Asilimia 90 ya Watanzania hawafikii kiwango cha ulaji matunda, mboga

Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia mazao ya mifugo, usalama wa chakula na lishe, Dk Nyamizi Bundala akizungumza leo Agosti 24, 2024 jijini Arusha wakati wa kongamano la kimataifa la wanasayansi wa mazao ya matunda na mboga lilishirikisha wadau kutoka nchi nane duniani.
Muktasari:
- Serikali ya Tanzania kupitia mpango kazi wa Taifa wa lishe, imelenga kupunguza asilimia za Watanzania wasiofikia ulaji wa matunda na mboga, kwa lengo la kusaidia kupunguza magonjwa yasiyoambukiza yanayochangiwa na ulaji usiofaa
Arusha. Watanzania zaidi ya asilimia 90 wanatajwa kutofikia kiwango cha ulaji wa matunda na mboga, hali inayotajwa kuongeza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza yanayochangiwa na ulaji usiofaa.
Serikali kupitia mpango kazi wa Taifa wa lishe wa sekta mbalimbali, umeweka malengo ya kupunguza asilimia ya Watanzania wasiotumia matunda na mboga kutoka asilimia 90 hadi kufikia asilimia 68 ifikapo mwaka 2025.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne Agosti 27, 2024, jijini Arusha na Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia mazao ya mifugo, usalama wa chakula na lishe, Dk Nyamizi Bundala.
Dk Nyamizi amesema hayo alipokuwa akizungumza katika kongamano la kimataifa la wanasayansi wa mazao ya matunda na mboga, lililoshirikisha wanasayansi 250 kutoka nchi nane.
Amesema ripoti ya lishe ya kimataifa ya mwaka 2022 ilibainisha idadi ya watu ambao wanashindwa kumudu lishe ya afya imeongezeka kutoka milioni 112 hadi kufikia bilioni 3.1 kote duniani.
Dk Nyamizi ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya kuratibu afua za kisekta katika mpango jumuishi wa lishe kitaifa, amesema kupitia mpango huo watashirikiana na wadau kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, idadi ya wasiomudu kula lishe ya afya unapungua kutoka asilimia hizo hadi 68.
Amesema bado Tanzania iko chini kwenye ulaji wa mboga na matunda licha ya kuzalisha kwa wingi, hivyo kupitia kongamano hilo, wadau watakuja na mikakati ya kuongeza ulaji huo ili kupunguza magonjwa yasiyoambukiza yanayochangiwa na ulaji usiofaa.
“Wakati huohuo, ulimwenguni kote magonjwa yasiyoambukiza yanayohusiana na lishe yamefikia asilimia 40 huku asilimia 20 ya watoto wote wakiwa wana uzito wa kupita kiasi,” amesema.
Dk Nyamizi amesema Tanzania imeweka kipaumbele katika kukabiliana na changamoto za utapiamlo kupitia mkakati wa miaka mitano kuanzia 2021/26, ambao umelenga kukabiliana na utapiamlo kwa namna zote na kwa rika zote.
“Na ina matokeo manne muhimu yanayolenga kupunguza lishe duni hasa kudumaa kutoka asilimia 31.8 mwaka 2021/22 hadi kufikia asilimia 24 ifikapo mwaka 2025/26 na maeneo mengine kwani chakula kinajitosheleza hapa nchini ikiwemo mboga na matunda, lakini ulaji wake ndiyo bado uko chini sana,” amesema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Mbogamboga na Matunda Bara la Afrika, Dk Gabriel Rugalema amesema umefika wakati wa nchi za Afrika kuendelea kutoa elimu zaidi kwa jamii juu ya umuhimu wa ulaji wa matunda na mboga.
Amesema ulaji huo utasaidia kupambana na magonjwa ikiwemo ya udumavu, uzito uliopitiliza na utapiamlo kwa watoto.
“Ulaji wa matunda na mboga kama ambavyo tumeona hapa bado ni mdogo kwenye maeneo mengi, wanasayansi wajipange na kuja na majibu zaidi ili kuhakikisha hali inabadilika na jamii inatambua zaidi umuhimu wa ulaji wa mboga na matunda ili kutunza afya zao,” ameshauri.
Dk Gabriel amesema kongamano hilo ni muhimu kwa Bara la Afrika, kwani wadau hao watajadiliana na kupeana mbinu za kuhakikisha wananchi wanalinda afya zao na watoto wao.
Mratibu wa mradi wa mboga na matunda kwa milo endelevu yenye afya (fresh) unaotekelezwa hapa nchini Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Mbogamboga na Matunda Bara la Afrika kwa kushirikiana na wadau wengine, Wiston Israel amesema mradi huo umelenga kuangalia mnyororo mzima wa mboga na matunda katika kuongeza ulaji, uzalishaji salama na kuongeza kipato.
Naye Profesa wa lishe kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Joyce Kinabo amesema tatizo la lishe nchini ni kubwa hasa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na waliopo shule, hivyo ni muhimu shule kuweka mifumo ya kuzalisha mboga ili zitumike kwa ajili yao.