Maradhi yanayosumbua jamii, namna ya kuyakabili

Dar es Salaam. Wakati Tanzania leo ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya afya duniani, ikiwa na kaulimbiu ya ‘afya kwa wote’, wataalamu wa afya nchini wameyataja maradhi yanaoisumbua jamii na namna ya kukabiliana nayo.

 Akizungumza na Mwananchi, Dk Hussam Uddin wa Hospitali ya Aga Khan alitaja ugonjwa unaowasumbua zaidi wanaume ni uvimbe katika tezi dume ambao huchangia mkojo kutotoka kwa mtiririko sahihi.

Anasema ugonjwa huo huanza kuwakumba wanaume wanapofikisha miaka 40 na dalili zake hutofautiana baina ya watu.

“Ugonjwa huu husababisha mkojo kutoka kila wakati iwe usiku au mchana, mtu huanza kukosa uwezo wa kuzuia mkojo kwa muda mrefu na wakati mwingine hutoka bila mtu kuwa na uwezo wa kuzuia,” anasema.

Dk Uddin anasema mwanamume mwenye ugonjwa huo hufikia muda mkojo huzuiliwa ndani ya kibofu au kutoka bila mtu kuwa na uwezo wa kuzuia, huku ukiwa umeambatana na damu, maumivu wakati wa kukojoa na wakati mwingine athari hutokea kwenye figo kutokana na shinikizo.

Daktari huyo mtaalamu wa magonjwa ya wanaume anasema wanaume wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea ni muhimu kufanya uchunguzi wa tezi zao na wakiwa na changamoto hiyo hushauriwa njia sahihi ya matibabu kama ni dawa au upasuaji.

Shida nyingine kwa wanaume wengi anayoitaja Dk Uddin ni changamoto ya nguvu za kiume.

Anasema baadhi ya wanaume wanapitia changamoto ya kushindwa kusimamisha uume, kushindwa kusimamisha kwa muda mrefu na kufika kileleni mapema.

Matatizo mengi yanayohusisha mambo ya uzazi yanatokana na changamoto za kisaikolojia ya mtu, hivyo huhitajika kupata msaada wa unasihi kukabiliana na tatizo hilo.

“Matatizo mengine kwa wanaume yanaweza kuchangiwa na matumizi ya dawa, mabadiliko ya homoni au mifumo ya uzazi kupata shida kidogo,” anasema.

Pia anasema uraibu wa baadhi ya vitu unaweza kupunguza uimara wa mwanamume, akitaja ugonjwa wa kisukari kuwa nao ni tatizo linaloathiri wanaume kwenye ushiriki wa mapenzi.


Shida ipo hapa kwa wanawake

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Dk Miriam Gonja anasema saratani ya shingo ya kizazi ndio ugonjwa unaowaathiri zaidi wanawake.

Hiyo ni kutokana na wanawake kuficha magonjwa yanayowaathiri sehemu zao za siri, hivyo mpaka ugonjwa unaowashambulia kugundulika tayari umeshasababisha athari kwa kiwango kikubwa.

Dk Miriam, ambaye ni Mkuu wa Idara ya magonjwa hayo katika Hospitali ya Aga Khan anasema changamoto iliyopo ni wanawake kutofanya uchunguzi wa saratani hiyo, hali inayochangiwa na ukosefu wa elimu na hata wale wenye elimu wanashindwa kupata matibabu kutokana na ukata.


Magonjwa yanayoitesa jamii

Akizungumzia magonjwa yanayoitesa jamii kwa ujumla, Dk Rajab Mlaluko wa Hospitali ya Rufani ya mkoa wa Mbeya anasema kuna makundi mawili ya magonjwa.

“Kutokana na mfumo wa maisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndiyo yanaitesa jamii, hasa shinikizo la juu la damu, saratani, uzito kupitiliza, utapiamlo na magonjwa mengine, hivyo ili kila mtu awe na afya bora ni muhimu kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora.

“Unakuta mtu anaingia ofisini tangu asubuhi hajatoka, hafanyi mazoezi anakula na kulala, wengine wanatumia pombe na wanavuta sigara. Vitu hivi ni hatari, ni muhimu kuzingatia maelekezo ya wataalamu kukabiliana na matatizo haya,” anasema.

Akizungumzia magonjwa yasiyo ya kuambukiza, mtaalamu wa lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Husna Faraji anasema jamii ikiwa makini na lishe itaepuka matatizo na magonjwa mengi.

Anasema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2006 zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kila mwaka vifo milioni 41 hutokea kutokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote duniani.

Ili kuepuka magonjwa hayo, Husna anasema ni muhimu kuzingatia makundi yote ya vyakula katika sahani ambayo ni wanga, mizizi, mboga za majani, matunda na kundi la mafuta na sukari.

Akizungumzia tatizo la msongo wa mawazo, Dk Raymond Mgeni anasema linachangiwa na mrundikano wa mambo mtu anayokosa kuwa na utatuzi nayo.

Tatizo hili linatajwa kuwa ni kubwa kwenye jamii na watu wamekuwa wakifanya matukio ya kutisha, ikiwemo kujiua.

“Msongo wa mawazo ni kichocheo kikubwa kinachoweza kuathiri mtu katika kupungua kwa umakini na utulivu, kutawaliwa na hali ya kukata tamaa na upweke na kukosa usingizi,” anasema.

Pia Dk Mgeni anasema msongo wa mawazo humsababishia mtu kupunguza ufanisi wa kazi na kumchelewesha mtu kufanya mambo mbalimbali, ikiwemo kuoa.


...Ngono salama ni muhimu

Akizungumzia maambukizi ya virusi vya Ukimwi, Dk Hafidh Ameir wa Tume ya Kudhibiti Maambukizi ya Ukimwi (Tacaids) anasema ili jamii iishi salama ni muhimu watu wahakikishe wanaepuka ngono isiyo salama kwa kutumia kondomu wakati wote na kwa usahihi.

“Kwa wale ambao tayari wamepata maambukizi ya VVU ni muhimu wazingatie dawa, kwani zitawasaidia kuishi maisha salama kwa muda mrefu. Ujumbe wangu kwa wale ambao hawajapima ni muhimu wafahamu, ukiijua hali yako ya afya ni ishara ya ushindi,” anasema.

Kwa mujibu wa takwimu za viashiria vya afya na Malaria Tanzania (THIS), inaonyesha Mkoa wa Iringa una maambukizi kwa asilimia 11.3 na Njombe kwa asilimia 11.4.


Maambukizi ya UTI

Dk Daniel Magomele wa kituo cha afya Magrefa kilichopo Mabibo, Dar es Salaam anasema UTI huwapata wanawake wengi na mara nyingi wajawazito kutokana na mabadiliko ya homoni mwilini.

Anasema maambukizi ya ugonjwa huo hutokea wakati bakteria kutoka kwenye ngozi au puru (rektamu - sehemu ya utumbo mpana), kuingia kwenye urethra na kuambukiza njia ya mkojo.

“Maambukizi yanaweza kuathiri sehemu kadhaa za njia ya mkojo, aina ya kawaida ni maambukizi ya kibofu lakini maambukizi kwenye figo ni aina nyingine ya UTI ambayo haitokei mara nyingi, lakini ni mbaya zaidi kuliko maambukizi ya kibofu,” anasema.

Ili kuepuka ugonjwa huo, Dk Magomele anasema ni muhimu watu kunywa maji mengi ili apate haja ndogo mara kwa mara ambayo inasaidia kusafisha njia ya mkojo.

Kwa upande wake, Dk Elisha Francis, anasema ili kuzuia UTI ni muhimu mtu kukojoa mara anapohisi haja hiyo, akisisitiza usibane/kukaa na mkojo kwa muda mrefu.

Pia daktari huyo anasema, lishe bora (yenye matunda na mboga za majani) husaidia kuongeza kinga ya kupambana na maambukizi (bakteria) kabla hawajasababisha madhara mwilini.


Ripoti ya NPS na magonjwa mengine

Pamoja na wataalamu kuainisha magonjwa hayo, ripoti ya utafiti wa ufuatiliaji kaya (NPS) 2020/2021 imeorodhesha maradhi matano yanayoongoza kulaza wagonjwa hospitalini nchini ambayo ni Malaria (asilimia 0.7), matatizo ya uzazi (asilimia moja), homa (asilimia 0.4), tumbo (asilimia 0.6), mapafu (asilimia 0.2) na magonjwa mengine (0.9)

Pia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya mwaka wa fedha 2022/2023, ilionyesha magonjwa yasiyoambukiza katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022 yaliongoza kulaza wagonjwa hospitali.

Wagonjwa wanaotajwa ni wale wenye umri wa miaka mitano, ambao walilazwa kwa malaria takribani wagonjwa (76,834), kichomi (wagonjwa 65,904), magonjwa ya mfumo wa mkojo (wagonjwa 50,723), upungufu wa damu (wagonjwa 45,997) na shinikizo la juu la moyo (wagonjwa 43,974).

Kwa upande wa watoto, matatizo ya lishe ndiyo yanayoonekana kuwaandama zaidi na kwa hapa nchini yalionekana zaidi mikoa ya Lindi, nyanda za juu yaani Mbeya, Iringa na Njombe.

Kulingana na takwimu za lishe, Mkoa wa Iringa unaongoza kwa udumavu kwa asilimia 56, Njombe asilimia 50.4 na Mbeya asilimia 31.5.