Wakulima, wafugaji Kiteto watakiwa kuondoa tofauti zao

Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto, Mosi Sassy akiwaeleza wananchi wa Kijiji cha Olpopong umuhimu wa kufanya usuluhishi katika migogoro.

Muktasari:


  • Watakiwa kufahamu gharama wanazotumia za utatuzi wa migogoro ni kubwa, wafanye suluhu kabla ya kufika mahakamani.

Kiteto. Wakulima na wafugaji wilayani Kiteto mkoani Manyara, wameshauriwa kuondoa tofauti zao kwa kutumia njia ya suluhu ili kupunguza gharama za kufuatilia mashauri ya kesi mahakamani.

Migogoro mingi ina suluhu, kama vile kugombea mipaka, kudaiana, kulishia mifugo shambani, ndoa na talaka lakini makosa ya jinai kama vile mauaji, ubakaji, ulawiti haya hayana suluhu.

Wakizungumza na wananchi wa Kijiji cha Olpopong leo Januari 26, 2023 Wiki ya Sheria jopo la wadau wa sheria wakiwemo mahakimu, mawakili, ustawi wa jamii, Mkuu wa Dawati la Polisi, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa na wasaidizi wa kisheria (Parelegal) wamesema wengi wa wananchi Kiteto wanatumia muda mwingi kushughulikia kesi kuliko shughuli zingine za kiuchumi.

"Unaweza kukuta mtu ana kesi ya kuku lakini anauza ng'ombe...hili halifai unaweza kufanya suluhu tu na kuruhusu shughuli zingine ziendelea," alisema Joseph Kaaya (Paralegal)

Alisema migogoro mingi Kiteto inahusu ardhi, hapa kama wakulima na wafugaji wangetumia njia ya usuluhishi ingesaidia kufanya na shughuli zingine pia za maendeleo.

Wakili Ibrahimu Mohamed Masawe akiongea na wananchi hao alisema migogoro mingi Kiteto inasababishwa na kutokuwa na uelewa wa kutosha namna ya kuitatua huku akisema pamoja na kwamba yeye anawakilisha upande moja kwenye kesi hizo anashauri pande hizo ziwe zinafanya suluhu kwanza kabla ya kuingia mahakamani.

"Kama ulishauriwa vibaya na mtu kwenye mgogoro ukaenda Polisi ukajikuta umefika siku ya kwanza kesho yake ukipata fahamu ondoa suala hilo hapo Polisi jielekeze kwenye usuluhishi utatumia gharama kidogo kupata haki," alisema Wakili Ibrahimu.

Hakimu Mosi Sassy akiongoza jopo hilo alisema kaulimbiu ya wiki ya sheria mwaka 2023 ni umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuhishi katika kukuza uchumi endelevu, wajibu wa mahakama na wadau.

Alisema kama jamii watatumia njia ya usuluhishi katika migogoro yao uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na hata Taifa utaimarika hivyo hakuna sababu ya kugharamia mahabusu na wafungwa kwa upande wa Serikali lakini hakuna sababu ya kugharamia safari kufuatilia kesi.

Hakimu wa Mahakamaya Mwanzo, Kibaya Aron Kosioki alisema suluhu inafanyika popote pale ilimradi pande hizo zikubaliane na kuondoa mgogoro wao huky akiwasihi  wananchi wilayani Kiteto kuitumia kauli mbiu hiyo kikamilifu kuondoa tofauti zao.