Askari adaiwa kuua mtoto

Askari adaiwa kuua mtoto

Muktasari:

  • Mtoto Jastine James (14) amefariki dunia kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kupigwa na askari polisi Eliud Msangi. Tukio hilo limetokea Agosti Mosi, mwaka huu na tayari mazishi ya Jastine, mkazi wa Magore B Kata ya Mzinga wilayani Ilala, yamefanyika juzi kwenye makaburi wa Magore.

Dar es Salaam. Mtoto Jastine James (14) amefariki dunia kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kupigwa na askari polisi Eliud Msangi.

Tukio hilo limetokea Agosti Mosi, mwaka huu na tayari mazishi ya Jastine, mkazi wa Magore B Kata ya Mzinga wilayani Ilala, yamefanyika juzi kwenye makaburi wa Magore.

Hata hivyo, imedaiwa kuwa askari anayetuhumiwa kuhusika na mauaji hayo, Msangi hajachukuliwa hatua zozote za kisheria na yuko nje akiendelea na majukumu yake.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limethibitisha kupokea taarifa za tuhuma kwa askari wake na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea.

Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro alisema juzi kuwa ametoa maelekezo kwa Kamanda wa Mkoa wa Ilala afungue jalada ili uchunguzi wa malalamiko hayo uanze ili kutafuta ukweli wa jambo husika.

Alipoulizwa kama mtuhumiwa huyo amekatwa, Muliro alisema kwa sasa wanafanya uchunguzi kabla ya kumkamata.

“Taarifa za lalamiko hilo nimezisikia na nimemuelekeza Kamanda wa Ilala afungue jalada kuchunguza malalamiko hayo ili kufahamu ukweli na ikiwa ni kweli hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema Muliro.

Mwananchi limezungumza na baba mzazi wa Jastine, James Msira ambaye alidai kuwa Agosti Mosi saa 10 jioni alipigiwa simu kuwa kijana wake amepelekwa kituo kidogo cha Polisi cha Kitunda baada ya kupigwa na jirani yake, ambaye ni askari polisi, Eliud Msangi.

Msira alidai kuwa alikwenda kituoni hapo na kumkuta Justine akiwa taabani huku akitupa miguu yake, haraka alimfuata askari wa kituo hicho na kumuomba Justine ili aweze kumpeleka hospitalini.

Hata hivyo, alidai kuwa askari huyo hakuchukua hatua zozote na ilipofika saa 3 usiku Justine alipoteza fahamu na hapo ndipo akapewa karatasi ya matibabu (PF3) ili apelekwe hospitali.

“Nilipofika Polisi pale Kitunda nilimuona askari ambaye ninamfahamu na kumuuliza kwanini mtoto wangu yupo ndani huku hali yake ikiwa mbaya na mtu aliyefanya unyama huo amekamatwa, lakini sikupewa jibu,” alisema Msira na kuongeza:

“Ninavyofahamu huyu jirani yangu Msangi kituo chake cha kazi kilikuwa Polisi Keko, kwa sasa yupo Chuo cha Polisi Kurasini anasoma kupata nyota tatu.”

Alidai saa 3 usiku walianza safari kwenda Hospitali ya Rufaa Amana, wakiwa njiani aliaga dunia na walipofika hospitali madaktari walithibitisha kifo chake na kisha mwili huo kuhifadhiwa hospitalini hapo kwa siku nne na ilipofika Agosti 5, mwaka huu, mwili huo ulipelekwa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.

Wakati hayo yakiendelea alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Stakishari na kupewa RB namba STK/RB/7496/2021 taarifa ya kifo 01/8/2021 Jastine James umri miaka 14-Magole B.

Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mdogo wa Justine, Paulo James alidai siku hiyo saa 9 alasiri alikuwa anakwenda stendi na wakati anapita karibu na nyumba ya Msangi alisikia kelele za ndugu yake akiomba msaada na aliposogea eneo hilo alimuona mtuhumiwa huyo akimshambulia kwa kutumia gongo.

Alidai kuwa alimsogelea mtuhumiwa huyo na kumuomba aache kumpiga ndugu yake, lakini hakukoma na badala yake aliendelea.

“Baada ya kuona anazidi kumshambulia nilipiga kelele kuomba msaada zaidi na baadhi ya watu walijitokeza na hapo Justine alipata upenyo na kukimbia. Alielekea nyumbani na Msangi aliendelea kumkimbiza, lakini hakufanikiwa kumpata baada ya Justine kukimbilia ndani na kufunga mlango.

“Watu walijitokeza walimsihi kutomshambulia,” alidai Paulo.

Alisema baadaye alimpigia simu mama yake ambaye hakuwepo nyumbani kwa wakati huo na alipofika alimchukua Justine na kwenda naye Kituo cha Polisi cha Kitunda ili kupata PF3, lakini alipofika aliambiwa kuwa Msangi amefika hapo kufungua jalada, hivyo wakamuweka ndani Justine badala ya kumpa ruhusa kwenda kupatiwa matibabu.

Naye mkazi wa eneo jirani na wanapoishi kina Justine, John Juma alisema mtoto huyo aliyemaliza darasa la saba mwaka jana alitarajiwa kusafiri kwenda Mwanza kuanza masomo ya ufundi.

Pia, alieleza kushangazwa na madai ya askari huyo kujichukulia sheria mkononi badala ya kuwa mfano kwa jamii inayomzunguka.

“Huyu mtoto alikuwa mpole sana na hakuwa na tabia ya makundi mtaani wala wizi, hivyo tunashangaa kusikia amefanyiwa unyama kama huu hadi kusababisha mauti yake. Tusubiri tuone uchunguzi utasema nini lakini ni muhimu sheria na haki kuchukua mkondo wake,” alisema Juma.