Madaktari bingwa wa saratani wapiga kambi ya siku tatu Kigoma

Badhi ya wananchi wa Mkoa wa Kigoma waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo Maweni kwa ajili ya uchunguzi wa saratani. Picha na Happiness Tesha

Muktasari:

Madaktari bingwa wa ugonjwa wa saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, wameweka kambi ya siku tatu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni kwaajili ya uchunguzi wa awali na matibabu ya saratani kwa wananchi wa mkoa huo.

Kigoma. Madaktari bingwa  kutoka katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) wameweka kambi ya siku tatu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni kwaajili ya uchunguzi wa awali, kutoa huduma na ushauri kwa matibabu ya saratani.

Akizungumza leo Alhamisi Aprili 6, 2023 na Mwananchi digital mjini Kigoma, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Saratani kutoka Taasisi ya saratani Ocean Road, Dk Crispin Kahesa amesema mbali na kutoa huduma hizo lakini pia watawajengea uwezo madaktari wa hospitali hiyo ili waweze kufanya uchunguzi wa awali wa saratani.

Kahesa amesema wameamua kwenda kigoma kwasababu mkoa huo upo pembezoni mwa nchi ya Tanzania na kwamba huduma za kibingwa na bobezi za ugonjwa wa saratani hazipo kwa wingi.

“Kigoma ni sehemu ambayo kwetu  ipo kimkakati na tunataka kuhakikisha kwamba tunapeleka huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani mkoa wa Kigoma na maeneo jirani lakini pia ni agizo la Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwamba wananchi wapate huduma hizi na iende sambamba na vifaa tiba na vya kibobezi,”amesema Kahesa

Amesema katika siku mbili za uwepo wa kambi hiyo, wamepima watu 405 kati ya hao wanawake ni 337 sawa na asilimia 83.7 na wanaume 68 sawa na asilimia 17.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Dk Lameck Mndengo amesema ujio wa madktari hao umekuwa muhimu kwao baada ya kujengewa uwezo katika upimaji wa awali wa saratani na matibabu jambo ambalo awali halikuwepo.

Dk Mndengo amesema hatua hiyo itakuwa endelevu kwa kuendelea kupeleka wataalam mara kwa mara kuwajengwea uwezo lengo ni  kuhakikisha madaktari wa hospitali hiyo wanakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa saratani wanaofika kupata huduma kwa ukaribu na sio hadi kutoka nje ya mkoa huo.

“Wananchi watafaidika kupata matibabu ya saratani wakiwa ndani ya mkoa katika hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma na itawapunguzia gharama za kusafiri kwenda Ocean Road labda kwa rufaa basi, kama watakuwepo wa kwenda huko ni wale wenye ulazima sana ila wengine wataishia hapa hapa kwetu,”amesema Dk Mdengo

Naye Mkazi wa Burega, Aidan Samwel aliyefika hospitalini hapo kupata huduma hizo amesema, kuwepo kwa madaktari hao kutaokoa muda wa mtu kusafiri kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam kwaajili ya matibabu.

huku ukisimamisha shughuli zao za kiuchumi lakini wakianza katika hospitali hiyo itakuwa rahisi kupata matibabu na kuendelea na shughuli zake za uzalishaji mali.

“Unaweza ukawa na dalili za awali za saratani lakini ukifikiria gharama za kusafiri na matibabu mgonjwa unashindwa kuchukua hatua kwaajili ya matibabu zaidi hasa kwa wananchi kama sisi wa hali ya chini na hatuna kipato kikubwa. Na kushindwa kujitibu kwa wakati kunaleta madhara makubwa baadaye,”amesema