda wote yakiwemo maeneo ya migodini.

Dk Mkapa amesema kati ya watu hao, 72 walikuwa pia na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi akitaja kutochukua tahadhari nakuwa na wapenzi wengi  ni chanzo cha watu hao kuwa na VVU.

Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na magonjwa hayo ikiwemo ya utoaji elimu na chanjo za kinga kuanzia kwa watoto.

“Jamii kubwa ya watu wa Bukombe ni wakulima na wengine wanajishugulisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu, kufuatia hali hiyo tumekuwa na mikakati malumu ya kuwafikia watoto kwa ajili ya kuwapatia chanjo,” amesema Dk Mkapa

Amesema katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2023 wametoa chanjo ya bega kwa watoto 6, 858 baada ya kuzaliwa ili kuwakinga na TB huku watoto 3, 986 wakichanjwa chanjo ya DPP inayowakinga dhidi ya magonjwa zaidi ya matano ukiwemo ugonjwa wa homa ya ini, pepopunda, donda koo, kifadulo na tetenasi.

Dk Mkapa amesema pia watoto 3, 986 walichanjwa chanjo ya polio na wengine 3, 219 wakipewa chanjo ya surua.

“Wataalamu wa afya walienda mashuleni na kuwachanja chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi wasichana 5, 000 wenye miaka kuanzia 14  kuanzia Januari hadi Mei 5 mwaka huu,

“Kuna watoto ambao walikuwa hawajapata chanjo kabisa tangu wazaliwe. Walichanjwa watoto 225,”amesema Dk Mkapa

Amesema wakazi wa wilaya hiyo 3, 820 walichanja chanjo ya kuwakinga dhidi ya Uviko 19 kwa kipindi hicho, wanaume wakiwa 2, 669 na wanawake 215.

 Amesema wamekuwa wakikumbana na changamoto ya jamii kudhani chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi huwafanya wasichana kushindwa kushika ujauzito kwa sababu ya kuchanjwa wakiwa wadogo na kudai wanaendelea kuwa elimisha ili waondokane na dhana hiyo

Mkazi wa Kata ya Igulwa, Sada Ally ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuendelea kutoa chanjo kwa watoto akidai mwanaye aliugua surua lakini baada ya kupata chanjo ya ugonjwa huo anaendelea vizuri.