Askari na mkewe wanaodaiwa kuiba umeme kizimbani kwa uhujumu uchumi

Thursday January 14 2021
askari nkizimbani pic
By Mussa Juma

Arusha. Askari polisi wa zamani, William Joseph (44) mkazi wa Muriet jijini Arusha na mkewe, Doricas Michael wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka matano likiwemo la uhujumu uchumi.

Joseph alikamatwa na mkuu wa Wilaya ya Arusha Januari 5, 2021 na siku chache baadaye alifukuzwa kazi.

Akisoma mashtaka leo Alhamisi Januari 14, 2020 mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Arumeru, Mary Mushi mwendesha mashtaka mwandamizi wa Serikali, Adelaide Kassalay amesema wanandoa hao wanatuhumiwa kuingilia mfumo wa ugawaji umeme.

Amesema walijiunganishia nishati hiyo kinyume na utaratibu na kuhujumu uchumi wa nchi. Amebainisha kuwa shtaka jingine ni kukutwa na mimea iliyozuiwa kisheria na pombe haramu aina ya gongo.

Shtaka jingine ni kutumia alama ya biashara kwa njia ya udanganyifu na kufanya Serikali kukosa mapato na kukutwa na vifungashio vya plastiki vilivyopigwa marufuku.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 27, 2021 huku washtakiwa hao wakirudishwa mahabusu.

Advertisement


Advertisement