Majaliwa mgeni rasmi Bunge Bonanza

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Muktasari:


  • Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ameeleza sababu za kuanzisha Bonanza la Michezo kwa wabunge na watumishi wa Bunge ikiwemo kula chakula kwa haraka.

Dodoma. Bunge limeanzisha utaratibu wa Bonanza la michezo kwa wabunge na watumshi wa Bunge yatakayofanyika mara nne kwa mwaka ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha mazoezi.

Akizungumza leo Januari 26, 2023, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema  bonanza hilo litanguliwa na maandamano yatakayoanzia Chuo cha Mipango saa 12.00 asubuhi Jumamosi (Januari 28,2023) na kuishia viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin.

“Kuanzishwa kwa Bunge Bonanza hatufuti ushiriki wetu katika michezo mingine ya kirafiki na michezo inayotukutanisha na wanamichezo wengine kutoka mabunge mengine ikiwa ni pamoja na michezo ya mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA),”amesema.

Dk Tulia ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM), amesema lengo kutoa fursa ya kuwakutanisha wabunge, watumishi wa ofisi ya Bunge na wadau mbalimbali katika mazingira ya nje ya ofisi na hivyo kuleta kufahamiana zaidi na kujenga umoja utakaosaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

Dk Tulia amesema katika bonanza hilo ambalo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kutakuwa na michezo 19 ikiwemo kukimbia na kijiko cha yai, kukimbia na glasi ikiwa na maji, kushindana kunywa soda na kula chakula haraka.

Amesema hata baada ya kumalizika kwa bonanza hilo anatarajia wabunge na watumishi wa Bunge watajiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kupunguza hatari ya kupata maradhi sugu yasiyoambukiza.
Naye Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Festo Sanga ameomba wakazi wa maeneo ya jirani kujitokeza katika bonanza hilo.

“Pia, tunakaribisha taasisi binafsi na Serikali ambazo ziko tayari kushirikiana katika mabonanza haya,” amesema Sanga ambaye pia ni Mbunge wa Makete (CCM).