Askofu anena na wachungaji wasiwe wasanii
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde, Geofrey Mwakihaba amewabariki wachungaji 17, akiwasisitiza kuacha usanii na kurejea kwenye misingi ambayo Mungu amewatuma.
Muktasari:
- Wachungaji wametakiwa kufanya kazi waliyoitiwa na Mungu kwa kuwajengea waumini imani ya kiroho ya kumtumikia.
Mbeya. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde, Geofrey Mwakihaba amewabariki wachungaji 17, akiwasisitiza kuacha usanii na kurejea kwenye misingi ambayo Mungu amewatuma.
Amesema hayo leo Jumapili, Januari 14, 2024 baada ya wachungaji hao kuhitimu masomo ya thiolojia katika hafla ya kuwabariki, iliyofanyika katika Usharika wa Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
“Idadi hii ya wachungaji ndani ya kanisa ikawe chachu ya kuwatumikia waumini kwa kuzingatia nini Mungu kawatuma na si kuwa wasanii. Fanyeni kazi mliyoitwa na Mungu kwa kuwajengea waumini imani ya kiroho katika kumtumikia Mungu,” amesema.
Pia amewataka kufundisha kwa usahihi neno la Mungu na kuwa faraja kwa waumini, kwa kuwa Mungu haangalii uzoefu bali wito waliotumwa.
Mchungaji Abel Mwaipaja wa Usharika wa Ngamanga Jimbo la Kusini, amewataka waumini kumuomba Mungu na kuwalea watoto kwenye njia ya wokovu yenye baraka ili kuwaepusha na vitendo viovu.
“Ni jukumu letu sote kuwatunza watoto kwenye misingi ya kimungu kwa kuwa na matendo mema, pia wazazi bebeni jukumu hilo ili kuwa na kizazi chenye kumcha Mungu,” amesema.
Mchungaji Solomon Mwakisyanju, ambaye ni miongoni mwa 17 waliobarikiwa amesema kwa hatua waliyofikia wanamshukuru Mungu na wako tayari kutumika katika kanisa lolote watakalopangwa kutoa huduma za kiroho.
“Sasa tuko tayari kutoa huduma za kiroho kwa waumini kwani ni mapenzi yake Mungu kufikia hatua hii ya kutumika kwa Wakristo ndani ya makanisa ya KKKT kama wachungaji,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa KKKT Dayosisi ya Konde, Benjamin Mbembela amewataka waumini hao kuungana kuimarisha miradi ya kanisa kama shule na hospitali ili liondokane na michango ya mara kwa mara.
Awali, ilielezwa idadi hiyo ya wachungaji waliobarikiwa itaziba mapengo kwa waliostaafu na baadhi waliofukuzwa kutokana na kuibuka kwa mgogoro ndani ya kanisa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Muumini wa kanisa hilo, Ester Joseph amesema ongezeko la wachungaji litaongeza chachu ya waumini kujengwa kiimani.