Askari saba wafukuzwa kazi kwa kuvuka mpaka, kuingia Malawi

Askari saba wafukuzwa kazi kwa kuvuka mpaka, kuingia Malawi

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi limewafukiza kazi askari wake wa kituo cha Polisi Wilaya ya Ileje baada ya kukutwa na kosa la kuvuka mpaka wa Tanzania na kuingia Malawi wakiwa wamevaa sare za Jeshi na silaha za moto kinyume cha sheria.

Songwe. Jeshi la Polisi limewafukiza kazi askari wake wa kituo cha Polisi Wilaya ya Ileje baada ya kukutwa na kosa la kuvuka mpaka wa Tanzania na kuingia Malawi wakiwa wamevaa sare za Jeshi na silaha za moto kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, ACP Janneth Magomi amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya askari hao kufikishwa katika Mahakama ya Kijeshi Septemba 20, 2021 na kuwakutwa na hatia.

Magomi amesema kuwa Septemba 15, 2021, askari hao walikuwa wakitumia gari la polisi na wakati wakitekeleza majukumu yao walifika eneo la Kijiji cha Ikumbilo wilayani humo.

Alisema katika kijiji hicho walikutana na mwendesha pikipiki mmoja ambaye walimshuku kupakia mzigo wa magendo na ndipo walipoanza kumfukuzia kabla mtu huyo hajakimbia na kuvuka mpaka kuingia nchi jirani ya Malawi.

Alisema wakati wanamfukuza mwendesha bodaboda huyo, askari hao walikutana na kundi la wananchi wa Malawi ambao walianza kuwashambulia kwa mawe.

Kwa mujibu wa Magome, askari hao walijitetea kwa kupiga risasi hewani ili kuwatawanya wananchi hao wasiwadhuru.

Bosi huyo wa polisi aliongeza kuwa baada ya purukushani hiyo, askari wa Malawi katika kituo kidogo cha Ipenza walifika eneo la tukio na kutuliza ghasia hizo na kisha kuwashikilia askari wanne kati yao, huku wenzao watatu 3 wakitoroka.

Amewataja askari waliofukuzwa kazi kuwa ni Askari G.3695 D/SGT Ramadhani, H.694 PC Edward, H.8096 PC Safari, WP.12285 PC Anastazia, H.9727 PC Joseph, H.9781 PC Husein na H.8764 PC Jumanne.