Ndugulile: Tuwekeze maabara kupata vipimo sahihi, kuepuka UTI sugu

Ongezeko la wagonjwa wenye maambukizi ya njia ya mkojo, maarufu kwa jina la UTI na typhoid limekuwa kilio kikubwa kwa Watanzania katika sekta ya afya kutokana na kutumia fedha nyingi katika kutibu wagonjwa kutokana na usugu wa dawa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2017, nchi zinazoendelea, ikiwamo Tanzania zinaathirika zaidi na kiasi cha dola bilioni tisa za Marekani zitatumika kila mwaka kupambana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa hizo.

Ongezeko hilo linamuibua Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile ambaye anasema ongezeko hilo linafanya wagonjwa kupewa dawa za kutibu magonjwa hayo wakati hawakustahili.

Kwa mujibu wa Dk Ndugulile, ambaye ni daktari wa binadamu, utafiti uliofanyika na Hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2014 kwa watu 25,743 waliokuwa na dalili za homa ulibaini kuwa watoto waliothibitika kuwa na typhoid walikuwa asilimia 3.7, UTI asilimia 5.7, virusi mbalimbali asilimia 62.2 na malaria asilimia 10.5.

“Maana yake tunatoa dawa kwa watu hao ambao hawaumwi tatizo hilo,” alisema.


Kutambua magonjwa

Dk Ndugulile alisema ili daktari kufikia uamuzi kwamba mgonjwa anaumwa typhoid inachukua kati ya siku moja hadi tatu.

Alisema kwanza daktari anatakiwa kumwangalia mgonjwa, kuchukua vipimo na kuthibitisha kuwa anaumwa magonjwa hayo.

“Nasema hivyo kwa sababu inatakiwa uchukue kipimo cha damu na kwenda kukipandikiza maabara na hiyo inachukua saa 24. Ukiendelea kutambua vimelea na dawa inayoweza kutibu inachukua saa 72 ambayo ni siku tatu,” alisema Dk Ndugulile, ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto.

Alisema hatua hizo ni sawa na zinazofanyika kwa wagonjwa wa UTI, ambao huchukuliwa sampuli ya haja ndogo na kisha kwenda kupandikizwa maabara na ili iote inachukua saa 24.

Dk Ndugulile alisema baada ya hatua nyingine za kutambua vimelea na kupata dawa inaweza kuchukua siku mbili.

“Sasa hivi shida inakuja mtu anakwenda kwa daktari na ndani ya dakika 15 hadi 20 anaambiwa kuwa ana magonjwa hayo au malaria. Hii si sahihi,” alisema.


Nini kifanyike

Alishauri wataalamu wa afya warudi katika misingi ya utoaji huduma za afya kwa kuhakikisha matibabu yanafanyika baada ya uthibitisho kuwa mtu anaumwa ugonjwa gani.

“Ina maana tuwekeze katika maabara kuhakikisha kuwa vipimo vya maabara vinatumika katika majibu ya ugunduzi wa magonjwa, lakini pia katika kutoa matibabu,” alisema.

Alisema alilazimika kuandika katika mitandao ya jamii (Twitter), lengo likiwa ni kujengea uelewa wananchi kuwa wanapokwenda hospitali wasikubali kuwa wana magonjwa hayo kwa kuchukuliwa vipimo kwa dakika 15 hadi 20.

“Watanzania wanapokwenda hospitali tujenge utamaduni wa kuhoji pale unapoambiwa una UTI ama typhoid. Na ukiambiwa kila mwezi una UTI maana yake kuna kitu ambacho daktari ama tabibu hajabaini,” alisema.

Dk Ndugulile alisema katika utaalamu wa utabibu unatakiwa kutumia muda mwingi kumuangalia mgonjwa, kuzungumza na kumfanyia vipimo na kubaini chanzo cha tatizo na kufanya matibabu ya ule ugonjwa mtu anaoumwa.

“Watu wanakwenda hospitali na tatizo la virusi, ukimpa antibiotiki haponi, baada ya siku tatu anakwambia homa haijashuka, maana yake dawa hazijamsaidia kwa sababu umempa dawa ambayo hastahili na hujatatua tatizo hilo.

“Visababishi vya homa vipo zaidi ya 100, wewe umejuaje kati ya hivyo ni magonjwa hayo na dalili za magonjwa ya virusi, bakteria, fangasi na mabadiliko mengine ya mwili zinafanana,” alisema na kuongeza:

“Utapata homa na viungo vinauma, tafiti hazionyeshi kuwa hatuna tatizo kubwa la malaria wala magonjwa hayo,” alihoji.


Athari za matibabu yasiyostahili

Dk Ndugulile alisema madhara ya kupewa dawa za kutibu ugonjwa ambao mtu hana ni kutengeneza usugu wa dawa ambalo limekuwa tatizo kubwa nchini.

“Kwa sababu unamtibu mtu kitu ambacho alikuwa haumwi, kwa hiyo tunatengeneza usugu wa dawa na hivi vimelea ukivipa dawa sana vinazoea, kwa hiyo haviogopi dawa vinatengeneza usugu,” alisema.

Alisema hali hiyo inamfanya mgonjwa kutumia dawa kali na zenye gharama kubwa na hivyo kuongeza gharama za matibabu kwa mhusika.

Alitoa mfano mgonjwa alikuwa atibiwe kwa dozi ya Sh5,000, sasa inambidi kutumia dozi ya Sh30,000 hadi Sh40,000 atakapoumwa kwa sababu alipewa dawa zisizostahili.

Alisema dawa nyingine ni kali zaidi na hivyo zinaweza kuleta athari zaidi, ikiwemo matatizo ya figo ambayo baadhi wamekuwa wakiyapata kwa sababu watu wanakula dawa nyingi ambazo hawakustahili. Athari nyingine ni kuumwa zaidi, kulazwa na wengine kufariki dunia.


Kwa nini UTI hujirudia?

Dk Rachel Mwinuka alisema ili kujikinga na ugonjwa wa UTI, hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira yanayowaweka katika hatari ya kupata ugonjwa huo ni kuhakikisha choo ni kisafi na kumwaga maji mengi kabla ya kukitumia.

“Ni vema vyoo vinavyotumiwa na watu wengi kuhakikisha vinasafishwa mara kwa mara ili kuepusha watumiaji kupata ugonjwa huo,” alisema.

Alisema ili kuepuka kupata ugonjwa wa UTI ya mara kwa mara inashauriwa kuzingatia unywaji wa maji mengi na kujiepusha na kubana haja ndogo kwa muda mrefu.

“Baadhi ya watu kutokana na kuwa busy na kazi zao hujikuta wakijizuia kunywa maji mengi wakihofia kuhisi haja ndogo mara kwa mara na wengine wana tabia ya kuubana kwa muda mrefu. Tabia hizi hazishauriwi kitaalamu, kwani zinamuweka mtu katika hatari ya kupata UTI mara kwa mara,” alisema.

Alisema kuwa jambo jingine linalochangia watu, hasa wanawake kupata UTI mara kwa mara ni tabia ya kupaka vitu mbalimbali sehemu za siri, akitolea mfano wa manukato na mafuta, hivyo kutoa wito kwa wanawake kuacha tabia hiyo ili kujiepusha na kupata UTI ya mara kwa mara.

“Mwanamke anaweza kufanya jitihada za kujikinga na UTI, lakini kama ana tabia ya kuweka au kupaka vitu katika sehemu za siri bado ataendelea kulalamika kuumwa ugonjwa huo mara kwa mara,” alisema.

Aliongeza kuwa pale mtu anapojihisi dalili za ugonjwa huo, ikiwemo kupata maumivu wakati wa kutoa haja ndogo, kutoa mkojo wenye rangi ya chai na harufu kali, homa, maumivu ya kiuno na nyinginezo ni vema kuwahi hospitali kupatiwa matibabu na kujiepusha na unywaji wa dawa kiholela bila kufika hospitali.

“Kuna baadhi ya watu wanapohisi tu dalili za ugonjwa wa UTI hukimbilia kunywa dawa bila kwenda hospitali kufanyiwa vipimo na kupata ushauri wa daktari, hii ni hatari, kwani inaweza kukufanya kutopata tiba stahiki ambayo itasababisha ugonjwa huo kujirudia au kutengeneza usugu wa dawa,” alieleza.

Pia Dk Mwinuka alishauri watu kuzingatia uvaaji wa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa pamba na kuzingatia usafi wake kwa ujumla.