Askofu aiomba serikali ipunguze gharama matibabu ya figo

Askofu wa Kanisa katoliki Jimbo la Geita Flavian Kasala akizungumza wakati wa uzinduzi wa idara ya magonjwa ya figo,mionzi,huduma ya dharura na huduma ya mtoto katika hospital teule ya halmashauri ya Wilaya ya Sengerema

Muktasari:

  • Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Flavian Kasala amesema gharama kubwa ya matibabu kwa wagonjwa wa figo imesababisha baadhi ya wagonjwa wanaotibiwa hospitalini kusitisha huduma kwa kushindwa kumudu gharama hivyo kupelekea vifo vya haraka ambavyo vingeweza kuzuilika.

Mwanza. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Flavian Kasala amesema gharama kubwa ya matibabu kwa wagonjwa wa figo imesababisha baadhi ya wagonjwa wanaotibiwa hospitalini kusitisha huduma kwa kushindwa kumudu gharama hivyo kupelekea vifo vya haraka ambavyo vingeweza kuzuilika.

Kutokana na hali hiyo Askofu Kasala ameiomba serikali kuona ni namna gani itawasaidia wagonjwa wenye tatizo la figo kupata huduma kwa gharama nafuu wakati huu ambao bado huduma ya bima ya afya kwa wote haijaanza.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa idara ya ya magonjwa ya figo, mionzi, huduma ya dharura na kitengo cha mama na mtoto katika Hospitali Teule ya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Askofu Kasala amesema serikali inawajibu wa kusaidia kwa namna moja au nyingine kupunguza gharama za usafishaji figo na huduma mbalimbali za matibabu.

Amesema wakati huduma za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo ikigharimu kati ya sh 240,000 hadi 300,000 kwa mzunguko mmoja Hospitali ya Sengerema inatoa huduma hiyo kw ash 180,000 kwa wagonjwa wale wasio na bima na wale wenye kipato duni lakini bado baadhi ya wagonjwa wameshindwa kumudu gharama hizo.

“Wakati serikali inafanya kazi ya kuhakikisha kila mmoja anapata fursa ya kuwa na bima ya afya iwe sambamba na kuwezesha wagonjwa kupata huduma za kibingwa na iwe bima rafiki hasa kwa wanaotoa huduma kama hospitali binafsi,“ amesema.

“Hali ya matatizo ya figo ni makubwa na yanaendelea kuongezeka,ni wajibu wetu kufanya uchunguzi wa afya mapema ili kupunguza tatizo katika mazingira yetu tupime mara kwa mara afya zetu na pale ambapo afya litatukumba  tusikate tamaa kwa kuwa huduma zipo”

Katika hatua nyingine Askofu Kasala ameiomba serikali kuipa hadhi ya Mkoa Hospitali ya Sengerema kwakuwa inavifaa na watoa huduma wa kutosha ili kuwapunguzia adha wagonjwa wanaolazimika kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza wakati ambao huduma hizo zinaweza kutolewa kwenye hospitali hiyo.

Awali, mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Marie Jose amesema tangu kuanzishwa kwa kituo cha kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo  mwaka mmoja uliopita watu 45 wanapata huduma  huku wengi wakiwa ni wagonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.
“Huduma hii ni rahisi kwa wenye bima za NHIF lakini kwa wagonjwa wasio na bima ni changamoto na sisi kama hospitali tumekuwa tukiwatoza gharama za matibabu pekee ambayo ni 180,000  ili kuwasaidia kuokoa maisha,” amesema.

Jose amesema endapo mchakato wa bima ya afya kwa watu wote utakamilika utasaidia na kuokoa maisha ya watu wengine na kwamba changamoto iliyopo ni wananchi wengi kutoelewa umuhimu  wa bima ya afya.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana amesema magonjwa yasiyoambukiza yanaathiri wananchi wengi kwa sasa na kwamba kama serikali na viongozi wa dini wanapaswa kuzungumza na wananchi masuala ya afya na namna ya kujikinga na magonjwa hayo.

“Miaka ya nyuma matibabu ya figo yalipatikana nje ya nchi na kwenye miji mikubwa kuzinduliwa kwa idara ya magonjwa ya figo kwa Sengerema itawasaidia wananchi wengi hasa wa vijijini wasio na uwezo kupata huduma na kuwapunguzia gharama za usafirii niwapongeze kwa hatua hii,” amesema.