Wananchi Lindi wataka huduma za saratani ziwe karibu

Wananchi mkoani Lindi wakisubiri vipimo vya saratani katika zoezi lilofanyika Hospitali ya Mkoa sokoine jana Mei 5, 2023.

Muktasari:

  • Taasisi ya saratani ya Ocean Road inafanya kambi ya siku tatu mkoani Lindi kwa ajili kuwabaini wenye viashiria vya ugonjwa huo, ili kuwaanzishia matibabu.

Lindi. Wakati Taasisi ya saratani ya Ocean Road ikifanya kambi ya siku tatu mkoani Lindi kwa ajili ya kubaini watu wenye viashiria vya ugonjw ahuo, baadhi ya wananchi wameiomba kusogeza huduma ya upimaji saratani karibu na jamii ili waipate huduma hiyo kwa urahisi.

 Wameyasema hayo jana Mei 5 baada ya kupima saratani katika hospitali ya mkoa ya Sokoine mkoani humo.

"Tunaomba serikali kusogeza huduma hii karibu na jamii ili kutupunguzia gharama ya kwenda Dar es Salaam kwani maisha na uchumi wetu hauruhusu kufuata huduma hiyo,” amesema Porisiana Poresiana Makunguru mkazi wa sabasaba Lindi mjini.

Kwa upande wake Charles Makwinya mkazi wa Lindi mjini ameiomba hospitali ya Ocean Road kufanya upimaji wa saratani kuwa endelevu mikoani na wilayani mara kwa mara kwani  litasaidia kupunguza tatizo la saratani nchini.

"Mpango huu uwe endelevu utasaidia watu tulio mbali na hospitali Ocean Road kujitokeza kwa wingi kwenye hospitali zetu za mikoa na wilaya," amesema Makwinya

Naye Hawa Aratanga mkazi wa Mpilipili Lindi ameshukuru kwa huduma hiyo kuwafikia mkoani kwake.

"Tuna washukuru Ocean Road na serikali kutuletea huduma hii kwani fursa hii ambayo ni adimu haipatikani mara kwa mara kwenye Hospitali zetu za mikoani na wilayani hamesema," amesema.

Akiizungumzia huduma hiyo, meneja kitengo cha uchunguzi wa saratani na elimu kwa Umma wa Ocean Road, Dk Maguha Stephano amesema ni utaratibu wao wa kuendesha kampeni ya upimaji saratani mikoani ili kuwarahisishia wananchi wasio na uwezo wa kusafiri kwenda jiji Dar es salaam kufuata huduma hiyo.

Dk Maguha kwenye amesema wanatarajia kuwafikia watu 800 kwa kipindi cha siku tatu na watakaobainika watapewa rufaa na wenye dalili za awali watatibiwa na kupata ushauri.

Amezitaja sababu na visababishi vya saratani niunene kupita kiasi, kutokula matunda na mboga mboga, kunywa pombe na matumizi ya tumbuka na miozi hatarishi ya jua kwa watu wenye ulemavu.

"Njia za kuzuia tatizo la saratani ni kupunguza unene, kuepuka pombe matumizi ya tumbaku na kupata chanjo ya kuzuia virusi vinavyosababisha saratani mlango wa kizazi na ini," amesema Dk Maguha.